Sunday, 1 July 2012

HADIDU ZA REJEA ZA TUME YA MABADILIKO YA KATIB

HADIDU ZA REJEA ZA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Tarehe 6 mwezi wa Aprili, 2012, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; Sura ya 83.
Kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria hiyo, jukumu kuu la Tume ni kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Tume inaongozwa na Hadidu za Rejea kama inavyoainishwa katika kifungu cha 8 na kufafanuliwa katika kifungu cha 9 na 17 cha Sheria. Aidha, Tangazo la Serikali Nam. 110 la 2012 limefafanua zaidi Hadidu za Rejea hizo katika kifungu cha 4(3) kwa kujumuisha vifungu vya 18, 19 na 20 vya Sheria hiyo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kifungu cha 4(3) cha Tangazo la Serikali Nam. 110 la 2012, Tume inatakiwa kutekeleza yafuatayo:-
a) Kuandaa na kuendesha programu za kuelimisha juu ya madhumuni na majukumu ya Tume; {17(2)}.
b) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi; {9(1)(a)}.
c) Kuitisha na kusimamia mikutano au mabaraza katika sehemu na nyakati mbalimbali kama ambavyo itakavyoamua; {17(2)}.
d) Kutathmini na kuchambua kwa kutofautisha maoni ya wananchi yanayokubaliana na yale yasiyokubaliana; {17(2)}.
e) Kupitia na kuchambua michango, mawazo, maoni, taarifa na mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma; {17(4)}.
f) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora; {9)(1(b)}.
g) Kumtaka mtu yeyote atakaye hiari kufanya hivyo kwenda mbele ya Tume kufanya majadiliano, kwa mazungumzo au kuwasilisha nyaraka, kuhusu jambo lolote la kikatiba ambalo Tume inaona ni muhimu na linahusiana na mchakato wa mapitio ya Katiba; {17(3)}.
h) Kushughulikia jambo lolote kama itakavyoona inafaa katika kutekeleza majukumu yake; { 8(2)(c)}.
i) Kuchapisha Rasimu ya Katiba katika Gazeti la Serikali na magazeti mengine ili kutoa fursa kwa wananchi kusoma na kutoa maoni zaidi kwa Tume kupitia mabaraza ya Katiba; {(18(5)}.
j) kutayarisha na kuwasilisha ripoti itakayojumuisha:-
i. Muhtasari wa maoni ya wananchi kwa kila hadidu ya rejea 19(1)(a);
ii. Mapendekezo ya Tume kwa kila hadidu ya rejea 19(1)(b);
iii. Ripoti za wataalamu/washauri waelekezi ambao Tume iliwatumia 19(1)(c);
iv. Rasimu ya Katiba 19(1)(d); na
v. Taarifa nyengine yoyote muhimu 19(1)(e).
k) Kuwasilisha ripoti ya Tume kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar 20(1).
l) Kuwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge Maalum 20-(3).
Katika kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika Hadidu za Rejea, Tume itazingatia yafuatayo:-
a) Misingi 9(2)
Tume itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo:-
i. kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
ii. uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
iii. mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
iv. uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
v. umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
vi. uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura;
vii. ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu;
viii. utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria;
ix. uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu; na
x. kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo 9(3).
b. Nyaraka: 17(4)Tume itazingatia nyaraka mbali mbali zikiwemo:-
i. Nyaraka zote zinazowakilisha mawazo, maoni ya wananchi kwa ujumla katika Waraka wa Serikali Na.1 wa mwaka 1962 kuhusu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika;
ii. Azimio la Arusha la Mwaka 1967;
iii. Tume ya Rais Kuhusu Kuanzishwa kwa Mfumo wa Kidemokrasia wa Chama Kimoja;
iv. Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM ya mwaka 1983 kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979;
v. Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania ya mwaka 1991;
vi. Kamati ya Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba (Waraka wa Serikali Na.1 wa mwaka 1998);
vii. Katiba ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961;
viii. Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ya mwaka 1962;
ix. Hati za Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;
x. Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965;
xi. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;
xii. The Constitutional Government and the Rule of Law Decree, 1967;
xiii. Equality, Reconciliation and Unity of the Zanzibar People Decree, 1964;
xiv. The Existing Laws Decree, 1965;
5
xv. Confiscation of Immovable Property Decree, 1964;
xvi. The Legislative Powers Decree, 1964;
xvii. The Cabinet Decree, 1964;
xviii. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979;
xix. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984;
xx. Ripoti ya Pamoja ya Tume ya Fedha na Ripoti ya Shellukindo Juu ya Changamoto za Muungano;
xxi. Ripoti ya Wangwe Juu ya Uharakishaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki;
xxii. Tafiti za kiuchambuzi na kitaalam zitakazofanywa na Tume; na
xxiii. Nyaraka nyingine zozote ambazo Tume itaona ni muhimu.
Kwa kuzingatia Hadidu za Rejea zilizoorodheshwa, Tume itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kukusanya maoni ya wananchi na hivyo kupata matokeo yaliyokusudiwa

SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA vifungu 18,19 na 20

Mabaraza ya Katiba
18.-(1) Kutakuwa na mabaraza ya kutoa maoni juu ya Katiba.
(2) Mabaraza yatatoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba na kujadili na kutoa maoni kwa kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume.
(3) Mabaraza ya katiba yataundwa na Tume kwa muda maalum kwa kuzingatia mgawanyiko wa kijiografia wa Jamhuri ya Muungano na yatashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi toka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii.
(4) Mabaraza yanayorejewa katika kifungu kidogo cha (1) na katika vifungu vingine vya Sheria hii yatakuwa maalum kwa ajili ya, na yatahudhuriwa na raia wa Tanzania pekee.
(5) Kwa madhumuni ya kifungu hiki, Tume kabla ya kukamilisha ripoti itachapisha Rasimu ya Katiba kwenye Gazeti la Serikali na magazeti mengine ili kutoa fursa kwa wananchi kusoma na kutoa maoni zaidi kwa Tume kuhusu maudhui yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba
(6) Kwa madhumuni ya kifungu hiki, Tume inaweza kuruhusu asasi, taasisi au makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
19.-(1) Kwa msingi wa mahojiano na uchambuzi uliofanywa kwa kuzingatia vifungu vya 17 na 18, Tume itatayarisha ripoti itakayokuwa na:
(a) muhtasari wa maoni ya wananachi kwa kila hadidu ya rejea;
(b) mapendekezo ya Tume kwa kila hadidu ya rejea;
(c) ripoti za wataalam waelekezi ambao Tume iliwatumia;
(d) Rasimu ya Katiba; na
(e) taarifa nyingine yoyote muhimu.
(2) Rasimu ya Katiba itakuwa ni kiambatisho kwenye ripoti ya Tume.
20.-(1) Baada ya kukamilisha kazi yake, Tume itawasilisha ripoti kwa Rais na Rais wa Zanzibar.
(2) Rais, ndani ya siku thelathini na moja baada ya kupokea ripoti, atachapisha Rasimu ya Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kwa ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa.
(3) Rais baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, atamuagiza Mwenyekiti wa Tume kuiwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum.
(4) Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha (3), Mwenyekiti na wajumbe wa Tume wanaweza kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge Maalumu.

Muundo wa Tume ya Katiba na Vitengo Vyake

Vitengo Vya tume
Muundo wa vitengo ni kama ifuatavyo:-
(i) Uratibu wa Maoni ya Wananchi.
Kitengo hiki kina watumishi wafuatao:-
(a) Waratibu;
(b) Maafisa wa Hansard;
(c) Watafiti; na
(d) Waandishi.
(ii) Utawala na Rasilimali Watu.
Kitengo hiki kina watumishi wafuatao:-
(a) Maafisa Utawala;
(b) Maafisa Utumishi;
(c) Maafisa Usafirishaji;
(d) Maafisa kumbukumbu;
(e) Mtakwimu;
(f) Mkutubi;
(g) Katibu Muhtasi;
(h) Madereva; na
(i) Wasaidizi wa Afisi.
(iii) Kitengo cha Fedha na Uhasibu.
Kitengo hiki kina watumishi wafuatao:-
(a) Wahasibu;
(b) Afisa Mipango; na
(c) Mtunza Fedha.
(iv) Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.
Kitengo hiki kina Maafisa Ukaguzi wa Ndani.
(v) Kitengo cha Ununuzi.
Kitengo hiki kina Maafisa Ununuzi.
(vi) Kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji.
Kitengo hiki kina Maafisa wa Mawasiliano na Uhamasishaji.
(vii) Kitengo cha Tehama.
Kitengo hiki kina Wachambuzi wa Mifumo ya Kompyuta.

No comments:

Post a Comment