Tuesday, 1 November 2011

Jaji Warioba: Tusidanganyane, kutaka Serikali tatu ni kuvunja Muungano

Serekali 3 nikuvunja Muungano asema Warioba
Posted on November 1, 2011 by zanzibar yetu
Mwandishi Wetu
■Asema ndani ya vyama vya siasa hakuna demokrasia ya kweli
■Ataka watu wadai demokrasia kwanza, si mabadiliko ya uongozi
■Ahoji nia ya wanasiasa kukimbilia kwa mabalozi na mantiki ya uhuru
OKTOBA 10, mwaka huu, Waandishi Wetu, walifanya mahojiano na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, kuhusu masuala mbalimbali, ikiwamo maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, Katiba mpya ya Tanzania na hali ya kisiasa nchini. Yafuatayo ndiyo yaliyojiri.
Raia Mwema: Nini ni maoni yako kuhusu yaliyojitokeza katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga?
Jaji Warioba: Igunga kwa maoni yangu, maandalizi yalikwenda vizuri kwa maana ya Tume ya Uchaguzi kujiandaa. Na hata kwa vyama vya siasa. Nadhani vilikuwa vimejiandaa vizuri kwenda kwenye kampeni Igunga.
Na kampeni kutokana na taarifa za vyombo vya habari, nadhani, wananchi walikuwa tayari kwa sababu walikuwa na hamasa, walihudhuria mikutano ya vyama vya siasa kwa wingi tu.
Kwa ujumla sikuwa na matatizo na maandalizi, lakini jinsi kampeni ilivyokwenda na jinsi tulivyofikia mwisho hali haikuwa ya kuridhisha sana.
Kumekuwa na kukosoa kwamba wananchi hawakupata elimu ya kutosha kwa wapiga kura kuweza kujitokeza. Mimi siamini kama ni suala la wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha, lazima kuwe na sababu.
Raia Mwema: Ni sababu gani hizo?
Jaji Warioba: Kwa kawaida mahali popote duniani, kwa uchaguzi mdogo, huwa ni jambo la kawaida wapiga kura hawajitokezi sana. Lakini kwa Igunga walijitokeza kwa wingi ukilinganisha na wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Katika Uchaguzi Mkuu waliojitokeza walikuwa 49,000 safari hii wamejitokeza 53,000. Kwa hiyo, kwa mazingira ya uchaguzi mdogo walijitokeza wa kutosha lakini ni kweli hawa waliojitokeza ni kama asilimia 30 tu ya waliojiandikisha.
Kwa hiyo, waliojitokeza ni wachache sana na hasa ukizingatia kwamba kampeni za Igunga zilikuwa na uzito mkubwa. Vyama, na hasa, vile vikubwa vilipeleka nguvu kubwa sana Igunga kwa maana ya watu waliokwenda kule na rasilimali iliyotumika. Vile vyama vikubwa vimepeleka viongozi wa ngazi ya kitaifa. Si mmoja ama wawili, ni wengi tu wamekwenda Igunga. Ukitazama nyenzo za kufanyia kazi, Igunga ilikuwa na magari mengi, pikipiki na helkopta.
Vyama vitatu vilipeka helkopta kule. Hiyo ilikuwa ni nguvu kubwa. Fedha iliyotumika hata ukitumia taarifa za baadhi ya vyama, ilikuwa ni kubwa kupita ile inayoruhusiwa kisheria.
Kwa mazingira hayo, ungetarajia kwa kuwa viongozi wengi wamekwenda kwenye jimbo moja tu na wamepita kila mahali, wapiga kura wengi wangejitokeza, lakini haikuwa hivyo. Wamejitokeza wachache.
Na hii ni reflection (mwangwi) ya yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu ambao walikuwa wachache sana ukilinganisha na daftari la wapiga kura. Kuna mengi yamezungumzwa na wengine wamelaumu Tume kuhusu hali hiyo.
Wanasema kwamba kama ingekuwa Tume huru watu wangejitokeza. Lakini huoni mahali ambapo unaweza kuunganisha kazi za Tume na kujitokeza kwa wananchi.
Kwa sababu kuhamasisha wapiga kura waende kupiga kura ni kazi ya vyama vya siasa, si kazi ya Tume.
Tume inatoa elimu ya mpiga kura kwa maana ya kanuni na taratibu, lakini kuwafikisha wapiga kura kwenye vituo ni kazi ya vyama vya siasa. Ukichukulia hii pamoja na mwaka jana hapa kuna upungufu kwa upande wa vyama vya siasa.
Raia Mwema: Lakini vyama ya siasa vinasema vyenyewe vimefanya kazi ipasavyo kwa kuendesha kampeni kubwa kuliko iliyopata kushuhudiwa katika uchaguzi mdogo huko nyuma?
Jaji Warioba: Nilichokiona Igunga inaonekana wananchi wapo katika makundi mbalimbali wapo ambao nadhani waliogopa kwa sababu ya aina ya kampeni ilivyokuwa Igunga.
