Serikali sasa kuhakiki tiba za magonjwa sugu |
Hadija Jumanne KATIBU Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, amesema serikali ipo mbioni kuhakiki tiba zinazotolewa na waganga walioibuka na kudai kuwa wanatibu magonjwa sugu, kama inavyofanywa na Babu wa Loliondo. Nyoni aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam,alipokuwa akipokea msaada wa dawa wenye thamani ya Sh30 milioni kutoka katika Shirika la World Vision."Hakuna mtu anayekatazwa kutumia dawa yoyote ile iwe ya serikalini ama tiba asili, lakini lazima tuzichunguze kwanza,"alisema Nyoni. Kwa mujibu wa Katibu mkuu huyo, kama dawa hizo zitathibitika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu, wizara haitakuwa tayari kuruhusu zitumike."Kama waganga hao watabainika kuwa wanatoa dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu na zile zisizokidhi matumizi ya uponyaji wa wagonjwa, watafungiwa mara moja," alisema Nyoni. Hadi sasa zaidi ya watu sita wamejitokeza kutoa tiba inayodaiwa kuponya magonjwa sugu, ukiwemo Ukimwi.Watu hao wapo katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Mbeya, Sengerema, Iringa na Loliondo mkoani Arusha. Akizungumzia msaada wa dawa hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Miradi ya Maendeleo katika World Vision hapa nchini, Anatoli Rugaimkamu, alisema umetolewa ili kusaidia kupunguza magonjwa ambayo hayakupewa kipaumbele ndani ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Alisema dawa hizo zitapelekwa katika mikoa mitano inayoongoza kwa wagonjwa wengi wa maradhi ya minyoo na kichocho."Kuna idadi kubwa hasa ya watoto wanaougua kichocho na minyoo na sisi tumeona ni vizuri tukaelekeza nguvu zetu katika maeneo hayo ili kupunguza vifo vya watoto wenye umri kati ya miaka sita na 15," alisema Rugaimkamu. Kwa mujibu wa Rugaimukamu,dawa hizo zitatolewa kwa wanafunzi wote wa shule za msingi katika Mikoa ya Dodoma,Manyara, Singida, Rukwa na Tabora.Alisema utoaji wa dawa hizo, utafanyika Agosti mwaka huu. |
No comments:
Post a Comment