Wednesday, 23 May 2012

CCM, yageuka paka, yatapika na kuramba



Elias Msuya
BAADA ya kuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na baadaye kuwa na semina kuhusu ‘Mwongozo wa CCM katika kushiriki mjadala wa Katiba mpya’ iliyofanyika mkoani Dodoma hivi karibuni chama hicho kimeibuka na maazimio yanayooneka kama ni kumeza matapishi yake.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais, uwezekano wa kuwa na Serikali tatu, kupunguza madaraka ya Rais, kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, kuwa na mgombea huru na kujadili kero za Muungano.

Kwa muda mrefu kumekuwa na shinikizo kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wanaharakati na wanasheria wamekuwa wakihoji kuhusu mambo hayo na hasa kuelekea katika Katiba mpya, huku chama hicho kikipinga.

Kwa mfano suala la mgombea binafsi limekuwa likipingwa na chama hicho kwa muda mrefu kwa hofu kuwa lingeweza kukiumiza pindi wanachama wake wanaposhindwa kura za maoni, kwani wangeweza kusimama binafsi na kushinda.

Suala la kupinga matokeo ya urais nalo limekuwa likilalamikiwa, lakini walalamikaji wamekuwa wakikosa nguvu kutokana na Katiba Ibara ya 41 (7) inayosema, “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais, hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Madaraka ya Rais wa Zanzibar nayo yamezua mjadala hasa kwa Wazanzibari wakihoji rais wao kushushwa hadhi.
Hayo yanatokana na mabadiliko ya 11 ya Katiba yalipomwondoa Rais huyo kutoka kuwa Makamu wa Rais na kubakia kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu Tume ya Uchaguzi, makundi mbalimbali yamekuwa yakishinikiza kuwapo kwa tume huru kwa madai kuwa tume ya sasa inaundwa na makada wa CCM wanaokipendelea chama hicho.

Kuhusu uteuzi wa mawaziri na Waziri Mkuu, kumekuwapo na maoni kutoka makundi mbalimbali kwamba mfumo wa Westminster wa kuteua mawaziri kutoka bungeni uachwe badala yake utumike mfumo wa mawaziri kuteuliwa nje ya Bunge ili kuwezesha uwajibikaji.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa Ibara ya 51 (2) Rais anaruhusiwa kumteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Lakini akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema mambo hayo yanahusu uendeshaji wa serikali na kutaka wananchi wapewe fursa ya kuchangia maoni yao kwa kadiri wanavyoona inafaa kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Ametaja mengine kuwa ni kuhusu muundo wa Bunge na Baraza la Wawakilishi na aina ya wabunge na wawakilishi, uwapo wa baraza la pili la kutunga sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, mfumo wa mahakama na nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Katiba

Licha ya kufunguka na kutaka mabadiliko yafanyike, Nape ameshauri mambo 15 kubakizwa katika Katiba kwa kuwa ndiyo misingi mikuu ya Taifa.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni muundo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwa wa serikali mbili yaani Serikali Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiongeza kuwa ni sera ya CCM isiyo na upungufu.

Mengine ni kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara katika vipindi maalum na kuzingatia haki ya kupiga kura kwa kila mtu mwenye sifa zinazohitajika kwa mujibu wa sheria, kuendeleza uhifadhi na ukuzaji wa haki za binadamu na kuheshimu usawa mbele ya sheria, kuendeleza sera ya dola kutokuwa na dini rasmi, bali inaruhusu kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoitaka mwenyewe.

Mengine ni kuendeleza sera ya serikali kuwa ndiye mmiliki wa rasilimali kuu za nchi, hususan ardhi, kuendeleza sera ya kuwapo kwa usimamizi madhubuti wa maadili ya viongozi kwa kuupa nguvu za kikatiba na kuimarisha madaraka ya umma.

Mengine ni kuhamasisha sera ya msingi ya kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine maalum katika jamii, kusimamia hifadhi ya mazingira na kuendelea kuwapo kwa Rais Mtendaji.

