Thursday, 13 June 2013

Rasimu ya Katiba:Kilio changu kimesikika – Kasaka 


Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, John Malecela na Njelu Kasaka ambaye kwa wakati huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Iringa na marehemu Peter Siyovelwa (mwenye mavazi ya kijadi kulia)  Picha: Kwa hisani ya Frank Leonard
Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, John Malecela na Njelu Kasaka ambaye kwa wakati huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Iringa na marehemu Peter Siyovelwa (mwenye mavazi ya kijadi kulia)
Picha: Kwa hisani ya Frank Leonard.
Baadhi ya wananchi wameisoma na kuanza kutoa maoni yao, huku wengi wao, akiwamo mpiganiaji wa Seriali ya Tanganyika katika miaka ya 1990, Njelu Kasaka, wakionyesha furaha kwamba rasimu hiyo imesikiliza kilio chao.
Hata hivyo, Mchungaji Christopher Mtikila licha ya kilio chake cha siku nyingi kusikika, sasa ameibuka na madai mapya kama anavyoeleza katika makala haya.
Furaha ya Kasaka
Mbunge na Waziri wa zamani, Njelu Kasaka anasema kuwa ndoto zake kuhusu kuanzishwa kwa Serikali ya tatu ya Tanzania Bara (Tanganyika) zimetimia.
“Kwa kweli nimefurahi sana, yale maono yangu ya miaka ya 1990 hatimaye yameanza kutimia. Hiyo inaonyesha kuwa hata ukijaribu kuuzima ukweli, ipo siku utatimia tu, anasema Kasaka na kuongeza:
“Wakati ule tulipewa sifa mbaya ya kuvunja Muungano, lakini sasa ukweli huu umetuondolea sifa hiyo. Namshukuru Mungu kwa yaliyofanywa na Tume ya Katiba.”
Kasaka aliongoza orodha ya wabunge 55 maarufu kama G55 mwanzoni mwa miaka ya 1990 kudai Serikali ya Tanganyika, lakini hoja yao, lichas ya kupitishwa na Bunge, ilipingwa vikali na Mwalimu Julius Nyerere wakati huo akiwa rais mstaafu.
Kwa maoni ya Kasaka, muundo wa Serikali tatu utazivutia hata nchi nyingine kujiunga na Shirikisho la Tanzania, na kuipa nafasi Zanzibar nafasi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Muundo wa zamani haukutoa fursa kwa nchi nyingine kujiunga na Muungano wetu, lakini sasa inawezekana. Tukiingia kwenye shirikisho ndiyo itakuwa vizuri kwa sababu Zanzibar nao watapata fursa ya kushiriki, maana watakuwa na Serikali yao,” anasema.
Kasaka aliyekuwa Mbunge wa Lupa wilayani Chunya, Mbeya na kushika nafasi ya unaibu waziri wa kilimo mwaka 1994 hadi mwaka 1995, alisema kuwa kama Chama Cha Mapinduzi kiking’ang’ania hoja yake Serikali Mbili kitapoteza mwelekeo.
“Kama CCM watang’ang’ania mfumo wao wa Serikali Mbili watapoteza kwani kwa hali iliyokuwepo, isingewezekana tena kuendesha nchi. Hutakiwi kuendesha nchi kwa kulazimisha mambo,” alisema Kasaka na kuongeza:
“Hata hayo masuala ya mgombea binafsi na kupunguzwa kwa madaraka ya rais ni masuala tuliyoyapigia kelele lakini tukapuuzwa. Nimefurahi sana kwa kweli.”
Mtikila: Hakuna kitu…
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila ameendelea kuupinga mchakato mzima wa Katiba akisema kuwa unatetea Muungano unaonyonya Tanganyika.
Mtikila amekuwa mpinzani wa Muungano kwa muda mrefu, hali iliyosababisha chama chake kukosa usajili mwaka 1992 kwa kutoitambua Zanzibar. Hata hivyo, baadaye alilazimika kukubali kwa shingo upande.
“Kama kweli Watanganyika wanauthamini Muungano, na Uhuru wa Desemba 9, 1961 uliopiganiwa na kina Nyerere na Malkia wa Uingereza ukapotea, ndiyo maana leo Watanzania wanashindwa kufaidi rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu, kila madini yakigunduliwa wanapewa “wapumbavu”, anasema Mtikila.
Mtikila amekuwa akipigania haki ya mgombea binafsi kwa muda mrefu. Mwaka 1993 alianzisha harakati hizo alipofungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma akiiomba iruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi.
Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 24, 1994 na Jaji Kahwa Rugakingira, Mtikila aliibuka mshindi.
Hata hivyo, Serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini wakati rufaa hiyo ikisubiri usikilizwaji na uamuzi, Serikali ilipeleka muswada bungeni na kufanya marekebisho ya Katiba na kuweka ibara inayotamka kuwa kila mgombea ni lazima awe amependekezwa na chama cha siasa.
Februari 17, 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi nyingine Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba ya mwaka 1994.
Katika kesi hiyo alikuwa akiiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine, iamuru kuwepo kwa mgombe binafsi.
Katika hukumu iliyotolewa Mei 5, 2006, Mchungaji Mtikila aliibuka mshindi kwa mara nyingine baada ya Mahakama Kuu kukubaliana na hoja na maombi yake na kuwepo kwa mgombea binafsi.
Serikali ilikata tena rufaa katika Mahakama ya Rufani, ikipinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, iliyosikilizwa na jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufani Aprili 8, 2010.
“Hata hayo masuala ya mgombea binafsi na kupunguzwa kwa madaraka ya rais ni masuala tuliyoyapigia kelele lakini tukapuuzwa. Nimefurahi sana kwa kweli.”
“Unaposema umri wa kugombea urais usipungue miaka 40, lazima pia kuwe na kikomo. Isije ikawa kama Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye hana kikomo…” anasema na kuongeza:
“Suala la maadili nalo linapaswa kuangaliwa, kwani maadili hayapo tu kwa viongozi bali ni kwa Taifa zima. Tunawezaje kujenga Taifa letu kimaadili? Walichofanya ni kuibadilisha tu sekretarieti ya maadili kuwa Tume, kitu ambacho hakitoshi.”
Kuhusu muundo wa Muungano ambapo sasa kila upande utakuwa na Katiba yake na Bunge lake, alisema kuwa gharama za uendeshaji zitapungua hasa katika mabunge kwani idadi yao itapungua kulinganisha na sasa.
Kauli ya Shivji
Hata hivyo, gwiji la taaluma ya sheria nchini, Profesa Issa Shivji anatoa angalizo kuwa huu siyo wakati wa kusherehekea bali kuitafakari rasimu hiyo mstari kwa mstari ili kuhakikisha kuwa inakidhi haja ya wote.
“Kuna haja ya kuifanyia kazi rasimu hiyo kabla ya kuanza kusherehekea. Ndiyo kazi ninayoifanya ili kupata mwelekeo kamili,” anasema Profesa Shivji.
CHANZO: MWANANCHI
 

No comments:

Post a Comment