SMZ, UAMSHO sasa wafungamana
MSIMAMO wa asasi ya Uamsho Zanzibar kuhusu kupinga Muungano, unaungwa mkono na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), MwanaHALISI limeelezwa.Taarifa za ndani ya serikali na Baraza la Wawakilishi, zinasema kuna “mfungamano imara” kati ya serikali na Uamsho kuhusu Muungano.
Msimamo huo unaimarika sasa wakati Uamsho wakitoa tamko la kuridhia kuhamasisha Wazanzibari kutoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Uamsho “walilazimika” kubadili msimamo juu ya maoni ya wananchi kwa tume ili kutoudhi serikali.
Tume hiyo yenye wajumbe 30, 15 kutoka kila upande, inaongozwa na Jaji Joseph Warioba na tayari imeshatuma makamishna wake katika mikoa tisa kuanza kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya.
Lakini, Uamsho wamekuwa, siku zote, wakishauri wananchi kutokubali kujitokeza mbele ya tume hiyo; kwa madai kuwa Wazanzibari hawautaki Muungano.
Hatua hiyo ya Uamsho, kuacha msimamo wake mkali na kukubali kuhimiza wananchi kutoa maoni, inatokana na muafaka kati yake na serikali, zimeeleza taarifa.
Uamsho imekuwa ikishinikiza SMZ kuitisha kura ya maoni itakayotoa nafasi kwa Wazanzibari kuamua iwapo bado wanataka Muungano na siyo kutoa maoni juu ya katiba mpya.
Juzi, Jumapili kiongozi wa taasisi hiyo inayojumuisha asasi kadhaa za Kiislam za Zanzibar, alielekeza wananchi kujitokeza kwa tume ya Warioba na kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya.
Akitangaza msimamo huo mbele ya viongozi wa asasi za Uamsho, Amir Sheikh Farid Hadi Ahmed alisema, tamko hilo limetokana na muafaka waliofikia ukifuatana na “sababu kadhaa.”
Amir Farid ametoa sababu za kufikiwa kwa tamko hilo, ikiwemo ya imani yao kuwa kutoshiriki kutoa maoni ni “…kutoa mwanya kwa maadui wasioitakia mema Zanzibar wa kutusemea na kutoa maoni dhidi ya nchi yetu.”
Hoja nyingine ni kwamba kushiriki kwao kunatengeneza hoja ya vitendo ya kuwasilisha matatizo ya msingi yanayoiumiza Zanzibar, ambayo yanatokana na mfumo uliopo wa Muungano wa serikali mbili.
Amir Farid, katika hoja hii, ametamka wazi kuwa wanaiheshimu na kuiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) iliyo chini ya “uongozi imara wa rais wetu mpendwa Dk. Ali Mohamed Shein.”
Katika tamko lake, ameshutumu jeshi la polisi kwa kile alichoita vitendo vya kuvunja amani walivyofanya waumini wa kiislamu tarehe 17 Juni eneo la Mahonda, jimbo la Donge, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Siku hiyo, polisi walizuia, kwa kutumia risasi za moto, mabomu na vipigo vya mwilini, msafara wa wafuasi wa Uamsho uliokuwa ukienda jimbo la Donge kwa ajili ya mhadhara.
Inadaiwa watu wapatao 40 waliumia katika kukurukakara na polisi ambao wanadaiwa kuingia msikitini na kupiga waumini.
Katika hotuba zao majukwaani, viongozi wa Uamsho wamekuwa wakidai kuwa Muungano “umesababisha madhila makubwa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa Zanzibar.”
Moja ya mambo yanayotajwa kama madhila ya kiuchumi ni kile kinachoitwa “kuinyima Zanzibar mapato mengi kutokana na serikali ya Muungano kudhibiti njia zote kuu za kuingiza mapato serikalini.”
Zanzibar wanalalamika kuwa hawapati mikopo na misaada ya kimataifa; mapato yanayotokana na magawio ya faida za kibiashara katika mamlaka za ndani ya Jamhuri ya Muungano; na hakuna ushirikiano kati yake na mamlaka za kikanda.