Kwa nini mabadiliko sasa?
Kutokana na msimamo huo mpya wa CCM ambayo zamani haikuwa nao, kumekuwa na hisia kwamba sasa chama hicho kimeanza kuhisi anguko hivyo kinajipanga kwa kutafuta ushawishi zaidi kwa wananchi.

Wakizungumza kuhusu hali hiyo, baadhi ya wataalamu wa siasa na wanasiasa wenyewe, wanasema hiyo ni dalili ya CCM kusoma mchezo wa mabadiliko yanayokuja siku za usoni hasa uchaguzi wa mwaka 2015.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Benson Bana anasema CCM kimesoma alama za nyakati.

“Hilo siyo suala la kushtuka, chama chochote cha siasa lazima kisome alama za nyakati za siasa, ndiyo maana utaona wamekubali hata suala la mgombea binafsi kama hivyo.”anasema Dk Bana.

Anaongeza kuwa CCM kimeshahisi homa ya mabadiliko nchini hasa nguvu ya upinzani inayokua kwa kasi na kutoa mfano wa Chadema.
“Kwa sasa kuna nguvu ya mabadiliko inakuja, kuna chama mbadala cha Chadema kwa hiyo lazima CCM kiwe ‘flexible’.”

Amengeza pia kwamba vyama vya siasa havipaswi kufungwa tu na itikadi na misimamo isiyovisadia kwani hufika mahali ikashindikana kutumika.

“Vyama vya siasa huunganishwa na itikadi zao, lakini wananchi hawaangalii itikadi, wao wanaangalia nani kafanya nini, kwa hiyo kung’ang’ania itikadi ni kufanya kosa,” anasema na kuongeza,

“Kwa mfano watu kama kina Shibuda (John) wangeweza kuhama CCM na kuwa wagombea binafsi kama wangeruhusiwa. Nadhani haya ni maendeleo mazuri kuliko kung’ang’ania misimamo ambayo hailisaidii Taifa.”

Kwa upande wake mhadhiri wa Chuo Kikuu Guria cha Tanzania Emmanuel Mallya, anasema tatizo la CCM ni ukongwe hivyo kinatafuta kujiepusha na matatizo yote yanayoelekezwa kwake.

“Tatizo la CCM ni ukongwe wa chama kma vilivyo vyama vingine vya muda mrefu kwa hiyo kila tatizo la nchi hii wanahusishwa nalo. Halafu hayo mabadiliko ambayo tunaita ni mabadiliko ya sura tu, kwa sasa yanahitajika mabadiliko kwenye chama na serekalini.”anasema Mallya.

Mallya anaonyesha wasiwasi kama kweli CCM kinadhamira ya kweli kukifanya kuwa chama cha wananchi wote, au ni yale yale ya kulindana?

“Je, katika mabadiko wanayofanya wanahusisha kukipeleka chama kwa wananchi? Jiulize wewe mwenyewe ni rahisi kugombea nafasi ya uongozi kupitia CCM kama si Mnauye, Mwinyi, Nyerere, Kikwete, Malecela au Mzindakaya?” anahoji Mallya.

Naye kada wa muda mrefu wa CCM Dk Hassy Kitine anasema kinachofanyika ndani ya CCM ni upanuzi wa demokrasia kutokana na kupanuka kwa demokrasia ndani ya chama na nchi kwa ujumla

“Mabadiliko ya CCM kama kuhoji madaraka ya Rais ni kupanuka kwa demokrasia ndani ya chama na nchi kulingana na hali ya siasa ya nchi” anasema Dk Kitine.
Ameongeza kuwa hali ya siasa imebadilika huku nguvu ya upinzani ikikitisha chama hicho kikongwe.

“Vyama vya upinzani ni vikubwa, ‘that’s obvious’, vimepanuka mno, lakini hata ndani ya CCM yenyewe kwa wanachama na wasio wanachama, wote wanataka demokrasia. Siyo kwamba CCM kimekuwa kikizuia demokrasia siku zote, hapana ni mabadiliko ya kupanuka tu kwa demokrasia,” anasema Dk Kitine.

undefined









 .





 .

 .

 .



 .





 .

  







No comments:

Post a Comment