Thursday, 3 February 2011

CUF: Hatuwezi kuwalamba miguu Chadema

 
Hussein Issa na Elizabeth Ernest
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema hakiwezi kuwalamba miguu viongozi wa Chadema, ili  wakubali kushirikiana nao.

Kauli hiyo, inafuatia baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kunukuliwa na vyombo vya habari juzi akisema hawawezi  kushirikiana na vyama vingine vya upinzani bungeni kwa kuwa vyama hivyo vimeungana na CUF ambayo 'imefunga ndoa' na CCM na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Dk Slaa alisema Kamati Kuu ya Chadema imeona kuwa chama hicho, hakiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo bungeni.

Kutokana na hali hiyo, alimuagiza kiongozi wa kambi ya upinzani kuunda baraza kivuli la mawaziri kwa kuwahusisha wabunge wa Chadema pekee.  Lakini jana, Kaimu Naibu Katibu Mkuu  wa CUF Bara, Julius Mtatiro alisema mbele ya wanahabari kuwa, chama chake hakiwezi kuilamba miguu Chadema ili ishirikiane nayo kwa kuwa haina faida yoyote kwa CUF.

"Tunapenda kuwataarifu Watanzania wote kuwa sisi (CUF), pia hatuwezi kuwalamba miguu viongozi wa Chadema kwani jitihada zetu za kuwaambia wafanye kazi na vyama vingine  tayari zimegonga ukuta," alisema Mtatiro.

Alisema mara nyingi Chadema imekuwa na historia ya kusaliti vyama vingine vya upinzani, kutokana na kuwa na uchu wa madaraka.  Alisema mwaka 2002 walifikia maamuzi ya kushirikiana  kwa vyama vinne vikiwemo Chadema, NCCR na TLP, lengo likiwa kuunga mkono chama chenye nguvu mahali panapofanyika uchaguzi, lakini Chadema ilikataa.

Alisema tofauti na matarajio ya malengo yao, katika uchaguzi wa marudio Jimbo la Tunduru NCCR na TLP walijitokeza kuisaidia CUF kwa kuwa huko ilikuwa ni ngome yake,  lakini Chadema walisimamisha mgombea wao na kumfanya mgombea wa CCM kushinda bila tatizo.  "Chadema walijifanya mapopo, wakasaliti makubaliano yaliyowekwa na vyama vingine, wakati hata tawi hawana kule Tunduru," alisema .

Alisema hali kama hiyo pia iliwahi kutokea katika majimbo ya Tarime, Busanda na Mbeya vijijini, ambako Chadema walikataa kutoa ushirikiano kwa vyama vingine kama walivyokubaliana na kuamua kusimamisha wagombea.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Chadema ndiyo inayotakiwa kuunda kambi ya upinzani bungeni, lakini CUF iliiomba Chadema ishirikiane  na vyama vingine vya upinzani ili kambi hiyo iwe imara zaidi na yenye nguvu, lakini Chadema walikataa suala hilo kwa maelezo kuwa wao hawako tayari kuungana na  CUF na vyama vingine ikiwa havitashirikiana na CUF.

"Jana Chadema wametoa kauli ya kinafiki eti wao hawawezi kushirikiana na chama kinachoongoza Dola yaani CUF,  na  kwamba wapo tayari kushirikiana na vyama vingine.

" Chadema ni chama popo sana, hawajui wanachokifanya, wamelewa  madaraka na kuchanganyikiwa vibaya baada ya kupata majimbo 20,"alisema Mtatiro.

 Aliifananisha Chadema kuwa ni sawa na mtu masikini sana kuamka ghafla akajikuta tajiri, hajui namna gani atatumia utajiri  wake na kuanza kuwatukana majirani zake alioishi nao kwa shida na raha katika umasikini wake.

Alisema kitendo cha Chadema kuwashambulia  CUF kwamba ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ni dhambi kubwa, kwani Wazanzibar walitaka kuungana na CCM.


"Chadema wamekuwa waoga mno, wanaiogopa CUF, wanajua CUF inamtandao mkubwa na mbinu ya kujiimarisha bara na hatimaye kuongoza nchi,"alisema Mtatiro.

No comments:

Post a Comment