Wednesday, 13 April 2011

'Waliotaka wabunge wajiondoe Bungeni ni kundi la wahuni'

Midraji Ibrahim,
Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, amesema vijana waliotaka wabunge wa Zanzibar wajiondoe bungeni ni kundi la wahuni.
Akizungumza kwenye ofisi za Bunge jana, Suluhu alisema vijana hao ni wahuni na kwamba waliamua kufanya hivyo kwa utashi wao na sio kwa utashi wa watu wa Zanzibar.

Suluhu alisema masuala mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa Kamati ya Bunge Katiba, Sheria na Utawala wakati ikikusanya maoni kuhusu muswada wa kuundwa kwa tume ya marekebisho ya katiba yalikuwa ni mawazo tofauti ya wananchi.

“Wanapokusanyika watu lazima watakuwa na mawazo tofauti, siamini kama kuna Mtanzania hataki amani na usalama wa nchi yetu,” alisema.Alisema kifungu cha tisa katika muswada huo, kinabainisha vitu muhimu kwa taifa ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa kwenye katiba mpya na kwamba wananchi hawakatazwi kujadili jinsi ya kuviboresha.

Kuhusu kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi wakati wa serikali ya awamu ya nne, Suluhu alisema wamefanikiwa kuondoa vikwazo kwenye mgawanyo wa mapato.“Serikali ya Zanzibar inapata asilimia 4.5 ya misaada ya kibajeti. Kuanzia mwaka wa fedha 2009/10, SMZ imeanza kunufaika na asilimia 4.5 ya mikopo ya kibajeti,” alisema.

Katika hatua nyingine, Serikali SMZ imeanza kupata misamaha ya fedha ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kwamba dola 15.12 milioni za Marekani zilitumika kununulia magari, vifaa vya kilimo na vifaa vya Hospitali ya Mnazi Mmoja.

“Imekubalika kuwa SMZ inaweza kukopa ndani na nje ya nchi, chini ya udhamini wa Serikali ya muungano wa Tanzania,” alisema Suluhu.Kuhusu wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili, Waziri huyo alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imetengeneza mfumo mpya wa usawa wa kutathimini Tanzania bara na visiwani na kwamba umeanza kutumika Februari 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment