Maalimu Seif ataka CCM kuchukua uamuzi mgumu
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad, amesema CCM, inapaswa kuchukua uamuzi mgumu katika kupambana na rushwa ndani ya chama hicho.Amesema uamuzi huo upaswa kuchukuliwa mapema kabla madhara makubwa hayajajitokeza. Maalim Seif alisema hayo juzi jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha 'Je Tutafika' kinachorushwa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten. Alisema CCM imefikia mahali kwamba kama mwanachama hana fedha hawezi kuchaguliwa katika nafasi za uongozi,hata kama mtu huyo anakubalika na wananchi wanaomzunguka. "Uamuzi mzito unapaswa kuchukuliwa ndani ya chama hicho ili kurudisha maadili ya zamani ya sitatoa wala kupokea rushwa,"alisema Hamad ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar wakati wa chama kimoja cha CCM. Alisema "uamuzi wa kujivua gamba nadhani unatafsiriwa vibaya, lakini maana yake ni kujirekebisha na kurudi katika maadili ya zamani. Lakini kujivua gamba kusichelewe, ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni." Maalim Seif alisifu utendaji kazi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere ambaye hakuchelewe kumshughulikia mtu aliyejihusisha na vitendo vya rushwa. "Mwalimu alikuwa na vyanzo vingi vya kujipatia taarifa, hakutegemea vyombo vya serikali pekee, aliwatumia watu wa kawaida hata kwenye mchezo wa bao ili kumpa taarifa hivyo aliwashughulikia wapenda rushwa na hakufanya hivyo kwa kuwaonea,"alisema Hamad. Alisema ubaya wa rais kutegemea vyombo vya serikali kumpa taarifa ni kwamba vyombo vingi humpa taarifa hata kama ni za uongo ili kumfurahisha. Maalim Seif alisema ushahidi wa vitendo vya rushwa ndani ya chama hicho ni namna viongozi wengi walivyokamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mwaka jana katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho. "Hali ile ilionyesha kwamba hali si shwari ndani ya CCM, maadili waliyojiwekea wenyewe sasa hawayafuati... uamuzi mgumu na wa haraka unatakiwa kuchukuliwa ndani ya chama hicho,"alisema Hamad. Viongozi wa upinzani Makamu huyo wa rais, amewataka viongozi wa vyama vya upinzani kukosoa bila kutumia lugha zinazoweza kuchochea vurugu nchini. Alisema wafuasi wa vyama vya upinzani wako tayari kufanya vurugu ikiwa viongozi wao wataruhusu kufanya hivyo. "Tukosoane kwa kutumia maneno ya kistaarabu ili kuepusha vurugu ili amani iliyodumu kwa muda mrefu iendelee kuwepo na kufurahiwa, Tanzania ni yetu sote,"alisema Hamad. Maandamano Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Hamad alisema ni kosa kwa polisi kuzuia maandamano bila kutoa sababu za msingi."Maandamano ni haki ya vyama vya siasa,polisi wanajulishwa ili kutoa ulinzi, lakini polisi wanapokataza maandamano bila ya kuwa na sababu za msingi ni kutofahamu haki za wananchi,"alisema. Pia alisema vyama vyenye wafuasi wengi ambao wanajaa kwenye maandamano na mikutano ya hadhara iwe changamoto kwa chama tawala kujitathimini kwa nini hali hiyo inajitokeza hivi sasa. |

No comments:
Post a Comment