Profesa Lipumba alia na Mkulo

Zikiwa zimesalia siku tatu kusomwa kwa mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, kwa takriban wiki tatu sasa, kumekuwa na ugumu wa kupata taarifa za Wizara ya Fedha na Uchumi kupitia mtandao wa kompyuta.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam katikati ya wiki hii, zinaeleza kuwa hali hiyo inatokana na tovuti ya wizara hiyo kutokuwa hewani.
Kwa mujibu wa habari hizo hali hiyo imesababisha wadau kushindwa kufanyia tathmini mapendekezo ya bajeti hiyo.
Mapendekezo ya bajeti hiyo yanatarajiwa kusomwa Jumatano ijayo na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, katika Mkutano wa Nne wa Bunge, unaotarajiwa kuanza mjini Dodoma, keshokutwa.
Miongoni mwa wadau wakubwa wa bajeti hiyo waliojitokeza hadharani kulalamikia tatizo hilo, ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Lipumba ambaye ni miongoni mwa maprofesa bingwa, alisema ni takribani wiki tatu amekuwa akihangaika kupata taarifa kuhusu bajeti ya serikali kwa ajili ya kufanyia tathmini na uchambuzi, kupitia tovuti ya wizara hiyo.
Hata hivyo, alisema juhudi zake zimekuwa zikigonga ukuta, kila anapojaribu kutafuta taarifa hizo, kutokana na tovuti ya wizara hiyo kutopatikana kwenye mtandao wa kompyuta.
“Jambo lingine ni hili, zaidi ya wiki mbili sasa, tovuti ya Wizara ya Fedha haifanyi kazi, haipatikani. Tunashindwa namna ya kufanya tathmini kuhusu bajeti inayopendekezwa na serikali,” alisema Profesa Lipumba alipozungumza na NIPASHE.
Taarifa kuhusu suala hilo, zilipatikana ndani ya kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi kilichofanyika kati yake na watendaji na wataalamu wa wizara hiyo wakiongozwa na Waziri Mkulo, katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, Jumatano wiki hii.
No comments:
Post a Comment