Igunga ilikuwa na matukio ambayo kwa kawaida yangeweza kumuogopesha mtu wa kawaida. Ukiona mahali kuna kampeni kisha ukaona kuna silaha hiyo tu inaweza kuogopesha watu.
Ukiona kuna matukio ya kumwagiana tindikali, matukio ya kukamata viongozi, kwamba vyama vya siasa vinakwenda kukamata DC (Mkuu wa Wilaya) kwa vyovyote hiyo inafanya baadhi ya watu wapate wasiwasi kwamba siku ya uchaguzi itakuwaje.
Lakini wapo ambao hawakwenda kupiga kura nadhani kwa kuona mwenendo wa kampeni, kuwa lugha inayotumika ni ya malumbano tu, huoni kama umuhimu unawekwa kwenye sera, inakuwa ni lugha ya kashfa, kejeli.
Kuna wananchi wanaangalia viongozi, wanataka kiongozi, lakini kama ni aina hii kuna wengine nadhani wanaanza kuwa na imani ndogo na uongozi kwa hiyo wanaona haya yote yanayosemwa hakuna maana ya kwenda kupiga kura. Nadhani wapo wapiga kura wanavyoona mtindo wa kampeni tulionao si wa kutafuta viongozi ambao wangeweza kusaidia.
Lakini pia unaona kuna kama element kwamba badala ya kuzungumzia demokrasia kwa maana mnataka kuchagua kiongozi, lugha inayozungumzwa ni ya aina ile ambayo imekuwa kama sasa ni mtindo duniani: badala ya demokrasia tunazungumza regime change (mabadiliko ya uongozi).
Hii regime change inaanza kuingia kwenye siasa zetu, kwa hiyo unakuta wale ambao wana madaraka wanataka kuzuia regime change wale ambao hawana madaraka wanataka regime change na hiyo inaingia kwa wananchi, tunapotosha ile demokrasia na wananchi hawakuzoea hivi.
Nadhani kuwa wengine wanaweza kuona kwamba hapa labda nataka mabadiliko. Kuna wengine wanataka mabadiliko tu yatokee labda kwa sababu Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kwenye uongozi muda mrefu, hawaangalii sera wala nini wanataka tu kiondoke.
Lakini inawezekana wananchi wakaona kama tunataka mabadiliko nani tunamleta (kumchagua kwenye kiongozi). Wakajiuliza hivyo na wakakosa mbadala kwamba pamoja na kwamba wanataka mabadiliko lakini hakuna mtu. Kwa hiyo wanasema kwa nini nijihangaishe, anabaki nyumbani haendi kupiga kura.
Kwa mwenendo huu hawatakuja kupiga kura, hata useme wananchi hawa hawana elimu ya kupiga kura ukweli ni kwamba hiyo si sababu kubwa.
Sisi hapa tunayo rekodi ya wananchi huko nyuma ambao hata wengine hawajui kusoma wala kuandika lakini walikuwa wanaelewa elimu hiyo na walijitokeza kwa wingi.
Raia Mwema: Inawezaka pia kwamba pengine wananchi wameanza kupoteza imani na vyama vya siasa?
Jaji Warioba: Sasa hivi ni lazima kuna mambo ya kisiasa na nafikiri matatizo yapo kwenye vyama vya siasa.
Haviwapi matumaini wananchi. Wameanza kuwa na wasiwasi, kwa hiyo, wameanza kupoteza imani na mfumo wa vyama vya siasa.
Vyama vinaweza kulalamika na vikatafuta makosa madogo madogo, lakini nadhani viangalie mfumo wetu wa siasa na wapi tunatia mkazo kama kweli hayo tunayosema yanawaingia wananchi.
Kwa mawazo yangu, nadhani wananchi hawana imani kama waliyokuwanayo mwazo, hili si la Igunga tu, hata kwenye uchaguzi wa mwaka jana.
Lakini wapo wengine wanakwenda kwa matumaini ya kupata chochote kwa wakati huo. Kwamba ukiona tunatumia fedha nyingi sana katika uchaguzi na kuna watu wanajitokeza ili wafaidi kwa hiyo itakuwa wengine wanataka kuwa mawakala.
Kwa hiyo, vyama vya siasa viangalie. Ni kweli vinazungumza juu ya Tume, lakini hivi kweli hili ndilo tatizo kubwa. Tutazungumza inatakiwa Tume inayoaminika, ni kweli.
Lakini hata huko nyuma kama unazungumzia majina yasiyoonekana hata wakati huo tatizo hili lilikuwapo. Lakini pia tujiulize hayo majina yanayokosekana ni sehemu kubwa kiasi gani katika idadi ya wapiga kura?
Jingine kuhusu Tume ni kwamba imechelewa kutoa matokeo. Ni kweli lazima tujitahidi matokeo yatoke mapema lakini huko nyuma mbona ilikuwa inachukua muda mrefu? Leo kuna maendeleo fulani.
