| Chiligati: Viongozi CCM walijisahau |
| Zulfa Mfinanga, Shinyanga NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kapteni John Chiligati, amesema hatua ya chama hicho kupoteza sifa, imetokana na vitendo vya viongozi wake kuacha kushughulikia matatizo ya wanyonge na kukifanya chama kuwa cha kwao. Kapteni Chiligati aliyasema hayo jana mjini Shinyanga, baada ya kushiriki katika shughuli za usafi katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya 50 ya Uhuru wa Tanzania. "Hili tutaendelea kulizungumza sana katika vikao vyetu, kwa kuwataka viongozi washuke chini na kusikiliza matatizo ya wanyonge na kuyashughulikia. Tumepoteza sifa kwa sababu tulijisahau kushuka chini ambako kuna wananchi wengi," alisema Chiligati. Hata hivyo, aliwataka vijana kuacha tabia ya kuchagua kazi na badala yake, wajitume katika kufanyakazi ili waweze kujikwamua kimaisha. Alisema hivi sasa vijana wengi wamekuwa na tabia ya kuchagua kazi, jambo linalosababisha wengi wao kujiingiza katika vitendo viovu kwa kutaka maisha mazuri na ya haraka. "Kazi ni kazi lakini simaanishi kuwa watu wafanye kazi yoyote kwani hata wizi ni kazi, bali wafanye shughuli yoyote halali inayowapatia kipato, lakini cha ajabu vijana wengi wanachagua kazi, kwanza watambue kuwa kazi ni heshima, na pia kwa kufanya kazi utaweza kuwasaidia hata wasiojiweza," alisisitiza. Naibu katibu huyo, yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya siku mbili ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru na kesho atakuwa katika Wilaya Kahama. |
No comments:
Post a Comment