Tuesday, 19 April 2011

FATMA FEREJI KUFUNGA MAFUNZO YA POLISI ZANZIBAR


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Fatuma Fereji, Alhamisi ijayo Aprili 21, mwaka huu, atakuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za kufunga mafunzo ya kujiendeleza kwa askari Polisi yanayofanyika kwenye Chuo cha Taaluma za Polisi Zanzibar (Zanzibar Police Academy).
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Afisa Uhusiano wa Jeshi hilo Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, imesema kuwa sherehe hizo zitakuwa na wahitimu 806 wa vyeo vya Koplo, Sajenti na Sajinimeja.

Insp Mhina amesema Ratiba ya sherehe hizo iliyotolewa na Mkuu wa Chuo hicho Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Maulidi Mabakila, inaonyesha kuwa shughuli za ufungaji wa mafunzo hayo zitakazofanyika kwenye viwanja vya Polisi Ziwani, zitaanza 2.30 asubuhi kwa gwaride la wahitimu kuingia uwanjani kabla ya kukaguliwa na Mgeni Rasmi na kufuatiwa na hotuba.

Mkuu wa Chuo hicho ACP Mabakila, amesema kuwa Sherehe hizo pia zitahudhuliwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Vikosi vya SMZ.

Wengine ni Wakuu wa Vyuo vya Polisi vya Dar es Salaam, Moshi na Kidatu Morogoro pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Wananchi wa Viunja vya mji wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment