Thursday, 26 May 2011

Ndege za kimataifa kutua Tanzania
Daniel Mjema,
Moshi
SERIKALI imeanzisha mkakati kamambe wa kuhamasisha mashirika makubwa ya kimataifa ya ndege duniani kuanzisha safari za moja kwa moja hadi nchini ili kuinua soko la utaliii nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige alisema tayari shirika la ndege la Jet Airways la India limeonyesha nia ya kuanza safari za kimataifa moja kwa moja kuja nchini kutokea mataifa mbalimbali duniani.

Maige alitoa kauli hiyo jana katika lango kuu la kupandia Mlima Kilimanjaro la Machame wilayani Hai wakati wa sherehe za kuwaaga watalii 150 kutoka nchi za Marekani na Mexico.

Watalii hao wakiongozwa na Rais wa Global Football, Patrick Steenberge ni wachezaji wa timu za Drake Univesity na Conadelp walioshiriki mechi ya kihistoria ya American Football iliyochezwa jijini Arusha.

“Siku chache zilizopita nilikuwa India na tumezungumza na wawekezaji wakubwa na sasa tuko katika mazungumzo na Jet Airways na tuko hatua za mwisho ili waanze safari za moja kwa moja kuja nchini,”alisema Maige.

Waziri Maige alisema serikali imefanya kazi kubwa ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya ndani licha ya sekta ya usafiri kukabiliwa na matatizo makubwa.

Kwa mujibu wa Maige, Kenya inafanya vizuri katika sekta ya utalii licha ya kuwa na vivutio vichache kulinganisha na Tanzania kwa kuwa kuna ndege nyingi za kimataifa zinazotua Kenya kutoka mataifa mbalimbali.

Alisema Tanzania inatumia wachezaji hao kutangaza utalii wa ndani na kwamba  kwa kuwa mechi iliyochezwa Arusha iliandikwa katika magazeti makubwa 250 Marekani na Mexico.

Maige alisema serikali imeamua kuwaondolea ada ya kupanda mlima huo ambayo ni Dola 700 za Marekani kwa kila mtalii ili wawe mabalozi wazuri wa kuutangaza mlima huo duniani.

Waziri Maige alimhamasisha Steenberge kufika kileleni kwa kuwa tukio hilo litaitangaza vyema Tanzania na kumpa ofa ya kutembelea mbuga ya Selou endapo atafanikiwa kufika kileleni.

Kwa upande wake, Steenberge alisema anajisikia fahari kupanda mlima huo mrefu barani Afrika.“Mheshimiwa Waziri nakuhakikishia kuwa nitajitahidi kufika kileleni,”alisema Steenberge.

1 comment:

  1. Jet Airways za India kwa mwaka zinadondoka Tano mbaya zaidi zikiwa zinakaribia kutua uwanjani zinapoteza mueleko, this is for sure mm nipo India na kila mwaka linatokea hlo zisiletwe Tz hzo wahindi wenyewe wamekua wakiziogopa siku hzi

    ReplyDelete