Thursday, 27 January 2011

Muungano kambi ya upinzani mashakani

*Mbowe awataka kina Hamadi Rashidi 'wazidi kusubiri'

Na Tumaini Makene

ZIKIWA zimebaki takribani wiki mbili kabla bunge la 10 halijaanza vikao vyake vya mkutano wa pili, hatma ya
vyama vyote vya upinzani kuwa na kambi moja rasmi bungeni, bado ni kizungumkuti, ikiwa vitaweza kuungana hivi karibuni kabla ya mkutano wa bunge ujao au hata baadaye.

Hayo yamefahamika ikiwa ni siku chache baada ya kamati ya wabunge wachache wa upinzani wasiokuwa katika kambi rasmi ya upinzani, kudai inasubiri majibu ya barua  waliyomwandikia Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe, wakiulizia uwezekano wa kuwa kitu kimoja kabla mkutano wa bunge haujaanza, Februari 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya wabunge hao wachache, Bw. Hamad Rashi Mohamed, 'kambi' yao inajumuisha Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi, United Democtratic Party (UDP) na Tanzania Labour Party (TLP).

Kwa sasa kambi rasmi ya upinzani bungeni inaundwa na Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya kutimiza masharti kama inavyoelekezwa katika Kanuni namba 14 (3) ya Kanuni za Bunge za mwaka 2007, inayosema kuwa ili chama cha upinzani kiweze kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni, lazima kiwe na asilimia 12 ya wabunge wote.  

Akizungumza na Majira jana juu ya hatma ya barua aliyoandikiwa, Bw. Mbowe alisema kuwa wabunge hao wanapaswa kuendelea kusubiri, kwani pande hizo zitaweza kuwasiliana kwa njia zilizo rasmi, si kupitia vyombo vya habari.

Alisema kuwa kwa sababu wabunge hao walimwandikia barua mkuu wa kambi rasmi bungeni kuulizia uwezekano wa vyama vyote kujumuishwa katika kambi hiyo, hawana haja ya kukimbilia kwenye vyombo ya habari, ilihali hawajui iwapo CHADEMA kimeshalijadili suala hilo katika vikao vyake au la.

"Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu suala hili si la Mbowe peke yake, suala hili lina process (taratibu) zake, wenzetu wasubiri majibu, sisi tutawasiliana nao kwa njia rasmi kama wao walivyotuandikia barua...hatuwezi kufanya maamuzi ya kisiasa kwa kupitia vyombo vya habari...la sivyo watu wanaweza kuwa wanatafuta cheap popularity.

"Hakukuwa na haja ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari, kama walinikosa mimi wangeweza kuwasiliana hata na naibu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni...lakini CHADEMA bado hakijafanya maamuzi, wala si rahisi kufanya maamuzi haraka haraka tu kwa sababu watu fulani au vyama fulani wanataka.

"Wakati mwingine si sahihi wala si vizuri kufanya maamuzi kwa pressure (shinikizo)...suala hili siwezi kusema no (hapana) wala yes (ndiyo) lakini halihitaji haraka namna hiyo," alisema Bw. Mbowe.  

Mwishoni mwa juma lililopita, wakati wakizungumza katika mkutano wao na waandishi wa habari, kupitia kwa viongozi wao, mwenyekiti wao Bw. Hamad (Wawi-CUF) na katibu wa kamati hiyo Bw. David Kafulila (Kigoma Kusini-NCCR Mageuzi), walisema kuwa hatma ya wao kuwemo katika kambi rasmi ya upinzani inategemea majibu kutoka CHADEMA.

"Tumemwandikia barua mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe...mnakumbuka kuwa katika mdahalo wangu na yeye, yaani mdahalo kati ya mkuu wa kambi rasmi ya upinzani katika bunge la 9 na mkuu wa kambi wa sasa katika bunge la 10, Mbowe alisema kuwa suala hilo linahitaji mchakato wa vikao vya chama, hawezi kuamua mwenyewe.

"Tunaamini kuwa tangu wakati wa mdahalo huo, ambao uliandaliwa makusudi kwa nia ya kujadili mstakabali wa upinzani bungeni kwa lengo la kuwa na kambi moja inayojumuisha vyama vyote kama ilivyokuwa katika bunge la 9 lililoisha, CHADEMA watakuwa wameshakaa vikao na kuamua juu ya suala hili.

"Hivyo tumemwandikia barua mkuu wa kambi rasmi ili tujue tunakwenda vipi katika bunge linalotarajiwa kuanza hivi karibuni...tujue kama tunakwenda tukiwa wamoja au tutakwenda kama tulivyo sasa," alisema Bw. Hamad.

Hata hivyo, jana Majira lilipata habari kutoka kwa mmoja wa wabunge wa upinzani, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, lakini akionesha dhahiri kuwa suala la vyama vyote vya upinzani kuunda kambi moja rasmi bungeni, bado ni ndoto ya alinacha.

"Unajua watu hawataki tu kusema au kuweka wazi mambo mengine, hii ndoa yetu ya wapinzani wote kuwa pamoja ni suala gumu na tata kwa kweli. Upende usipende ushirikiano wa CUF na CCM katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar ni moja ya vikwazo hapa, ni ngumu mno.