Kwangu haya si matatizo ya kimsingi kama ilivyo kwenye mwenendo wa vyama vya siasa. Ni lazima vyama hivi vifanye kazi kuleta imani kwa wananchi waweze kuthamini uchaguzi.
Raia Mwema: Ukichukua matukio ya Igunga na hali ya jumla ya siasa nchini, kwa maoni yako, nchi inakwenda vizuri?
Jaji Warioba: Tumepiga hatua kubwa sana. Kwa kiwango kikubwa nadhani tumekwishakuzoea mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hii ni hatua kubwa. Lakini vyama vyetu havijaingia katika utaratibu rasmi wa kushindana katika siasa za vyama vingi.
Tatizo moja ni kwamba vyama vyote havina mwelekeo. Unapowasikiliza unajiuliza hawa sera yao ni nini? Sera hazipewi umuhimu.
Tunatumia matukio katika mfumo huu wa mabadiliko ya uongozi. Niliona kwenye vyombo vya habari, ikitokea jambo lolote katika nchi fulani, swali linakuja tumejifunza nini kutokana na hilo?
Kwa hiyo ikija regime change unasema tumejifunza nini kutoka Tunisia, kutoka Misri, Libya au Yemen.
Baada ya uchaguzi wa Zambia ni hayo hayo. Ukisoma makala nyingi utaona ziko katika mfumo huo. Badala ya demokrasia tunashabikia mabadiliko ya uongozi.
Niliona kwa kiwango kikubwa kusema tujifunze nini Zambia ni kwa kuwa MMD (chama tawala) kilikuwa kimekaa madarakani miaka 20. Kwa hiyo MMD kutolewa ni funzo na kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwatoa walioko katika utawala.
Ningedhani tungeulizana tumejifunza nini kutoka Zambia kwa kupima hawa wanaotoka au kuingia ni kipi ambacho wameleta kipya ambacho mna matumaini hali za wananchi zitabadilika. Kwangu kutoka tu ni mafanikio.
Na vyama vyetu hivi ni kama viko hivyo. Kwanza kuna matatizo karibu vyama vyote. Tatizo moja kubwa ni kuwa vyama hivi vimebaki ni vyama vya viongozi.
Wanachama wa kawaida hawana nafasi sana. Ni vyama vya viongozi, kwa hiyo focus ni kwenye uongozi, kubadili uongozi siyo kubadili hali za wananchi.
Kwa hiyo kwa kiwango kikubwa hali hiyo iko katika vyama vyote kwa ndani, kwa maana ya msukumano wa ndani ya vyama vyenyewe, hakuna chama ambacho unaweza kusema msingi wake ni wanachama. Kwamba wanachama wakisema wanataka hiki, hicho ndicho kitakachofanyika.
Utaona matatizo yako kwenye uongozi. CCM wako kwenye matatizo ya uongozi na unaona hata Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaanza kuingia katika matatizo ya uongozi. Wanayozungumza unaona yanahusu zaidi uongozi.
Wasiporekebisha hili, vyama vikarudi kwa wanachama, vyama vitayumba. Kwa sababu wasisahau wanachama wana nguvu sana, hasa ukifika kwenye uchaguzi. Ukiwa una nguvu ya wanachama wakapigania chama chao katika ngazi ya chini kabisa, chama hicho kitakuwa na nguvu. Lakini kama wanachama wanapigania makundi ndani ya chama, chama hicho hakiwezi kuwa na nguvu na hili lipo, kwa kiwango kikubwa linaonekana ndani ya CCM, lakini kuna dalili linaanza kujionyesha kwenye vyama vingine pia.
Sasa hivi, vyama vyote nguvu wameziweka katika kamati kuu na halmashauri kuu. Wakiamua huko wanasema chama kimeamua ingawa si kwamba uamuzi husika umetokana na wanachama.
Kwa hiyo, vyama hivi visipofanya mageuzi ya ndani, vikarudi kwenye msingi kwamba nguvu ya chama ni wanachama si viongozi, utaona mwenendo huu wa wananchi kujiondoa katika hali ya kawaida ya kutetea vyama vyao hadi inapofika wakati wa uchaguzi wanakwenda kwa sababu mbalimbali lakini si kwa sababu ya chama.
Nikiangalia hali ya kisiasa inaathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya nchi. Siku hizi tunazungumza sana juu ya siasa, hatuzungumzi mambo ya uchumi na huduma za jamii kwa kiwango kinachotakiwa. Tumefika mahali unaona mambo yale ya kisiasa ndiyo yanatiliwa mkazo.
Kwa mfano, Dowans imekuwa ni suala la kisiasa hivi. Ni suala la kisiasa kwa manufaa ya wanasiasa lakini kwa kutumia jina la wananchi. Ni mapambano ya wao kwa wao, ama ndani ya vyama au kati ya vyama. Ni mapambano yao kwa kutumia mgongo wa mwananchi.
