Friday, 1 July 2011


KAMATI YA KATIBA SHERIA NA UTAWALA BORA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

NA-NAFISA MADAI (HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala Bora ya Baraza la Wawakilishi imewataka wafanyabiashara kutoigeuza hatua njema ya serikali ya kupandisha kiwango kipya cha mishahara kuwa kichocheo cha tamaa binafsi kwao na kupandisha bei za bidhaa kiholela.

Hayo yalisemwa leo na mjumbe wa kamati hiyo Ismail Jussa Ladhu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo alipokuwa akisoma hotuba ya kamati yao katika Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Aidha kamati hiyo imesema kwamba serikali imeamua kupandisha kiwango kipya cha mishahara kwa asilimia 25% katika Bajeti hii ya mwaka 2011/12 bila ya kupandisha viwango vya kodi au kuanzisha kodi yeyote mpya katika mwaka huu wa fedha jambo ambalo linapaswa kupongezwa.
Akizungumzia suala la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Mjumbe huyo alisema Kamati hiyo imeridhishwa na utendaji kazi wa Mkuu wa Ofisi hiyo kwa kazi nzuri inazozifanya jambo ambalo limepelekea mageuzi makubwa ya kiutendaji kazi katika ofisi anayoiongoza.

Alisema kuwa, Kamati inatoa wito kwa Serikali kuitumia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kama kigezo chema ya vipi Ofisi zetu na utendaji wao wa kazi unapaswa kuwa.

Kamati hiyo imeiomba Serikali kuendelea kuitafutia fedha ili zikamilishe mradi wa marekebisho makubwa ya jengo la ziada la ofisi walilolinunua kwa lengo la kufanyika vyema kazi zao kwa taifa.
Akizungumzia suala la Chuo Cha Utawala wa Umma cha Zaznibar amesema kuwa Kamati haikufurahishwa na kitendo cha chuo hicho kushindwa kuwasilisha mbele yake kumbukumbu sahihi za mapato yake yanayotokana na ada za masomo zinazotozwa na jinsi yanavyotumika.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye alisoma hotuba ya kamati hiyo kwa niaba ya Kamati yake alisema kuwa chuo hicho kimewasilisha makisio ya mapato na matumizi ya chuo kwa mwaka ujao wa Fedha badala ya mapato kama ilivyotakiwa.
Alisema kuwa kamati yao imeona kuwa hali hiyo haipaswi kuachwa ikiendelea na ofisi inapaswa kulifuatilia suala hili na kujua hali halisi ya mapato na matumizi ya chuo hicho.
Juu ya Utawala Bora Kamati imeitaka Idara hiyo kuchukua hatua za kuwasilisha yale yanayoripotiwa katika taarifa hizo katika wizara na taasisi za umma zinazohusika ili hatua za marekebisho ya hali ya haki za binadamu ziwezekuchukuliwa na kuzidi kuipandisha chati Zanzibar katika uwanja huo.

No comments:

Post a Comment