"CUF wanapaswa kukubali kuwa faida waliyoipata kukubali kushirikiana na CCM huko Zanzibar ndiyo gharama ya wao kukosa uhalali wa kuonekana kuwa ni wapinzani wa kuaminika huku bara...kwa mfano hivi anapewa....(anataja jina la mmoja wa wabunge wa CUF) uwaziri kivuli wa mambo ya ndani, hivi atakuwa mtiifu kwa nani, kwa Mbowe au kwa Makamu wa Rais wa Kwanza, ambaye pia ni katibu mkuu wake.

"Achilia huo mfano, chukua mfano mwingine...hivi kwa mfano tunaingia sasa katika umoja, halafu mmoja wetu anawasilisha hoja binafsi inayogusa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, mfano suala la mabadiliko ya katiba huko yalivyovuruga katiba ya muungano, hivi wabunge wa CUF watasimamia wapi," alisema mbunge huyo.

Alienda mbali na kutoa madai kuwa CUF kinaviburuza vyama vingine katika kile kinachoitwa kamati ya wabunge wachache wasiokuwa katika kambi rasmi, "wanaburuzwa tu kama msukule akina...(anataja jina la mbunge mwenzake wa upinzani kutoka NCCR-Mageuzi), lakini hamna kitu pale, hata UDP na TLP hawamo mle, basi tu," aliongeza mbunge huyo.

Lakini pia tumaini la kamati hiyo ya wabunge wa CUF, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, kuwa na kambi ndogo ya upinzani, limeonekana kutoweka baada ya Spika wa Bunge, Bi. Anna Makinda kunukuliwa na vyombo ya habari akisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za sasa za bunge, haiwezekani kuwa na kambi tatu bungeni.

Alisema kuwa CHADEMA walikuwa na sifa zote za kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa kuwa wana asilimia 12.5 ya wabunge wote, tofauti na vyama vingine vya upinzani, hivyo akavishauri vyama hivyo kuangalia uwezekano wa kuungana na CHADEMA.

Mabadiliko ya kanuni yalikuwa ni njia mojawapo ya kutaka kupata nafasi ya kutambulika, iwapo ile ya kuwaomba CHADEMA itashindikana "kwa kweli wakati tukibadilisha kanuni wakati ule tulijisahau kuangalia hili...si vizuri kabisa kukiacha nje ya kambi rasmi ya upinzani chama kingine cha upinzani chenye wabunge pia," alisema Bw. Hamad, huku akiungwa mkono na Bw. Kafulila katika mkutano wa mwishoni mwa juma.

Semina elekezi

Wakati huo huo, wabunge wa bunge la 10 wamekumbushwa kuwa wanao wajibu wa msingi katika maeneo manne, ambayo ni; katika majimbo yao ya uchaguzi, kwa nchi, kwa vyama vyao na kisha kwa dhamira zao wenyewe.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Dkt. Ghalib Bilal wakati akifungua semina elekezi kwa wabunge wote jana Dar es Salaam, akiongeza kwa kutoa wito kuwa wanapaswa kuwa karibu na wananchi waliowachagua ili kwa pamoja waweze kutafuta majawabu ya kero mbalimbali zinazowakabili.

"Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza mojawapo ya kazi yenu muhimu-uwakilishi wa wananchi. Miaka mitano kuanzia sasa si mingi," alisema Dkt. Bilal.

Spika na hoja binafsi za wabunge

Naye Spika wa Bunge, Bi. Anna Makinda jana alisema kuwa hatakuwa na tatizo kwa hoja binafsi yoyote itakayowasilishwa ofisini kwake almuradi iwe imekidhi vigezo vya kikanuni kuiwezesha kujadiliwa bungeni, baada ya kuangaliwa na wataalamu.

Alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) juu ya mgawo wa umeme na sakata la kampuni tata ya Dowans, ambapo alisema mpaka sasa mbunge huyo bado hajawasilisha hoja yake hiyo mbali na kuwa tayari ameshawasilisha barua ya kusudio la kuwasilisha hoja.

"Ni muhimu mkaelewa mpaka sasa alichowasilisha (Kafulila) ni barua ya kusudio la kuleta hoja binafsi, si hoja binafsi...hivyo ni vitu viwili tofauti kabisa...lakini sina tatizo na hoja yake au ya mbunge mwingine yeyote, kinachotakiwa ikidhi kanuni za bunge tu...akileta tutakaa na wataalamu tutaifanyia kazi, ikiwa haina tatizo tutamwambia ajiandae kuiwasilisha," alisema Bi. Makinda.

Habari zilizopatikana jana jioni katika eneo la semina elekezi ya wabunge na kuthibitishwa na Bw. Kafulila, zilisema kuwa ofisi ya bunge imejibu barua ya mbunge huyo, ikimtaka awasilishe hoja yake ofisi za bunge, tayari kwa kufanyiwa kazi.

"Ndiyo nimepata barua hiyo, lakini ni ya siri, siwezi kukuonesha...lakini jibu la lini nitawasilisha hoja yangu ofisi ya spika siwezi kulisema sasa, labda kesho nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema," alisema Bw. Kafulila.

No comments:

Post a Comment