
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imekiri kwamba kitengo chake cha wagonjwa mahututi (ICU) kipo katika hali mbaya kutokana na uchakavu wa vifaa vyake kuwa ni va muda mrefu.
Naibu Waziri wa Afya Dk Sira Ubwa Mamboya aliyasema hayo wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujuwa mikakati ya kuimarisha kitengo cha ICU ikoje kufuatia kukabiliwa na upungufu wa vifaa.Dk Sira alikiri kuwepo kwa uchakavu wa vifaa vilipo katika kutengo hicho cha wagonjwa mahututi na ambapo baadhi yake vimechakaa na havipo katika kiwango kizuri kinachotakiwa kwa sasa.
“Mheshimiwa spika wizara yangu inalitambuwa tatizo hilo la uchakavu wa vifaa vya kitengo cha wodi ya wagonjwa mahututi ICU na kwa sasa tunafanya mawasiliano na baadhi ya nchi wahisani kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kwa sababu sote tunafahamu umhimu wa kitendo hicho. Hapa Zanzibar ni sehemu pekee yenye kulazwa wagonjwa mahututi ni hospitali yetu kuu ya Mnazi Mmoja” alisema.
Naye Waziri wa wa wizara hiyo, Juma Duni Haji akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo alisema vifaa vya kitengo cha wagonjwa mahututi kwa kawaida ni ghali sana na bajeti ya wizara katika kupatikana vifaa mbali mbali ni ndogo sana.
Alisema wastani zaidi ya shilingi bilioni moja zinahitajika kwa ajili ya kupata vifaa vya kitengo cha wagonjwa mahututi na fedha hizo ni nyingi na wizara haina uwezo huo kwa wakati huu.
“Wajmbe wa baraza hili wote ni mashahidi juu ya bajeti yetu tuliotengewa ni ndogo sana kulingana na mahitaji yetu, bajeti haiwezi kuhudumia na kufanya mambo mengi kama kununuwa vifaa vya kitengo cha wagonjwa mahututi ICU kwa sababu vifaa vyake ni ghali sana lakini tuna hamu kubwa ya kukiimarisha kitendo chetu hicho”Alisema Duni.
Duni alisema katika hatua za awali wamefanya mazungumzo na serikali ya watu wa China kuhusu kusaidiwa kwa kitengo hicho na wanasubiri majibu yake na iwapo serikali hiyo itakisaidia itakuwa ni faraja kubwa kwa seikali ya Zanzibar.
Waziri huyo aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi vifaa vya kitendo cha ICU vilitolewa na moja ya taasisi moja ya Kikristo ambayo iliisaidia hospitali ya Mnazi Mmoja wakati huo ikiitwa V.I Lenin.
Duni alisema vifaa vya kitendo hicho ni ghali sana lakini serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imekuwa na dhamira nzuri ya kuwapatia wananchi wake afya bora kama ilivyoahidiwa na rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Sheni wakati alipokuwa akinadi sera zake kama akichaguliwa kuwa rais wa Zanzibar katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.
No comments:
Post a Comment