JK ateua, ahamisha Makatibu Wakuu
.jpg)
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo
Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya Makatibu Wakuu na kumwondoa Dk. Ladslaus Komba kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mabadiliko hayo yanaifanya wizara hiyo kuongozwa na Makatibu Wakuu watatu tangu serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani Desemba, 2005.
Katibu Mkuu wa kwanza ni Salehe Pamba ambaye alifuatiwa na Blandina Nyoni kisha kurithiwa na Komba, ambaye kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, jana, amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo atapangiwa kazi nyingine.
Kwa mujibu Luhanjo, Rais Kikwete amewateua Makatibu Wakuu watano wapya, kati ya hao wanne walikuwa ni manaibu katibu wakuu wa wizara.
Rais Kikwete pia amewahamisha makatibu wanne kutoka wizara moja kwenda nyingine kutokana na muundo mpya wa serikali na baadhi yao kustaafu.
Taarifa ya Luhanjo ilieleza kuwa madiliko hayo pia yanatokana na muundo huo Serikali baada ya Wizara ya Miundombinu kugawanywa katika wizara mbili na makatibu wakuu kustaafu kazi kwa mujibu wa Sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kikwete amemteua Fanuel Mbonde kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi wake Mbonde alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hussein Kattanga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), John Haule Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Balozi Herbert Mrango Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Eric Shitindi Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira.
Kabla ya uteuzi wake Kattanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Haule Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Balozi Mrango Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Shittindi Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Rais Kikwete amemhamisha Sazi Salula kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais; Maimuna Tarishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii; Omar Chambo kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi akitokea Ukatibu Mkuu wa Wizara ya zamani ya Miundombinu na Kijakazi Mtengwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Rais Kikwete pia amemhamishia Elizabeth Nyambibo Wizara ya Fedha na Uchumi ambako anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliyoachwa wazi na Haule. Kabla ya uhamisho huo, Nyambibo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment