Chadema kuivaa CCM kuhusu Katiba mpya
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepanga kuijibu CCM kuhusu maamuzi ya Halmashauri Kuu (NEC) yao katika mchakato wa Katiba mpya ambayo CCM imedai kuwa muundo wa Serikali mbili lazima uwepo kwenye Katiba hiyo mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema wamepanga kufanya mkutano mkubwa Mei 26 mwaka huu maalumu kwa ajili ya kujadili mchakato wa Katiba mpya.
Mnyika alisema wameamua kwenda kwa wananchi kwa kuanzia Dar es Salaam kwa kuwa CCM katika matamko yao ya NEC wameonyesha kuwa hawana nia ya kuwa na Katiba mpya bali kufanya marekebisho ya iliyopo.
“Wanataka kuchakachua kama walivyosema kwamba wanataka muundo wa serikali mbili, hayo ni maoni yao na kila mtu anapaswa kutoa maoni yake hivyo watoe nafasi hiyo,”alisema Mnyika na kuongeza;
“Tutakuwa na Katiba mbovu badala ya Katiba mpya, tunataka wananchi wote wahusishwe na maoni yao yapewe kipaumbele.”
“Tutatumia nguvu ya umma kwa kuzungumza na wananchi kwa kuwa CCM imeshapoteza nguvu hiyo na wananchi hawaisikilizi,” alisema.Katika mkutano huo wa Mei 26 Mnyika alisema utahutubiwa na viongozi wote wakuu wa chama na wabunge mbalimbali wa chama hicho.
Alisema baada ya hapo Mei 28 mwaka huu wataanza kuunguruma mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kwa siku 15 mfululizo kuwahamasisha wananchi na kutoa elimu juu ya katiba mpya.
Kuhusu Shibuda
Mnyika alisema kuhusu matamko yaliyotolewa na Shibuda hiyo ni haki yake kidemokrasia lakini Chadema hakiwezi kikaruhusu demokrasia ikaleta ghasia.
“Kikatiba Shibuda ana haki ya kugombea nafasi yoyote ila hatuwezi tukaruhusu demokrasia tuliyo nayo ikaleta ghasia,” alisema Mnyika.
Alisema tayari chama kilishampa onyo Shibuda wakati wa kamati kuu ya chama na hilo liliweza kufanyika baada ya malalamiko kuwasilishwa kwa utaratibu.
“Hivi sasa hakuna mtu yeyote ndani ya chama aliyewasilisha malalamiko juu ya Shibuda hivyo hatuwezi kusema chochote. Utaratibu ni lazima malalamiko yawasilishwe ili yaweze kufanyiwa kazi,” alisema Mnyika.
Kuhusu bunge lijalo
Mnyika alisema wamejipanga kupeleka hoja mbalimbali za mambo yanayowahusu wananchi ikiwa ni pamoja na mfumuko wa bei unaowaumiza wananchi.
“Hoja hizo tutazizungumza na wananchi katika mikutano yetu na tukirudi bungeni tutazipeleka kama hoja tunazotaka zipewe hadhi ya kibunge,”alisema Mnyika.
Alisema pia watasimamia suala la katiba na migogoro mbalimbali inayowakumba wananchi hasa ardhi na suala la bodi ya mikopo.
Suala la Nyerere
Mnyika alisema hadi hivi sasa wanasubiri taarifa rasmi kuhusu kilichomkuta mbunge wao Leticia Nyerere huko Marekani baada ya kuripotiwa kuwa amekamatwa na ana kesi.
“Bado hatujapata taarifa rasmi lakini tumemwandikia na tunasubiri atakachotueleza tutakieleza kwenye umma,’alisema
No comments:
Post a Comment