Mpaka sasa sijaelewa watapata faida gani kuliendeleza hivi. Tupende tusipende uamuzi ule wa Dowans ni kweli kwamba wote unatuuma, kwamba Taifa litapoteza fedha lakini mimi naamini wote wale wanasema kisiasa.
Wanajua hawawezi kubadili chochote. Wanayofanya sasa hivi ni ya malengo ya kisiasa na yatakuja kuligharimu Taifa kiwango kikubwa zaidi cha fedha kuliko kilichoamuliwa na Mahakama (ya Kimataifa).
Ile Mahakama walipotoa hukumu ilikuwa Tanesco walipe bilioni 94, sasa wamezuia hapa utekelezaji ule, wamekwenda mahakamani kuzuia utekelezaji na fedha imeongezeka sasa imefika bilioni 111, kama wanaendelea ikazuia hatua zisichukuliwe kukubaliana namna ya kulipa itakapofika wanalazimishwa kulipa inaweza kuwa kubwa zaidi. Hivi nani atakuja kuhusika na hili, kwa vyovyote vile tutalipa lakini kwa sababu ya haya mambo ya kisiasa, yataligharimu Taifa kiasi kikubwa zaidi huko mbele. Tutakuja kutafutana zaidi nani amehusika kutufikisha hapo.
Lakini mimi ningependa tuangalie hasa hali ya uchumi. Huko nyuma Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akisema fedha si msingi wa maendeleo, ni matokeo. Sasa hivi tunaona fedha ndiyo msingi wa maendeleo na wote sasa tunatazama fedha ili tupate mwanya wa kusema kuna ufisadi hapa ili uwe mtaji wa kisiasa.
Hatuangalii yale mambo yanayoweza kutufanya kujiongezea fedha. Uchumi wanasema unakua lakini tunaona maeneo ambayo uchumi unakua. Nadhani unakuwa kwenye ujenzi, madini na utalii.
Mahali ambako ungesema kama kuna kukua kwa uchumi ambako kutabadili hali za wananchi ni kwenye kilimo, kwa sababu masikini wengi wanategemea kilimo ambacho kisipokua umasikini unaongezeka.
Ni kweli nakubali tupige vita ufisadi lakini kama ni ufisadi tu bila kuweka mkazo kwenye maeneo haya umasikini utazidi. Hakuna anayechambua hali ya kukua kwa uchumi, mkulima mdogo ni lazima apate mambo fulani.
Lazima umsaidie gharama zake za kuzalisha zisiwe kubwa sana kama ilivyo sasa. Lakini si hilo tu, usipompa soko la hakika hawezi kujiondoa kwenye umasikini.
Kuangalia mahitaji ya mkulima hasa mdogo ni muhimu sana. Wakulima wakubwa huko wanaendelea kupewa ruzuku, kwa nini sisi hatuangalii hili kwa upana zaidi?
Kwa kadiri tunavyopata matatizo au upungufu wa chakula ndiyo inflation itakuwa kubwa zaidi. Kilimo ni suala la kuangalia sana, viongozi wetu wakae watafakari haya masuala mazito, umeme, suala la chakula na mafuta ambavyo matokeo yake ni kuanguka kwa shilingi na kusababisha mfumuko wa bei.
Lakini hali ilivyo si hivyo, viongozi wengine sasa yatapotokea matatizo badala ya kukaa kwa pamoja na kutafakari, wanayatumia kama mtaji wa kisiasa. Hali hiyo haimalizi tatizo la mwananchi. Sasa tuna hili la umeme wajue wananchi wanaumia sana hasa wale wenye shughuli ndogo ndogo.
Tumebaki kuchukua eneo moja kisiasa la ufisadi ambalo ni mapambano kati ya viongozi lakini hatujatia umuhimu kwa mambo mazito yanayomhusu mwananchi. Hiyo ndiyo hali ninavyoiona.
Raia Mwema: Baada ya matokeo ya Igunga, hasa baada ya kufanya vibaya huko kwa Chama cha Wananchi (CUF), yamezuka maoni kwamba wingi wa vyama vya upinzani si muhimu, kwamba kuwe na vyama walau viwili tu vya upinzani ili vipambana vyema na chama tawala, hili linawezekana?
Jaji Warioba: Kuwa na vyama vingi hainipi matatizo. Vingine vitakuwapo kwa majina na hivyo vipo, na vingine ni watu tu, mtu akitoka chama nacho kimekwenda.
Kwa hiyo vyama vingine ni watu, si vyama. Unaona ni wale wale na hawafanyi mikutano. Vipo tu kwenye orodha ya usajili lakini hakika si vyama vya siasa.
Kwa hivi vinavyotajwa kuwa ni vyama vikubwa vilivyopo viangalie kama nilivyosema, kuna watu wanaotaka mabadiliko ya utawala. Ni ukweli ukiwa kwenye uongozi muda mrefu kuna watu watataka mabadiliko.
