Monday, 11 July 2011

Mfalme wa Ashanti amtembelea Rais Kikwete
Mwandishi Wetu
MFALME Otumfuo Osei Tutu wa Pili wa Ufalme wa Ashanti nchini Ghana, amewashauri baadhi ya Waafrika kuacha kutumia demokrasia vibaya kwa kutoheshimu viongozi wa nchi na serikali, ambao anaamini wamedhamiria kuimarisha demokrasia kwenye bara la Afrika.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa mfalme huyo pia alisema hali ya baadaye ya bara la Afrika itakuwa nzuri, lakini mafanikio hayo yatategemea jinsi Waafrika wenyeji wanavyoendesha nchi zao, siyo sera za mashirika ya fedha duniani.
Pia, Mfalme huyo na Rais Jakaya Kikwete wamekubaliana kuwa ,Afrika ndilo bara ambalo dunia nzima itakuwa inalikimbia siku zijazo.
Mfalme Otumfuo Osei Tutu wa Pili na Rais Kikwete alikutana Ikulu jana, baada ya Mfalme huyo kuwasili nchini kuanza ziara ya siku 10 kwa mwaliko wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
Baada ya mazungumzo yao, viongozi hao wawili walikula chakula cha mchana pamoja na Mkapa na wawakilishi wachache wa familia zilizokuwa za kichifu nchini.
Mfalme alimwambia Rais Kikwete kuwa, ni vizuri kuona maendeleo makubwa ya demokrasia Afrika na ari ya viongozi wa sasa kuimarisha demokrasia hiyo, lakini ni jambo la kusikitisha baadhi ya Waafrika wameanza kutumia vibaya demokrasia kwa kutoheshimu, na wakati mwingine kudharau viongozi.
“Kiongozi wa nchi huchaguliwa na wananchi wote. Hivyo, ni muhimu baada ya uchaguzi kufanyika na kumalizika, wananchi wote, waliompigia kura na wale ambao hawakumpigia kura kuonyesha heshima inayostahili kwake kwa sababu yeye sasa ndiye kiongozi wa nchi," alisema.
Katika mazungumzo yao, Mfalme na Rais Kikwete pia walikubaliana miaka ijayo dunia itakuwa inalitegemea bara la Afrika katika kudumisha mafanikio ya uchumi duniani.
“Hali ya baadaye ya uchumi wa dunia itakuwa mikononi mwa Afrika. Changamoto ya bara letu, ni jinsi gani ya kuweka akili yetu pamoja kuweza kubuni sera nzuri zinakazoendeleza matunda ya uchumi na jamii ya bara letu na zitakazoleta maisha bora kwa wananchi wetu. Mpira uko uwanjani mwetu lakini hali ya baadaye ya uchumi wa dunia ni Afrika,” alisema Rais Kikwete.
Mfalme alikubaliana na Rais akisema: “Afrika ndilo bara linaloangaliwa na dunia nzima kwa sasa na miaka ijayo. Lakini mafanikio ya Afrika yako mikononi mwa sisi wenyewe na wala siyo kwenye mikono ya IFM (Shirika la Fedha Duniani) ama Benki ya Dunia.”
Pia, walikubaliana kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Ghana, ambao ulijengwa miaka ya mwanzo ya uhuru wa nchi hizo kupitia kwa Mwalimu Julius Nyerere na Osagyefo Kwame Nkurumah. Ghana ilikuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata uhuru, kutoka ukoloni wa Kiingereza mwaka 1957.
“Nimefurahi kufika Tanzania. Nimesikia mambo mengi mazuri kuhusu nchi hii tokea wakati wa viongozi wetu Julius Nyerere na Kwame Nkurumah. Naamini ziara yangu itaanzisha jitihada kubwa zaidi za kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu mbili” alisema Mfalme Tutu wa Pili.

No comments:

Post a Comment