Monday, 24 October 2011

Gaddafi aliahidi utajiri wa fedha, dhahabu kujiokoa

Aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi
MISRATA, Libya
ALIYEKUWA kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alitoa ahadi ya utajiri wa fedha na dhahabu kwa watu waliomtia nguvuni, ikiwa ni katika kujaribu kuokoa uhai wake.

Mmoja wa mashuhuda, Hammad Mufti Ali (28) alieleza namna kiongozi huyo alivyowaahidi utajiri tofauti vijana waliobaini maficho yake kwenye mtaro wakupitisha maji barabarani jambo ambalo lilikuwa ni tofauti na matarajio yao.

Ushuhuda huo umetolewa huku kukiwa na utata kuhusu nini kilichotokea katika dakika za mwisho za kifo cha Kanali Gaddafi, ambaye mazishi yake yameendelea kucheleweshwa kutokana na wito wa kutaka kufanyika kwa uchunguzi.

Ali ambaye ni kamanda wa brigedi moja ya kijeshi katika Mjini wa Sirte, alikaririwa na Gazeti la Coriette Della Sera la Italia akisema baada ya kutolewa katika mtaro, kisha kusukumwa huku na kule, alitoa ahadi nyingi akiomba asiuawe.

“Alisema yuko tayari kutoa chochote ili kulinda uhai wake. Alisema anazo fedha na dhahabu kwa ajili yetu iwapo tutamwacha akiwa hai.”
“Alikuwa akitokwa na damu nyingi, alikuwa na umri wa miaka 69 hivyo mwili wake usingeweza kuhimili. Alikuwa katika hali mbaya sana. Alikuwa na majeraha kila sehemu ya mwili wake, ya risasi na yaliyotokana na kipigo,” alisema na kuongeza:
“Kuna wakati mmoja wetu alipayuka akimwambia kuwa badala ya kuzungumza kuhusu fedha, kama Mwislamu mwadilifu, anatakiwa kuomba kwa ajili ya nafsi yake iweze kupokewa mbinguni kabla hajafa. Lakini aliendelea kusisitiza kwamba yuko tayari kutupa fedha nyingi na dhahabu nyingi kadiri iwezekanavyo”.
Kanali Gaddafi alionekana akitolewa katika mtaro huo wa maji wa barabarani akiwa hai, huku akiwa na majeraha kadhaa ya risasi.
NTC yajikosha

Hata hivyo, Baraza la Serikali ya Mpito (NTC), limekuwa likisisitiza kwamba alijeruhiwa wakati wa mapambano makali ya risasi baina ya wafuasi wake waliokuwa wakimlinda na wapiganaji waliokuwa wakimpinga, lakini baadhi ya mashuhuda wamekuwa wakieleza kuwa aliuawa baada ya kukamatwa.

Mmoja wa makamanda wa jeshi mjini Misratah, ambako ndiko mwili wake ulikopelekwa alisema hawakuwa na la kufanya, morali ya vijana wao iliwazidi nguvu.
“Tulitaka kuhakikisha kuwa anakamatwa na kufikishwa kunakohusika akiwa hai. Lakini kutokana na vijana tuliokuwa nao, mambo yaligeuka, walituzidi nguvu,” alisema.

Taarifa nyingine zinasema Kanali Gaddafi alikuwa na utajiri unaozidi dola200 bilioni za Marekani ikiwa katika fedha taslimu na dhahabu uliofichwa katika akaunti za siri maeneo mbalimbali duniani.
Taarifa zilizopatikana awali wakati vuguvugu la kumwondoa madarakani lilipoanza, zilieleza kwamba amehamishia sehemu kubwa ya utajiri wake nchini Zimbabwe.
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limeeleza kwamba inaaminika Libya inazo zaidi ya tani 140 za dhahabu zilizofichwa nje ya nchi hiyo, nyingi zikiwa zimefichwa kwa kutumia jina la Benki yake Kuu.

Inaaminika kuwa Kanali Gaddafi alichukua kiasi kadhaa cha dhahabu na fedha katika siku zake za mwisho, ili kuzitumia kama sehemu ya makubaliano na wale watakaomkamata.

Utata wa maziko
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Sky News, baada ya kuibuka kwa mvutano kuhusu maziko ya kiongozi huyo wa zamani wa Libya, huenda mwili wake ukakabidhiwa kwa ndugu zake,.

Msemaji wa Mambo ya Nje wa NTC, Ahmed Jibreel alikaririwa na kituo hicho akisema makabidhiano hayo huenda yakafanyika haraka.

Iwapo matatizo hayo yaliyojitokeza na kutoelewana kuhusu suala hilo yasipofikiwa kwa wakati, hali ya amani ya Libya huenda ikawa katika utata zaidi.
“Ninadhani uamuzi tayari umeshafikiwa, ambao ni kuukabidhi mwili wa Gaddafi kwa familia yake ambayo ni pana na iliyotawanyika maeneo mengi.

“Kuna majadiliano ambayo yamefanyika baina ya NTC na watu wa kutoka Sirte, ambako mwili wake huenda ukakabidhiwa. Baadhi ya ndugu zake wako Sirte na wengine katika miji mingine. Tunatarajia hili litafanyika mapema, kama si katika saa chache zijazo, itakuwa katika siku chache zijazo,” alisema Jibreel.

Kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu, mwili huo ulitakiwa kuzikwa katika muda usiozidi saa 24 baada ya kifo chake, lakini sasa tayari umeshafikisha zaidi ya saa 60.

Kanali Gaddafi aliuawa Oktoba 19, mwaka huu baada ya mapambano ya takriban miezi saba na waasi wa nchi hiyo ambao walikuwa wakiungwa mkono na mataifa ya Jumuiya ya Kujihami ya Ulaya Magharibi (Nato), tangu Februari mwaka huu baada ya machafuko katika nchi za Tunisia na kisha Misri.

No comments:

Post a Comment