Misri: Mapigano mapya yazuka Tahrir
mamia ya waandamanaji wakiwa eneo la wazi la Tahrir
Polisi nchini Misri wamepambana na mamia ya waandamanji wanaoipinga serikali mjini Cairo katika eneo la wazi la Tahrir na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa.
Polisi wa kuzuia ghasia walitumia mabomu ya machozi kujaribu kutawanya waandamanaji, wengi wao waliwarushia mawe polisi.Uwanja wa Tahrir ulikuwa kitovu katika mageuzi ya mwezi Februari yaliyosababisha Rais Hosni Mubarak kuachia madaraka.
Wengi wa waandamanaji walikuwa wanataka kesi za maafisa wa zamani ziendeshwe kwa haraka.
Hadi kulipopambazuka alfajiri, mawe na vioo vilikuwa vimetapakaa mitaani karibu na eneo la Tahrir.
Walioshuhudia walisema ilikuwa ni ghasia mbaya kuwahi kutokea katika wiki kadhaa.
Vurugu zilianza Jumanne wakati polisi walipowafukuza katika ofisi za Televisheni ya Taifa wanafamilia wa wale waliouawa katika vurugu za mwezi Februari, wanaharakati walisema.
Baadaye waandamanaji walikusanyika nje ya ofisi za wizara ya mambo ya ndani na kupambana na polisi.
Mapigano yalisambaa na kufika katika eneo la Tahrir ambako polisi waliokuwa na ngao za kuzuia ghasia waliwazuia kuingia katika mitaa mikubwa ambayo ilikuwa na magari kadhaa ya usalama.
Wakati mabomu ya kutoa machozi yakimiminika majeruhi walionekana wamelala chini baadhi wakititikwa na damu
"Watu wanataka kuondolewa kwa utawala," baadhi ya waandamanaji walikuwa wakiimba.
Ahmed Abdel Hamid, mwenye umri wa miaka 26, ambaye alikuwa miongoni mwa waandamanaji alisema watu walikuwa wamekasirika kwa kuwa kesi mahakamani dhidi ya maafisa waandamizi zilikuwa
zinacheleweshwa.
Wiki iliyopita waziri wa zamani wa Biashara nchini humo Rachid Mohamed Rachid alihukumiwa miaka mitano jela bila kuwepo mahakamani kwa ubadhirifu wa fedha za umma.
No comments:
Post a Comment