Kuna watu wanaangalia mwenendo wa chama na vyama vyote hivi ukiangalia kati ya mwaka jana na sasa hata hivi vyenye nguvu sasa, wananchi wakati mwingine wanasema hapana.
Igunga CUF imeporomoka lakini CHADEMA imepanda, hutakuwa na uhakika kama hiyo CHADEMA iliyopanda itaendelea kupanda.
Hakuna huo uhakika kwa sababu inategemea chama chenyewe kitajiendesha vipi. Wafuatilie kwa karibu mwenendo huu. Unaweza kukuta jinsi wanavyo-behave wanadhani wananguvu kumbe zinakwisha. Wanadhani wanapata nguvu kumbe ni nguvu ya fedha.
Raia Mwema: Unaitathmini vipi miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara?
Jaji Warioba: Mimi ningependa tuangalie si mafanikio na changamoto tu, lakini tuangalie hasa misingi ya taifa ili tuzidi kuiimarisha.
Nilikuwapo uwanjani siku ile (Desemba 9, mwaka 1961) wakati bendera ya Mwingireza inateremka. Nilikuwa takriban mita 10 kutoka eneo inapoteremshwa bendera.
Tulikuwa tumepata bahati vijana wa sekondari tunaojua Kiingereza kuja kuwa wasaidizi wa wageni kutoka nje.
Ari iliyokuwapo niwatu kuhisi ukombozi wa dhati, walijiona kwamba wanaweza. Kiburi cha wakati ule kwamba tunaweza nadhani tukiendeleze.
Kwa sasa kimeteremka maana naona hata viongozi wakilalamikiana wanakwenda kushitaki kwa mabalozi. Ni kama vile hujiamini na huwaamini Watanzania, lazima ukashitaki kwa mtu mwingine, kiburi kile nadhani tuwe nacho.
Sasa hivi nchini wapo wengine wanachoona ni mafanikio tu, na kuna wengine wanachoona ni upungufu tu. Ningependa ile misingi ya taifa sasa iimarishwe.
Kushitakiana kwa mabalozi ni kama hatujiamini na pia hatuamini Watanzania hawa. Ule umoja wetu uliokuwapo katika kudai uhuru ni lazima tuurejee, sasa hivi umemomonyoka.
Hili la kusema mara nyingi vijana wapatiwe nafasi mimi sielewi. Nchi hii muda wote imejengwa na kuongozwa na vijana. Mnatuita wazee lakini tulikuwa vijana wakati tunaongoza nchi.
Historia ya nchi yetu ni kwamba imeongozwa na vijana. Mwalimu Nyerere wakati anakuwa Rais wa TANU alikuwa na miaka 32. Amekuwa Rais wa nchi akiwa na miaka 39… ni kijana. Lakini amekuwa Waziri Mkuu mwezi mmoja na kumwachia Rashidi Kawawa kuwa Waziri Mkuu mwenye madaraka kamili, akiwa na miaka 35 au 36 hivi…ni kijana.
Ukiona Baraza la Kwanza la Mawaziri ni vijana watupu kwa sababu wachache sana walikuwa na umri zaidi ya Mwalimu (Nyerere). Na baada ya hapo, mabadiliko ya baraza yaliongeza vijana zaidi.
Amekuja Sokoine (Edward) kuwa Waziri Mkuu, akiwa na miaka 36 tu…kijana. Wakati Mwalimu anatoka madarakani (urais) 1985, Baraza la Mawaziri lililoundwa walikuwa vijana, wazee waliokuwapo ni Jamal, Kawawa na Bomani.
Wengine wote ni vijana, kina Makinda (Anne Makinda) alikuwa na miaka 24. Akaingia Salim (Dk. Salim), amekuwa Waziri Mkuu akiwa na miaka 42 …kijana. Nikaingia mimi (Waziri Mkuu) nikiwa na miaka 45, bado kijana.
Ni Malecela (John) na Msuya ndio waliokuwa na umri mkubwa kwenye nafasi hiyo, Sumaye aliyefuatia alikuwa kijana miaka 45. Sasa watu wajue jukumu la kuendesha nchi hii ni la vijana kihistoria.
Haifai kuanza kulalamikia wazee na kuwatafuta wako wapi, vijana ndiyo waongoze nchi. Nadhani pengine tufanye utafiti kubaini kuna tofauti gani kati ya vijana wale na vijana wa leo (katika maadili na uwezo wa kiuongozi).
Wale vijana walijenga umoja wa nchi hii na umoja huo tungetaka ujengwe na vijana wa siku hizi. Taabu ninayoiona ni vijana hawa (siku hizi) wamegawanyika.
Utaona wamegawanyika kwa misingi ya vyama, wamegawanyika kwa misingi ya makundi ndani ya vyama. Hawana umoja katika masuala ya kitaifa. Wakigawanyika hivyo wajue umoja wa Taifa uko hatarini na hasa unapoingiza masuala mengine ya kugawanywa kwa misingi ya fedha, udini na ukabila.
