MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka Serikali ya Muungano kutopuuza hoja nzito ya posho za wabunge iliyoibuliwa na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Juni saba mwaka huu Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA) aliwasilisha barua ofisi ya Bunge kukataa posho akisema watumishi wa serikali na wabunge, hawastahili kulipwa posho wanapohudhuria vikao rasmi vya uwajibikaji wao wa kawaida.
Zitto alisema posho hiyo haistahili kulipwa kwake, wabunge wengine wala watumishi wa umma kwa kuwa kuhudhuria vikao ni sehemu ya kazi zao. Wabunge wanalipwa posho ya sh 80,000 na sitting allowance ya sh 70,000, hivyo kuweka kibindoni sh 150,000 kila siku.
Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na ITV, Maalim Seif alisema hapendi kuichambua zaidi hoja hiyo kwa kuwa suala hilo halimhusu bali ipo haja ya serikali kuiangalia kwa upana zaidi.
Alisema suala la posho ni hoja yenye nguvu, hivyo serikali isiipuuze bali inaweza kuipuuza iwapo itakuja na utetezi mzito zaidi wa kuipiku hoja ya CHADEMA.
“Hoja iliyoibuliwa na CHADEMA ni ‘very strong’ wala serikali isiipuuze, na kama kuna hoja ya serikali iliyo nzito zaidi ya hiyo basi serikali itoe, lakini si jambo la kupuuzwa,” alisema Maalim Seif.
Akizungumzia kuhusu suala la kisiasa, Maalim Seif alisema kwa sasa Zanzibar ni shwari lakini Bara bado kuna tatizo ambalo linasababishwa na Jeshi la Polisi kusahau majukumu yake.
Alisema polisi wamekuwa wakiingilia masuala ya kisiasa kwa ajili ya kuifurahisha serikali lakini sheria inakataza kwani jeshi hilo linatakiwa kutopendelea chama chochote cha siasa.
Alisema katika suala la Muungano bado kuna matatizo makubwa hivyo viongozi wanapaswa kuwa tayari kukabili kero hizo.
“Muungano ni tatizo hata nikitumia neno kero halitoshi maana wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika sana hasa kuhusu kulipishwa bidhaa zao ushuru mara mbili,” alisema.
Alisema ingawa jambo hilo lilikwisha jadiliwa katika kikao walichokutana na viongozi wa juu wa serikali ya Muungano lakini utekelezaji wake kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) limekuwa zito.
Maalim Seif alisema kuhusu suala la uchumi wa visiwa hivyo linapaswa kuachiwa Wazanzibari wenyewe ili kuwa na uhuru kutokana na uchumi huo kuwa tofauti.

|
No comments:
Post a Comment