

Na Ally Saleh,
Kwa hakika takwimu zinatisha. Zinatisha kiasi cha kutokuamini kuwa haya yanatokea Zanzibar nchi ambayo watu wake wana sifa ya ukarimu, watiifu kwa dini yao lakini pia ni makini katika mambo yao.
Kumbe ni kinyume kabisa na hali ilivyo imekuwa ya kuogopesha kiasi ambacho wanasiasa wameona kuna haja ya kulivalia njugu jambo hili ili kuondosha kama si kupunguza madhila yanayofanywa dhidi ya wanawake na watoto.
Na kwa upande mwengine wana harakati nao wameona kuna haja ya kuunganisha nguvu zao ili suala la unyanyasaji wa kijinsia lizungumziwe kwa uwazi na undani ili lifike jamii katika ukweli wake hasa.
Na ndipo mwishoni mwa wiki iliyopita Chama wa Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA ikaandaa kikao cha ubadilishanaji wa habari ambacho kiliwashiriksha waandishi wa habari waandamizi na wahariri huko Zanzibar ili kujaribu kuunganisha nguvu zao kupiga vita hali hiyo.
Lakini sio tu kupiga vita bali pia kuendesha kampeni ya kitaifa juu ya suala hili ili kukuza uelewa wa wananchi juu ya matendo haya ambayo yanaidhalilisha jamii na kudhulumu wanawake na watoto kupita hata maelezo.
Baadhi ya watafiti wa kike kutoka TAMWA walitoa ushuhuda wa kutisha wa watoto waliodhulumiwa sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba baadhi ya kadhia hizo naziona ngumu hata kuziandika lakini itoshe kusema kuwa wadhulumiwa wengine wameharibika tupu zao za nyuma na mbele bila ya nafasi ya kuweza kurekebishika.
Pia Chama cha Wanasheria Wanawake wa Zanzibar ZAFELA walieelezea jinsi juhudi za kufiksiha kesi mahakamani zinavyokwama au kudonda baada ya kufika huko kiasi ambacho kinatisha na kuvunja moyo.
Mfano ulitolewa wa ustadh wa chuo cha Kur-ani ambaye alifikishwa mahakamani akishutumiwa kwa ubakaji wa watoto kadhaa wa kiume na kike lakini akaponyoka Mhakamani katika hali ambayo imewaacha wanaharakati, wazee na wathirika wenyewe wakizubaa.
Inaelezwa kuwa kesi zinazofikishwa hospitali kila wiki ni wastani wa 10 na kwa maana hiyo ina idadi inayothubutu tu kwenda hospitali basi inatisha tukijua kuwa kesi nyingi za unyanyasaji wa kijinsia na watoto kwa utamaduni wa Zanzibar huishia nyumbani.
Pia mkutano huo uliofadhiliwa na taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu UNFPA ulishuhudia wahariri na waandishi waandamizi wakielezewa jinsi ambavyo juhudi za Wizara ya Wanawake na Watoto katika eneo hilo na mipango yake ya kutandandika sheria na sera.
Kwengineko pia wana habari wakasikia jinsi ambavyo kituo cha Mkono kwa Mkono ambacho kilizinduliwa miezi mitano iliyopita kinavyofanya kazi kurahisisha huduma za wadhulumiwa wa kingono na kijinsia.
Kituo cha Mkono kwa Mkono kipo ndani ya eneo la Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambapo huduma za kumsaidia muadhirika zinapatikana chini ya mwamvuli mmoja na hivyo kujali maumivu ya mdhulumiwa huyo.
Ndani ya kituo kunapatikana huduma za Polisi, kisheria, kiafya, kiushauri na kadhalika lakini msimamizi mkuu wa kituo hicho Dk. Msafiri Marijani alieleza uwepo wa changamoto kadhaa ambazo zinakabiliwa na kituo hicho.
Changamoto hizo ni pamoja na zile za kukosa wataalamu wa ushauri ambao ni muhimu sana ili muathirika mbali ya kutibiwa kiafya au kividonda lakini pia atibiwe kiakili kwa sababu unyanyasaji aliofanyiwa unaweza ukabakia katika akili yake kwa muda mrefu na hivyo kutia doa kubwa katika maisha yake ya kila siku.
Pia Dk. Marijani alisema kuna changamoto ya kutokuwa na watendaji wa kutosha katika kituo hicho kiasi cha kuzorotesha huduma maana watendaji waliopo hutakiwa kufanya kazi nyengine za kihospitali hasa zinazohusiana na masuala ya dharura ambayo ni ya kila siku.