Wiki chache zilizopita, Kamati Maalum ya Baraza la Mawaziri ilikutana na viongozi wakuu wa Uamsho na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu harakati za taasisi hiyo.
Kamati hiyo iliundwa na mawaziri wawili wa serikali, Abubakar Khamis Bakary (Sheria na Katiba) na Mohamed Aboud Mohamed (Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais), kamati ya Maridhiano iliyoratibu utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa kati ya CCM na CUF mwaka 2010 na vyombo vya ulinzi na usalama.
Taarifa ndani ya serikali zinasema, pamoja na majadiliano marefu yaliyofanyika, hakuna popote ilipotoka kauli kuwa Uamsho waache kuzunguka Unguja na Pemba na kuhamasisha wananchi kuukataa Muungano.
MwanaHALISI lilipomuuliza Amir Farid kuhusu hilo alisema, “Sisi tunafanya kazi kwa mipango ya taasisi zetu. Wasiotaka Muungano ni asilimia mia moja ya Wazanzibari. Lakini wapo wanaotusumbua na kuwashawishi polisi watupige mabomu. Hawana shida na maslahi ya wananchi wa Zanzibar moyoni.”
Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaundwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Wiki tatu zilizopita, viongozi wa umoja wa kitaifa walikuwa wakishutumiana, kila upande ukidai upande mwingine unaunga mkono Uamsho.
Katika majadiliano ndani ya baraza la wawakilishi, wajumbe wa vyama hivi wanatoa kauli za kulalamikia mfumo wa Muungano na kuilaumu serikali ya Muungano kwa kuikandamiza Zanzibar kiuchumi.
Wanasema kwa ufupi kuwa Muungano ulivyo sasa, unaionea Zanzibar na unaibana “kama vile koti linavyombana mtu; na wakati umefika sasa kwa koti hilo kuvuliwa.”
Ufuatiliaji wa gazeti hili katika mjadala wa bajeti ya SMZ umeona wajumbe kadhaa wakiitaka SMZ kuchukua maamuzi magumu kuiwezesha kupata walichoita “mapato yake stahili yanayonyonywa na Serikali ya Muungano.”
Orodha inaonyesha wajumbe waliogusa hoja hiyo kutoka CCM ni Salmin Awadh Salmin (Magomeni), Asha Bakari Makame (Viti Maalum), Mbarouk Wadi Mtando (Mkwajuni), Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), Ali Salum Haji (Kwahani), Makame Mshimba Mbarouk (Kitope) na Mansour Yussuf Himid (Kiembesamaki).
Wajumbe kutoka CUF waliogusa hoja hiyo ni Suleiman Hemed Khamis (Konde), Saleh Nassor Juma (Wawi), Hija Hassan Hija (Kiwani), Omar Ali Shehe (Chake Chake), Asaa Othman Hamed (Wete) na Ismail Jussa Ladhu (Mji Mkongwe).
Katika mahojiano maalum kwa njia ya simu na MwanaHALISI juzi Jumatatu, Jussa alitaja maeneo kadhaa yanayoingiza mapato kwa serikali ya Muungano lakini hayagawiwi kwa uwiano na Zanzibar.
Alisema maeneo hayo ni pamoja na mamlaka zilizoundwa kwa mwamvuli wa Muungano kama vile Shirika la Ndege (ATCL), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Shirika la Posta (TPC), Kampuni ya Simu (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na shughuli za bahari kuu na raslimali ya gesi.
Jussa alisema mamlaka zote hizo haziendeshwi kwa uwazi kiasi cha kuiwezesha SMZ kujua mapato halisi yanayopatikana kila mwaka. Mapato yote yanayopatikana kutokana na shughuli zake, alisema hayagawiwi kwa kuzingatia haki ya Zanzibar.
“Inasikitisha hata ile BoT ambayo ilianzishwa kwa SMZ kutoa mchango wa asilimia 11 ya hisa, haitoi gawio kwa kuzingatia ukweli huu. Haiwezekani utaratibu huu kuendelea,” alisema Jussa ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar.
Chanzo – Mwanahalisi
No comments:
Post a Comment