Tukibaki hivi nchi inakufa kwa sababu msingi wa nchi ni umoja. Umoja ujengwe ndani ya vyama. Tunazungumzia demokrasia katika nchi wakati katika vyama hakuna demokrasia. Kuna tatizo hapa, madaraka ndiyo imekuwa msingi wa vyama si sera na kwa sababu ya madaraka vijana wanagawanyika, hawawezi kuona ni kipi chenye manufaa kwa Taifa.
Ni kweli hatujapiga hatua kubwa za mafanikio katika huduma za jamii lakini ukiona tulipoanza na wahitimu wa vyuo vikuu kama 12 sasa hivi tuna maelfu, japo bado hawatoshi. Lakini tumepiga hatua, inawezekana tatizo ni je, tunawatumia vizuri na pia hawa wanaohitimu wana uwezo wa kulisaidia Taifa?
Tuandae na mfumo wa elimu unaowapa uwezo wahitimu kujitegemea, kujiajiri ili wasaidie nchi. Bado ile hali ya elimu ya kujitegemea si nzuri.
Ongezeko la watu wetu ni kubwa kuliko kukua kwa uchumi, ingawa hapa unaweza kusema umri wa kuishi miongoni mwa Watanzania umeongezeka, vifo vimepungua, lakini sasa kuna changamoto katika uchumi.
Tufanye kazi, na tatizo jingine ni kwamba ile hali ya ku-mobilise watu wafanye kazi imepungua. Tunafanya zaidi siasa. Na kuna hali nyingine viongozi wanajidai kuwa wanaweza binafsi kumwendeleza mwananchi.
Hakuna kiongozi anayeweza kumwendeleza mwananchi. Sasa hivi inaonekana kama kila kitu kinawezakana kutoka serikalini, lakini ukweli ni kwamba uongozi ni kuonyesha njia.
Raia Mwema: Maoni yako haya ndiyo tathimini yako ya awamu ya kwanza na zilizofuatia?
Jaji Warioba: Awamu ya kwanza ilikuwa na mafanikio. Hawakuwa na mfano wa kuiga, walijenga misingi na dira ya nchi hii, kwamba tunataka kwenda wapi na kwa nini?
Kwa kiwango kikubwa awamu hii ilifanikiwa kupanga misingi ya nchi, vita dhidi ya maadui wale watatu: ujinga, maradhi na umasikini iliakisi dira hii.
Hawa pia ndio waliopanga kujenga taasisi, taifa lolote lile linahitaji kuwa na taasisi zenye nguvu. Misingi hii yote ni kwa ajili ya kujenga nchi imara. Ni kweli kulikuwa na matatizo lakini waliweka misingi. Kuna changamoto, kwa mfano, miaka ya 70, bei ya mafuta ilipanda, vita ya Uganda na matatizo mengine.
Kipindi cha Rais Mwinyi (Ali Hassan) kilikuwa wakati wa kujijenga kutoka katika matatizo ya awali kiuchumi lakini wakati wote hatukupoteza lengo la baadaye kwamba tunafanya hiki lakini tunajua tulikokuwa tunataka kuelekea.
Kuna mafanikio. Hapa utaona ile smooth transition kutoka kwenye command economy kwenda kwenye liberalization. Ilikuwa ngumu lakini ilifanywa vizuri na ni wakati huo huo ilianza transition ya ku-liberalize siasa. Hii haikuanza 1992, ilianza mapema.
Wakati wa Mkapa alitaka ku-consolidate yale yaliyoanzishwa na Mwinyi akakazania sana kwenye uchumi, akadhibiti mfumuko wa bei lakini kipindi hicho baada ya vyama vingi hatukuwekeza sana katika masuala ya siasa.
Tumeacha siasa inaelea, tumeanzisha vyama vingi bila udhibiti. Kuna tatizo kubwa zaidi si tu katika uchumi na maendeleo lakini ni pamoja na kujenga mfumo mzuri wa siasa.
Sasa hivi tuna tatizo la kuzungumzia regime change badala ya demokrasia. Hii ni changamoto sasa ili tujenge nchi ya kidemokrasia na si nchi ya regime change tu.
Raia Mwema: Unazungumziaje suala la Katiba mpya?
Jaji Warioba: Sina hakika kama viongozi wetu wanaelewa ni kitu gani kilicho muhimu. Nadhani tunaingia katika tatizo hili la kila mmoja anatazama manufaa yake.
Katiba hii msingi wake ulikuwa ni chama kimoja. Tumefanya mabadiliko kuna mambo ambayo yametokana na chama kimoja lakini ni ya msingi katika kuendesha nchi. Ni muhimu tuyatazame na kati ya hayo ni Tanzania ya aina gani tunayotaka kuijenga.
