Thursday, 27 January 2011

Serikali yajipanga kudhibiti kisukari



Serikali imezindua programu maalum inayolenga katika kushughulika na udhibiti wa ugonjwa wa kisukari nchini ambapo jumla ya Dola za kimarekani milioni 2.3 zinatarajia kutumika.
Akizindua programu hiyo jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Hussein Mponda, alisema programu hiyo itadumu kwa miaka minne na lengo lake ni kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa kwa asilimia kubwa.
Dk. Mponda alisema kati ya magonjwa yasiyoambukiza, kisukari ndio unaonekana kuwa wa kwanza kwa kuongeza idadi ya wagonjwa ambapo asilimia tano mpaka sita ya wagonjwa wa kisukari wanaishi mijini, na asilimia moja tu ni waishio vijijini.
Alizitaja baadhi ya sababu zinazochangia ni umaskini, matumizi mengi ya tumbaku, kutofanya mazoezi, matumizi mabovu ya chakula na matuimizi mengi ya kilevi.
Aidha alisema programu hii pia inalenga kutoa huduma kwa wagonjwa wanaougua ugonjwa huo katika Hospitali, Kliniki na katika kila Zahanati zilizoko nchi nzima.
Alisema kwa sasa Serikali imeboresha mfumo wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa kisukari, kwa kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapatiwa elimu mahsusi ya na namna ya kujijengea tabia ya kupima ugonjwa huo kila mara ili wale wanaobainika waweze kutibiwa mapema.
Aliongeza kuwa endapo wananchi watajenga tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara, idadi ya vifo vinavyotokana na uzembe wa kuchunguza afya vitapungua.

No comments:

Post a Comment