Saturday, 4 June 2011

RAIS KIKWETE ANATARAJIWA KUZINDUA MPANGO WA KWANZA WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO (2011/12 – 2015/16) WA KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuzindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) wa Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 Jumanne ijayo mjini Dodoma.

Uzinduzi wa Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioandaliwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango unatokana na uamuzi wa Mheshimiwa Rais na Serikali yake kuirejesha nchi kwenye utaratibu mzuri wa kupanga maendeleo yake ya muda mrefu, wa kati na mfupi. Pia kuratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango.

Vilevile Serikali ilifanya uamuzi wa kutazama upya shabaha na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kuihuisha panapostahili na kuandaa mkakati wa kutekeleza Dira kwa miaka 15 ijayo.

Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 na mkakati wake utagawanywa katika vipindi vitatu vya miaka mitano mitano, kila kipindi kikiwa na mpango wake wa maendeleo.

Dhana ya Mpango wa Maendeleo wa sasa ni “Kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi wa Tanzania”. Mpango unaozinduliwa Jumanne ni awamu ya kwanza ya Mpango Elekezi (roadmap) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025 kwa kipindi cha miaka 15 iliyobaki.

Uzinduzi huo utahudhuriwa na makundi mbali mbali ya wadau wa maendeleo wakiwamo wananchi, viongozi wa Serikali, wabunge, mabalozi, taasisi na mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali.

Imetolewa na;

Dkt. Philip Mpango

KATIBU MTENDAJI

OFISI YA RAIS – TUME YA MIPANGO

No comments:

Post a Comment