Moja ambalo limetokana na mfumo wa chama kimoja ni kwamba TANU, ASP na CCM vilikuwa na itikadi ambayo ilikuwa inafafanua tunataka Tanzania ya aina gani na wananchi wakaielewa.
Bila kujali ulikuwa unakubaliana na Ujamaa na Kujitegemea ulijua huu ndio mwelekeo wetu tunataka Tanzania ya Ujamaa na Kujitegemea. Ni Ujamaa na Kujitegemea na miiko yake ilikuwa inaeleweka nchi nzima. Wananchi walikuwa wanatoa uamuzi kulingana na itikadi.
Sasa hakuna. Hatujui ni Tanzania gani tunayotaka kuijenga na hapo nadhani tunapokwenda kwa wananchi tutarajie hilo kwamba kubwa tunalotaka kutoka kwa wanannchi ni Tanzania gani wanataka tuijenge.
Tusiende kwamba kulazimisha kuyazungumza haya tunayoona ni makubwa kwa sababu watazungumza kwa jinsi wanavyoona mambo yao. Unaweza kwenda sehemu ukakuta tatizo lao ni ardhi. Wengine wanaweza kuzungumzia madini. Tuyasikilize yote haya na kutokana na hayo utaona Watanzania wanataka Tanzania ya aina gani.
Katika kile kifungu cha malengo muhimu ya Taifa haya yaelezwe ndani ya Katiba kwamba Watanzania malengo waliyonayo ni haya.
Kwa hiyo, kwangu hili ni muhimu la sivyo tutabaki katika yale yale ya kujidanganya kwamba Tanzania ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea wakati ile misingi haipo. Lazima tujipange kuhakikisha tunajenga Tanzania tunayotaka. Katiba ni wananchi na wananchi waachwe waamue mambo yao muhimu.
Tusipofafanua Tanzania tunayoitaka bado tutakuwa na mgogoro kwa sababu hapatakuwa na yard stick ya kuwapima viongozi na Tanzania tunayotaka kuijenga.
Kuna suala la msingi kuwa wananchi ndiyo wenye madaraka. Lazima tueleze ni madaraka gani yako kwa wananchi, kwamba wana uwezo upi wa kukataa viongozi.
Saa hivi kuna kujichanganya, unakuta tunasema madaraka yako kwa wananchi lakini tumeyahamisha kwa kiwango kikubwa kwenda kwenye dola au kwenye vyama vya siasa.
Serikali utakuta imepewa madaraka makubwa lakini wanasema ni kwa niaba ya wananchi. Vyama vya siasa navyo ni hivyo, vimepewa madaraka makubwa nao wanasema ni kwa manufaa ya wananchi.
Sasa hivi pamoja na Katiba kusema kwamba msingi wa madaraka ni wananchi kwa hiyo wanachagua wawakilishi lakini bado msingi huo unabanwa kwamba unawaambia kama unataka mwakilishi lazima ufuate taratibu hizi. Kama wewe si mwanachama wa chama cha siasa basi huna nafasi hiyo.
Kwamba watu wanaweza kumchagua mwakilishi lakini chama cha siasa kinaweza kumfukuza huyu mwakilishi. Wanakorofishana ndani ya chama wanamfukuza na anapoteza mandate ya wananchi kama vile mwakilishi huyo alichaguliwa na chama. Lazima mipaka iwekwe ndani ya Katiba.
Baada ya hapo tuangalie zile taasisi muhimu, Bunge, Serikali na Mahakama tuangalie upya mgawanyo wa madaraka haya, ile separation of powers iwepo lakini pia lazima kuwapo checks and balances.
Sasa hivi nadhani itabidi tuimarishe Mahakama. Iwe na uhuru wa kifedha, wasitegemee hisani ya Katibu Mkuu wa Hazina.
Kama tumefika mahali unasema Bunge litapata bajeti kiwango fulani na vyama vya siasa vinapata bajeti fulani, Mahakama nayo lazima tuseme wanapata asilimia fulani.
Tuingie kwenye utendaji, tuangalie mgawanyo wa madaraka kati ya Rais na taasisi za utendaji. Najua Rais lazima atakuwa na madaraka lakini kuna mahali pengine ama madaraka haya yanaweza kwenda kwenye taasisi au utendaji wake Rais lazima ashauriwe.
Inawezekana tukaamua, je, kuna umuhimu wa kumpa Rais madaraka ya kuteua mawaziri lakini wawe wanathibitishwa mahali? Ateue majaji lakini wathibitishwe mahali.
Sasa hivi naona kuna watu hawataki Rais awe na madaraka makubwa lakini mimi nafikiri Rais lazima awe na madaraka isipokuwa tuangalie yale mengine awe nayo lakini kwa kushauriwa. Lazima katika Taifa kuwe na mtu mnasema lazima awe na madaraka haya, isipokuwa ni kutengeneza utaratibu.
