Monday, 6 June 2011

CUF yatangaza maandamano kupinga mauaji ya raia

 
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) akizungumza na waandishi habari nje ya Kituo cha Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaa baada ya juhudi zake za kumwekea dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kugonga mwamba.
Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza kuandaa maandamano ya amani yatakayoongozwa na Mwenyekiti wake Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, viongozi waandamizi na baadhi ya wabunge wa chama hicho, kwa lengo la kulaani mauaji dhidi ya raia, ambayo yamekuwa yakifanywa na polisi katika maeneo mbalimbali nchini.
Tamko la maandamano hayo lilitolewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Shaweji Mketo, alipozungumza na waandishi wa habari, katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema maandamano hayo yatafanyika Jumapili ijayo na yataanzia eneo la Ubungo Mataa saa 3.00 asubuhi na kuishia katika viwanja vya Bakhresa Manzese, ambako mkutano wa hadhara utafanyika.
“Kupitia kalamu zenu tunaomba kuwafahamisha umma wa wapenda haki wote na Watanzania kwa jumla kwamba CUF itafanya maandamano makubwa hapa jijini Dar es Salaam siku ya tarehe 12 Juni 2011,” alisema Mketo.
Alisema miongoni mwa mauaji ambayo CUF itatumia maandamano hayo kuyalaani, ni pamoja na yale ya Mei 16, mwaka huu, ambayo polisi waliwaua raia wanne kwa kuwapiga risasi katika Kijiji cha Matongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara kwa madai ya kukusanyika katika eneo la mgodi wa North Mara wakiwa na nia ya kupora mchanga wa dhahabu.
Mketo ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Bunge, alisema pamoja na mauaji hayo, wabunge wawili wa Chadema; Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalum) pamoja na wanachama wengine waandamizi wa chama hicho walikamatwa na polisi na kuwekwa rumande.
Alisema pia waandishi wa habari watatu; akiwamo Anthony Mayunga (Mwananchi), Beldina Nyakeke (The Citizen) na Anna Mroso (Nipashe), nao walikamatwa na polisi katika harakati za kuzuia wananchi kutopata ukweli wa matukio yanayofanywa kwa nia ya kuficha maovu yao.
Mketo alisema wakati hayo yakiendelea, Mei 24, mwaka huu, polisi pia waliua raia mmoja kwa kumpiga risasi Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora.
Alisema walifanya mauaji hayo baada ya kuvamia Kijiji cha Shela, kilichopo Kata ya Ngusa katika Jimbo la Urambo Magharibi na kupora ng’ombe zaidi 6,000 na kuwapeleka makao makuu ya Kata ya Usinge kwa madai kwamba, mifugo hiyo inakula majani katika eneo la hifadhi.
 Alisema siku iliyofuatia, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Shela wakati akifuatilia tukio la kukamatwa kwa mifugo hiyo lililoripotiwa na wakazi wa kijiji chake, alipofika katika eneo, ambalo mifugo inashikiliwa, naye alikamatwa, kupigwa mpaka kuvunjwa mguu na polisi.
 Mketo alisema Mei 27, mwaka huu, CUF iliamua kuwatuma baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, akiwamo Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya na kwamba walipofika wilayani humo, walikamatwa na polisi na hadi sasa wanashikiliwa rumande baada ya kunyimwa dhamana.
 “Jambo la kusikitisha zaidi miongoni mwa watu waliokamatwa ni Zainabu Nyumba, ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), pamoja na hali yake hiyo, huku Jeshi la Polisi likifahamu hana hatia, bado walimkamata na kumsweka rumande hadi leo tunapozungumza,” alisema Mketo.
 Alisema kunyimwa dhamana kwa watuhumiwa hao, ni mwendelezo wa vitendo vya hujuma dhidi ya CUF na viongozi wake kwa kuwa wanaamini kukamatwa kwao kumetokana na mashinikizo ya kisiasa kutoka kwa wapinzani wao na si kwa kuwa walitenda kosa lolote lililostahili wao kutiwa nguvuni.
 Kutokana hayo, alisema wataandamana kwa kuwa wakati huo, wananchi wengi katika Jimbo la Urambo Magharibi, wamekuwa wanakamatwa na polisi na kubambikiwa kesi.
 “Kitendo cha polisi kufanya matukio ya kinyama huku serikali ikiwa kimya inadhihirisha ni jinsi gani serikali yetu ilivyo dhaifu, butu isiyo na meno wala uwezo wa kuwatetea raia zake. Tunaomba wananchi kuamka na kukataa kwa nguvu zote juu ya aina yoyote ya unyanyasaji na uonevu unaofanywa na jeshi hili,” alisema Mketo.

No comments:

Post a Comment