| Ticts wapuuza agizo la Kikwete |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete Na Raymond Kaminyoge KAMPUNI ya Kupakia na Kupakua Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam (Ticts) imepuuza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kutaka iilipe Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Dola za Marekani 261,000 ambazo inadaiwa kwa kuondoa makontena bandarini. Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac), imekitafsiri kitendo hicho kuwa ni sawa na kuwatukana Watanzania.Mwenyekiti wa Poac, Zitto Kabwe, alisema kitendo cha Ticts kupinga kulipa fedha hizo hata baada ya kuagizwa na Rais Kikwete, kimeisikitisha kamati yake na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo. Rais alitoa agizo hilo baada ya kutembelea bandari hiyo mwaka jana na kukuta msongamano mkubwa wa makontena na kuiagiza TPA kuyaondoa makontena hayo haraka. Jukumu la kuyaondoa makontena hayo lilikuwa la Ticts. "Tunataka ufafanuzi kuhusu fedha ambazo Ticts inadaiwa na TPA zimefikia wapi wameshazilipa," alihoji Zito kwa niaba ya kamati. Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Idd Mkwata, alisema Ticts imekataa kulipa fedha hizo kwa madai kuwa hakuna mkataba iliyoingia na TPA kuhusu uondoaji wa makontena hayo. "Ticts wamekataa kulipa fedha hizo kwa kuwa wanasema hawakuingia mkataba wala mazungumzo na TPA, ili kuondoa makontena hayo," alisema Mkwata. Zitto alihoji kwa nini wasilipe fedha hizo wakati makontena yaliondolewa na TPA na kupelekwa katika bandari ya nchi kavu."Kwa hiyo Wizara ya Miundombinu na TPA mmechukua jukumu gani baada ya wazungu kukataa kulipa fedha hizo au mnawaogopa wazungu," alihoji Zito. Kwa upande wake, Mkwata alisema rais aliagiza uongozi wa bandari, wizara ya Miundombinu na Ticts kukutana ili kuzungumzia suala hilo."Lakini tangu Februari 2 mwaka huu tulipoagizwa na rais tukutane, hatujawahi kufanya hivyo, kwa kuwa Ticts hawataki,"alisema. Zitto `akawacharukia ’ wizara ya Miundombinu kwa kuhoji hatua walizochukua baada ya agizo la rais kudharauliwa na Ticts.Mwakilishi wa wizara hiyo, mhandisi Saad Fungafunga, alisema bado juhudi zinafanywa ili pande hizo tatu ziweze kukutana. Hata hivyo Zitto aliwahoji viongozi wa bandari kuhusu manunuzi yaliyofanyika yenye thamani ya Sh 1.2 bilioni, bila kufuata sheria za manunuzi. Alisema katika taarifa ya bandari, baadhi ya manunuzi yamefanyika bila ya kutangazwa kwa zabuni kama sheria za nchi zinavyoeleza.Kufuatia kasoro zilizojitokeza, Zito aliikataa ripoti ya fedha ya TPA na kutoa maagizo.Katika maagizo hayo, alitaka Ticts wafikishwe kwenye Kamati ya Bunge ya Maadili kwa kudharau agizo la rais. Pia TPA waipelekee tena Ticts taarifa za kudai fedha hizo.Pia Zitto alitaka TPA kutoa ufafanuzi kuhusi matumizi ya fedha bila kufuata kanuni za manunuzi.Pia aliutaka uongozi wa bandari kuitisha mkutano wa wadau wa Maendeleo mkoani Mtwara, ili kuwapa taarifa kuhusu wawekezaji waliokodi sehemu ya Bandari ya Mtwara. "Haiwezekani mnafanya jambo bila kuwashirisha viongozi wa mkoa kwani hao ndiyo wadau wa maendeleo ya eneo hilo, kwani mnaficha nini," alisema Zitto aliwataka viongozi wa bandari kuheshimu na kuhudhuria vikao vya kamati kwa kuwa viko kwa mujibu wa sheria. Hatua hiyo inafuatia Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraem Mgawe na viongozi wengine kutohudhuria kikao hicho kwa madai kuwa wako safarini nje ya nchi. |

No comments:
Post a Comment