Hata kama tunataka Rais wa kikatiba tu ingawa sioni hilo kama ni zuri katika nchi, kama tunataka awe waziri mkuu sawa. Lakini suala la madaraka ni muhimu.
Katika mabadiliko ya mwaka 1984 nia ilikuwa kupunguza madaraka ya Rais, Waziri Mkuu asimamie zaidi utendaji lakini sasa hivi unaona kama Waziri Mkuu hana madaraka ya kusimamia utendaji.
Imejitokeza Rais anasimamia utendaji, anakwenda wizara kwa wizara, anatoa maagizo ya utendaji, Katiba haijamzuia lakini imemuwekea mtu wa kumsaidia, nimeona kwenye Bunge Waziri Mkuu anaulizwa maswali ya papo kwa papo anazumgumzia sera. Sera si ya kwake, iko chini ya Rais.
Kwa hiyo tutakapozungumza Katiba ni lazima hapa tufafanue nini kazi za waziri mkuu au kama kuna sababu ya kuwa na waziri mkuu. Tuzungumze, je, mawaziri wawe kama walivyo kutokana na Bunge?
Bunge nalo liangaliwe, madaraka yake yafafanuliwe. Unajua wakati mwingine Bunge limeingilia mambo ya utendaji, lazima sasa iwepo mipaka kati ya Serikali na Bunge na tujue nani anastahili kuchaguliwa kwenda bungeni, tujue utaratibu wa kupiga kura.
Sasa hivi wanazungumzia sana Tume ya Uchaguzi. Tuzungumzie hili. Kuna watu wanafikiri lazima iwakilishe makundi fulani fulani. Zanzibar wanazungumzia uwakilishi wa vyama. Kwingine, Afrika Kusini wanaye kamishna. Ghana wanayo tume ambayo mwenyekiti ni yule yule, amekuwapo kwa muda kwa sababu yuko huru.
Naamini Tume yetu ikiwa na wajumbe kutoka vyama vya siasa haitakuwa huru. Nadhani utaratibu wa Katiba mpya utuwezeshe kupata maoni ya wananchi.
Ninachokiona sasa ni kila kundi kwa maslahi yake linatumia hoja ya wananchi kuwa wanataka utaratibu fulani. Vivyo hivyo, Serikali nayo inataka kuweka mipaka fulani kwa maslahi ya wananchi.
Tusiweke mipaka. Wananchi watoe mawazo yao. Kuna vyama vya siasa vinasema kwa manufaa ya wananchi tuwe na Bunge la Katiba ambalo litachagua Tume na kutoa hadidu za rejea na kusimamia mchakato na baada ya kupitisha watakwenda kwa wananchi.
Sikubaliani na hilo. Wananchi waachwe wazungumze yote wanayotaka, Katiba yao iweje. Wakishakuzungumza, hiyo tume itengeneze muswada wa katiba urudi kwa wananchi. Wazungumze, kusiwe na kikundi hapa katikati kinasema kwa manufaa ya wananchi. Hapana.
Wananchi wazungumze muswada na chombo cha kupitisha kipitishe baadaye. Wasilete vikao hapa katikati huku wanajitafutia nafasi. Mchakato huu uende moja kwa moja kwa wananchi. Tusiwawekee mawazo.
Kuna wanaharakati wanataka kuleta mambo ya kuwajaza wananchi. Nina hakika wananchi wakiachiwa uhuru, watasema na wataalamu watapanga vizuri. Nasisitiza la msingi ni kuwaacha wananchi waseme wanataka nchi ya namna gani.
Suala la Muungano pia liwe katika Katiba. Tusipokuwa makini kwa maneno yanayozungumswa sasa tutavunja Muungano.
Muungano huu una misingi yake na upo kwa manufaa ya wananchi. Tufafanue manufaa hayo ni nini kwa mwananchi wa kawaida.
Wakati wote kwa mwananchi wa kawaida, kumekuwa hakuna matatizo ya Muungano. Matatizo yanatoka kwenye midomo ya viongozi.
Shughuli za wananchi wa kawaida haziangalii orodha ya mambo ya Muungano, bali haki yao kama raia. Wanajiona ni raia katika shughuli zao za kibiashara au nyingine. Mwananchi wa kawaida anaona anayo haki ya kufanya biashara mahali popote. Wananchi wamezoa hivyo. Msiwafikishe mahali wakajiona kuwa kwenda Zanzibar au kuja Bara inabidi wafuate taratibu za kwenda Kenya au Uganda.
Tunayo matatizo ya madaraka, kwamba unazo Serikali mbili kwa hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha Serikali hii ina madaraka gani. Wanagombania madaraka.
Kama suala ni mafuta au mengine tuzungumze. Inategemea mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo yatakuja kuwatenganisha wananchi. Kama kwa mfano, kuna watu wanafikiri kuimarisha Muungano ni kuwa na serikali tatu, unaimarishaje?
Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote.
Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa.
Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa pande zote mbili. Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake unavunja Muungano

No comments:

Post a Comment