Thursday, 30 June 2011

Tabia ya ubakaji wa watoto katika jamii ya visiwa vya Zanzibar

Tabia ya ubakaji wa watoto katika jamii ya visiwa vya Zanzibar, inaonekana ikizidi kuota mizizi siku hadi siku kutokana na ufatiliaji usio makini wa vyombo vya sheria, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limewachosha wananchi na kukata tamaa kabisa ya kupata haki pindipo watoto wao wanapopatwa na kadhia ya ubakaji .
Wengi wetu tunajiuliza ni kwa nini iwe hivi kila siku utasikia kesi imekosa ushahidi na matokeo yake kuishia visivyojulikana bila ya kujali athari alizozipata mtoto lakini cha kusikitishwa wabakaji kuachiwa watambe mitaani wakiwa hawana hata chembe ya wasi wasi.

Hii ndio hali halisi iliyozoeleka kwa muda mrefu sasa, hadi masikio yetu yamezoea kusikiliza leo mtoto wa Fulani kabakwa na kesho wa Fulani lakini kesi zao hazina ushahidi wa kumtia mtendaji wa kosa hatiani.

Hebu tujiulize kukosa ushahidi kwa kila kesi za ubakaji na udhalilishaji ndio utendaji sahihi wa kazi? utendaji ambao unawapa fursa watu wenye roho za kinyama kuendeleza vitendo vya ubakaji huku wakijua dhahiri kwamba hakuna kitakachofanyika dhidi yao .

Hivi karibuni Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, alikemea vikali kuhusu ongezeko la vitendo hivi na kuitaka idara ya mahakama kuacha tabia ya kuzipiga danadana kesi za ubakaji na kutaka zishughulikiwe haraka iwezekanavyo.

Alionesha kukasirishwa sana na utendaji wa vyombo vya sheria kwamba inasikitisha kuona kesi zinazofunguliwa zinaishia kilholela kwa kisingizio cha kukosa ushahidi hata pale mtuhumiwa anapopatikana akiwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo.
Kutokana na utendaji huu usio wa uhakika isipokuwa ni nenda rudi ya kila siku bila mafanikio, ni lazima wananchi wakose imani ya kuripoti kesi zao katka vituo vya sheria na hatimae kufikia kuchukua hatua mikononi mwao jambo ambalo kisheria halikubaliki.
“haiwezekani kuwaachia wabakaji watambe, mahakama nenda rudi zisikuwepo kama ushahidi upo sheria ichukue mkondo wake, haipendedezi mbakaji kukutwa juu ya mgongo bado hakuna ushahidi mnataka ushahidi gani?”alihoji Balozi Iddi .
Wakati akifungua kituo cha kuwahudumia waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto (One Stop Centre ) kilichopo katika hospitali ya Mnazi mmoja mjini Zazibar,

Balozi Iddi aliitaja idadi ya watoto waliobakwa tangu mwaka 2006 hadi kufikia mwaka 2010 imefikia 3,116 matukio ambayo yameripotiwa katika hospitali ya Mnazi mmoja , Makunduchi, kivunge, Abdalla Mzee, Chake Chake na Wete ambapo kati ya takwimu hizo yamo matukio ya ubakaji na mamba za utotoni.
Kwa kweli juhudi za Serikali katka kupambana na tatizo la makosa ya ubakaji na udhalilishaji kwa wanawake na watoto ni kubwa sana ili kuona matendo hayo yanafikia kikomo, lakini bila ya mashirikiano ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa au kumwaga chumvi baharini.

Kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu itayowezesha kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na lengo kuu ni kuona kazi zinazohitajika zinafanyika ipasavyo pamoja na kuwarejeshea matumaini wananchi hasa wale wanaofikwa na matatizo hayo kama ni watu wenye mahitaji muhimu, na kukifanya kituo kuwa endelevu na sio Non Stop Centre badala ya One Stop Centre.

Itakuwa ni jambo la busara sana kama kituo hichi kitahakikisha kinapambana na wale wote wenye tabia ya kuendeleza vitendo vya udhalilishaji vikiwemo ubakaji kwa wanawake na watoto na hakuna budi kufanya kazi kwa bidii bila ya kuoneana aibu ambayo mwisho wa siku inatuweka katika rekodi mbaya ya kuwa na idadi kubwa ya kesi za udhalilishaji na ubakaji.

Mkoa wa Kaskazini unguja umetajwa kuwa ndio unaongoza kwa matendo ya ubakaji jambo ambalo lilikemewa vikali na mhe Balozi Seif ikizingatiwa ndio mkoa wake anakotoka, amewataka waache mara moja vitendo hivyo na wale wataobainika kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa dhidi yao.

Ni mara nyingi sana kusikia kuhimizwa kwa polisi, madaktari na wanasheria kufanya kazi zao kwa mashirikiano na umakini mkubwa, ikizingatiwa wao ndio wadau wakubwa wa kikimbiliwa pindipo yanapotokea matatizo na wanategemewa kuwa waadilifu katika kuyapatia ufumbuzi.

Kufunguliwa kwa vituo vya kutoa huduma za matendo yatokanayo na udhalilishaji wanawake na watoto ni miongoni mwa juhudi za serikali katika kujivua gamba la aibu la kuwa na wimbi kubwa la kesi za udhalilishaji ambazo hazitafutiwa ufumbuzi wowote, hivyo basi kinachohitajika kuonekana ni utendaji wa kazi na haki bila ya kujua mtendaji wa kosa ni nani na ana cheo gani.

No comments:

Post a Comment