Ushauri wake kwa wana habari ukawa ni kukiimarisha kwa kuhimiza ushiriki wa wadau katika kituo hicho kwa kutoelemeza wajibu wote kwa Serikali kuu kwa vile kituo hicho hasa muundo wake ulikusudiwa kupata michango ya taasisi zisizo za kiserikali kama mfano huo ulivyoigwa kutoka nchini Zambia.
Wanaharakati ikiwa ni pamoja na Mzuri Issa wa TAMWA walielezea haja ya kuwa na kituo kimbilio kwa waathirika wa mashambulizi ya kijinsia yawe ni ya nguvu au kiakili, jambo ambalo litawapa angalu tulizo la muda wakitafakari hatua ya kuchukua baada ya hapo.
Lakini kwa hali ilivyo hivi sasa watoto na wanawake wengi wanaonyanyaswa hulazimika kurudi katika nyumba zile zile walizopata matatizo na kurudi kwa jamaa wale wale ambao ni sehemu ya hujuma kwao.
Takwimu zinasema kuwa wengi wa wanyanyasaji hao ni wajomba, kaka, ami, baba, babu na kwa hivyo mara nyingi mno muathirika anakosa sauti kwenye familia kwa ama kuonekana ni muongo au kutaka kuficha aibu kifamilia.
Na hilo ndio linalotokea katika vituo vya Polisi ambako mara nyingi tatizo la aina hii huambiwa ni la kifamilia na kwa hivyo kutakiwa kumalizwa kifamilia na wakati mwengine hata kutumika neno fidia kutolewa kwa muathirika.
Kumekuwa katika siku za karibuni na kauli za wanasiasa ambazo zimepaza sauti kuhusu madhila hayo jambo ambalo linatia moyo sana, lakini upande mwengine linahoji utekelezaji wa sheria ziliopo ambazo hao hao wanasiasa ndio wanaozitunga katika Baraza la Wawakilisha.
Ila kwa hakika inatia moyo kuona wanasiasa wanalipandisha chati jambo hili kufikia ngazi ya kitaifa na kulifanya ni tatizo la kinchi na si kifamilia. Kwamba vita hivi ni vya kila mtu ndio ujumbe wa wanasiasa hao.
Na ndipo TAMWA na UNFPA wakakusanya waandishi wa habari ili nao washiriki katika kampeni maalum ya kupiga vita unyanyasaji wa jinsia kwa kutumia kalamu na sauti zao na ikitarajiwa kuwa taarifa zitamfika kila mtu.
Lakini baadhi ya washiriki walisema ukweli ni kuwa kila mtu anajua kwamba kuharibu mtoto wa kiume au wa kike ni kosa la kidini, kijamii na kidunia na kwamba kila mtu anajua pia kuwa kumpiga mwanamake au kumnyanyasa kiakili pia ni kosa na kila mtu anajua.
Kwa hivyo muelekeo wa wanahabari hao ukawa kuwa kampeni hiyo ilenge suala la kubadili tabia miongoni mwa watu wetu kwa sababu sheria zipo na zinaeleweka, dini zipo na zina waumini wake lakini pia maadili yapo na jamii ndio inayosimamia.
Kwa hivyo kila mtu akichukua nafasi yake basi tatizo hili litaweza kupigwa vita maana si kwa kuwa ni geni au halikuwepo au litaondoka kabisa, lakini ni muhimu kuzuia lisikuwe kwa sababu kila likikuwa inakuwa ni mzigo na janga kwa jamii.
Tungependa kuwa na jamii yenye amani na isiyo na makovu ya dhulma kama hizi, na wengi tunaamini hilo linawezekana. Sioni sababu gani lisiwezekana wakati watoto ni wetu na wake au wanawake ni wetu.
Jee jamii ya Kizanzibari imechoka kuwaheshimu watoto wao wa kike na kiume au imechoka kuheshimu wake zao? Hivi ni vitendo vya aibu na aibu hii inarudi ndani ya nafsi ya kila mtu. Ifike wakati kila mtu aisute nafsi yake kwa nini haya yanatokezea na ni vipi yeye kila mmoja anaweza kuzuia, kukemea au angalau basi kulizunngumzia kwa njia ya kugomba, kushauri au kulipiga vita.
chanzo mwananchi
No comments:
Post a Comment