Saturday, 16 April 2011

JWTZ haingilii kazi za jeshi la polisi

JIBU LA SWALI LA MBUNGE Tumbe

na Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imesema Jeshi la Wananchi (JWTZ), hufanya kazi katika matukio ya ndani hasa inapobaikina kuwa jeshi la polisi limezidiwa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alilieleza Bunge kuwa jeshi hilo linaweza kufanya kazi za polisi inapoombwa na baada ya kujiridhisha kuwa jeshi la polisi limezidiwa.
Waziri Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Rashidi Ali Abdallah (CUF), aliyetaka kujua ni wakati gani JWTZ linawajibika kufanya kazi za ndani badala ya jeshi la polisi.
Aidha, Waziri Mwinyi alisema msaada wa JWTZ kwa shughuli za ndani si katika masuala ya uraia tu bali jeshi linaweza kuombwa kusaidia katika shughuli nyingine, inapobidi kama vile shughuli za uokoaji, ujenzi hususan wakati wa dharura na majanga mbalimbali.
Alisema majeshi la ulinzi yatatumika pale panapotokea uvunjifu wa amani, au dalili za uvunjifu wa amani na inapodhihirika na mamlaka za kiraia kuwa polisi wamezidiwa.
Waziri huyo alisema majeshi ya ulinzi yanapotoa msaada huo hayachukui nafasi ya mamlaka za kiraia isipokuwa yanasaidia kudumisha sheria na amani.
Dk. Mwinyi, alisema kwa mujibu wa sheria kifungu Na. 21 cha sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 2002, Jeshi la Ulinzi wa Tanzania linaruhusiwa kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia pale ambapo kuna machafuko, ghasia au uasi pindi linapoombwa na mamlaka za kiraia pale ambapo mamlaka hizo haziwezi kuzuia au kumaliza vurugu ama machafuko au maasi.
Alisema Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania linaweza kufanya jukumu la ulinzi wa vituo muhimu nchini endapo uwezo wa polisi ni mdogo.

No comments:

Post a Comment