Hospitali ya Rufaa Mnazimoja Z`bar hoi
-Mashine zote za ICU ni mbovu
-Hazijawahi kufanyiwa matengenezo
-Viyoyozi pia vimekufa, hewa ni madirishani
-Matengenezo kusubiri bajeti ya serikali
Mashine tano za huduma kwa wagonjwa mahututi, ziitwazo Monitor Machine zimeharibika katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimoja kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, imebainika.
Kwa kawaida mashine hizo aina ya HP/Hewlett Packard, huwasaidia madaktari kujua mwenendo ya mgonjwa aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Uchunguzi wa NIPASHE JUMAPILI, umebaini kwamba mashine hizo zilianza kuharibika moja baada ya nyingine kuanzia mwaka jana na hadi Januari mwaka huu zote ziliharibika.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa mashine hizo ziliwekwa miaka 10 iliyopita, lakini zimekuwa hazifanyiwi matengenezo kutokana na ukosefu wa mafundi wa kuzikagua na kuzitengeneza kwa kuzingatia teknolojia yake.
Kuharibika kwa mashine hizo kwa mujibu wa chanzo cha habari kilichoomba kuhifadhiwa jina, tayari umesababisha watu kupoteza maisha kwa kukosa uangalizi wa afya yao unaohitaji matumizi ya mashine hizo.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa viyoyozi aina ya Sanyo vilivyopo chumba cha ICU vimeharibika na kusababisha madirisha ya chumba hicho kuachwa wazi kuruhusu hewa kupita.
Chumba cha wagonjwa mahututi cha hospitali hiyo kina uwezo wa kupokea wagonjwa sita.
Katibu Msaidizi wa hospitali hiyo, Omar Juma, alithibitisha chumba hicho kukabiliwa na hali mbaya kwa kukosa vifaa hivyo. “ICU na yenyewe ipo ICU inahitaji matengenezo makubwa au kununuliwa vifaa vipya.”
Omar alisema uongozi wa hospitali hiyo tayari umepeleka makadirio ya bajeti ya karibu Sh. milioni 80 kugharamia utengenezaji wa vifaa hivyo.
Alisema matengenezo ya vifaa hivyo ni muhimu ili kuiwezesha hospitali kurejesha haraka huduma kwa wagonjwa.
Mmoja wa madakari bingwa katika hospitari hiyo, alisema mashine hizo huwawezesha madaktari kufahamu kiwango cha hewa safi (oxygen) katika mapafu ya mgonjwa mahtuti.
Alisema kuharibika kwa mashine hizo kumesababisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa kutofanyika kwa usahihi unaohitajika kitaaluma.
Daktari huyo ambaye pia aliomba jina lake kuhifadhiwa, alisema wagonjwa wenye matatizo ya kupumua husaidiwa kufanya hivyo kwa kutumia mitungi ya oxygen kwa kuunganisha mpira ili kumwongezea mgonjwa uwezo wa kupumua.
Alisema mashine hizo zilizoharibika pia hutumika kupima kupanda na kushuka kwa shinikizo la damu ya mgonjwa.
Alipohojiwa juu ya tatizo hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya, alisema lipo na tayari hatua za kutafuta ufumbuzi zimeanza kuchukuliwa.
Alisema hatua hizo ni pamoja na kupeleka bajeti serikalini ili kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa ICU mpya katika hospitali hiyo.
“Wakati tukiwa katika mpango wa kutengeneza mashine zilizoharibika pia tuna mpango wa kujenga kitengo kipya cha wagonjwa mahtuti na tunatarajia kupata fedha za mradi huo mwaka huu,” alisema.
Hospitali hiyo inakabiliwa na ukosefu wa vifaa hivyo muhimu katika huduma za afya, huku kukiwa na malalamiko juu ya serikali kuwanunulia magari ya kifahari watendaji wake wakuu wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Juhudi za kumpata Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji, hazikuweza kufanikiwa.
No comments:
Post a Comment