Balozi wa Uingereza azungumzia ushoga
Aeleza kuwa kigezo hicho hakitaigusa Tanzania
Alalamika kuwa jambo hilo limepotoshwa.jpg)
Balozi wa Uingereza nchini, Diane Corner
Balozi huyo alitoa kauli hiyo jana wakati wa mahojiano ya kipindi cha Breakfast Talk Show, kinachorushwa moja kwa moja na Redio ya East Africa, alizungumzia pia mambo mengine ikiwamo ziara ya mwana wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles na Mkewe, Camilla, ya siku tatu nchini kuanzia keshokutwa.
“Naona kama suala lenyewe limekuzwa nje ya muktadha. Vigezo vya misaada ya maendeleo havitegemei suala moja tu, kuna vitu vingi vinaangaliwa,” alisema.
Kwa mfano alisema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika Ripoti ya Taasisi ya Mohamed Ibrahim (MO) katika vigenzo vya kupima utawala bora, hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu kwamba misaada itakatwa.
Katika ripoti ya mwaka huu MO ambayo ilipima nchi za Afrika kwa mwaka jana, ambayo Rais wa Cape Verde Pedro Verona Pires, alinyakua tuzo ya mwaka 2011 kwa marais wastaafu wa bara hilo ambao utawala wao ulizingatia demokrasia na utawala
bora, Tanzania ilikuwa ya 13 kati ya nchi 53 za bara hilo na ilipimwa kwenye vigezo vinne ambavyo ni usalama na utawala wa sheria, ushiriki katika demokrasia, vivutio endelevu vya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Balozi huyo alisema misaada ya kwa Tanzania itandelea kama ilivyopangwa ukiwamo mkataba wa Sh. trilioni 1.5 kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa miaka mitano ijayo.
Corner alisema Tanzania ina rekodi nzuri ya haki za binadamu na kwa vyovyote haitaathirika na msimamo huo mpya wa Uingereza.
Uingereza ni miongoni mwa mataifa yanayotoa misaada mingi kwa Tanzania, ikiwamo inayopitia kwenye kundi la nchi wafadhili katika kusaidia bajeti lakini pia misaada mingine ya moja kwa moja.
Kauli ya kufungamanisha misaada na haki za mashika ilitolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, baada ya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Australia wiki iliyopita.
Baada ya kauli hiyo, upinzani mkali uliibuka nchini ukihusisha vikundi mbalimbali vya kijamii, na juzi mwaziri wanne wa serikali ya Muungano wa Tanzania walitoa misimamo yao kuashiria kwamba Tanzania ilikuwa radhi kukosa misaada kuliko kushinikizwa itunge sheria za kuruhusu ushoga nchini.
Mawaziri hao ni wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, Sheria na Katiba, Celina Kombani na Fedha, Mustafa Mkulo.
Kadhalika, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, naye akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa serikali ya umoja wa kitaifa tangu ashike madaraka, alisema ushoga hautakubalika visiwani humo na wako tayari kukosa misaada.
Wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu, nao wamepaza sauti zao wakisema ni bora kuwa masikini kuliko kukubali kuhalalisha ushoga nchini. Kauli kama hiyo pia imetolewa na viongozi wa dini wa Kikristo na Waislamu nchini. Na Richard Makore.
DK. MVUNGI: TULIKATAA FEDHA ZA UINGEREZA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, amesema anatamani kufa na kutangulia ahera ili asione Tanzania wakati itakaporuhusu ndoa ya jinsia moja kama inavyoshinikizwa na Uingereza.
Dk. Mvungia aliyasema hayo jana jijini Dare s Salaam jana wakati akitoa mada kwenye warsha ya kujenga uwezo wa ushiriki katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambayo iliwashirikisha wanaharakati na waandishi wa habari.
Alisema ni aibu kubwa kwa Tanzania ikiwa siku moja itaruhusu ndoa ya jinsia moja, na kwamba ikiwa itafanya hivyo, itakuwa inakwenda kinyume na sheria za nchi kwa kuwa tendo la kulawiti ni kosa la jinai.
Alitaka Watanzania kupinga sula hilo kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha halipati nafasi na kwamba umasikini usiifanye Tanzania ipoteze heshima yake.
“Naomba Mungu siku ikitokea ushoga ukaruhusiwa mimi niwe nimekufa ili nisione kitakachokuwa kinaendelea,” alisema Dk. Mvungi ambaye pia mwanaharakati
Alifafanua kuwa Uingereza inataka kuwaona Watanzania na Waafrika kwa ujumla ni wajinga na kuwashinikiza wakubali ndoa za aina hiyo wakati wao suala hilo hawajaliingiza kwenye Katiba yao.
“Jambo hili likiingizwa kwenye Katiba litapotosha taifa kwa kuwa lilianza kujipenyeza kwenye Kanisa la Anglikana, lakini halikupata nafasi hivyo ni lazima lipingwe,” alisema.
Dk. Mvungi ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa Kituo cha sheria na haki za Binadamu (LHRC), alisema kuna wakati Uingereza ilikipatia kituo hicho fedha kwa ajili ya kuhamasisha kutambuliwa kwa ndoa za jinsia moja, lakini walizikataa zikapelekwa kwa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Juzi, serikali ilitoa msimamo wake wa kukataa kuzitambua ndoa za jinsia moja na kusema kuwa Tanzania iko tayari kukosa misaada ya Uingereza.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa fedha, Mustapha Mkulo; Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment