Moto wa Katiba wasambaa
Na Romana Mallya
Msekwa aungana na wananchiAsema Tanzania inahitaji Katiba inayoenda na wakati uliopo
Asema atawaeleza viongozi wa CCM wasome alama za nyakati
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Pius Msekwa
Mjadala wa kuandikwa kwa Katiba mpya umeendelea kushika kasi hapa nchini baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Pius Msekwa, kuunga mkono hoja ya kufanya badiliko hilo ili kukidhi mahitaji ya wakati uliopo.
Msekwa ambaye amekuwa Spika wa Bunge kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 1995, amesema licha ya kuunga mkono hilo, atawaeleza viongozi wenzake wa CCM wasome alama za nyakati na kukubaliana na hoja ya katiba mpya.
Msekwa aliitoa kauli hiyo juzi usiku jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa katiba uliohusisha wabunge wa vyama mbalimbali, viongozi wa vyama vya siasa, wasomi na waandishi wa habari.
Mdahalo huo uliandaliwa kwa pamoja na East African Business and media Training institute, Vox Media, ITV na Channel five (EATV).
Katika mdahalo huo ambao ulichukua takribani saa mbili, Msekwa alijikuta akikubaliana na wazo hilo la kuundwa kwa katiba mpya baada ya kubanwa vikali na washiriki wengi waliokuwa wakitaka katiba mpya.
Washiriki hao walimbana vikali Msekwa kwa maswali na hoja mbalimbali wakitaka aeleze bayana kuwa katiba ya sasa inatakiwa kubadilishwa na sio kuwekewa viraka.
Upepo wa mdahalo ulibadilika baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alipoingilia kati na kumkingia kifua Msekwa kuwa aeleze mapungufu na atumie uzoefu wake wa masuala ya katiba ili kuelimisha wajumbe.
Msekwa alikubaliana na hoja hiyo na kuanza kueleza, “Binafsi naunga mkono mabadiliko ya Katiba na ninaahidi kuwaeleza viongozi wenzangu wa CCM wasome alama za nyakati na kukubaliana na hoja ya katiba mpya,” alisema.
Pia washiriki hao walieleza wasiwasi na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba, kitu ambacho Msekwa alikitetea na kudai hakuna haja ya wananchi kuwa na wasiwasi na dhamira ya Rais.
Msekwa alisema kuwa wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi na Rais Kikwete na CCM kuhusiana na dhamira ya kuunda katiba, kwani historia inaonyesha hata huko nyuma zimewahi kuundwa tume za chini ikiwemo ile ya Jaji Francis Nyalali na ya Jaji Robert Kisanga.
Akitetea hoja yake ya kuwepo kwa katiba mpya, Msekwa alisema kuna haja ya kuingiza vipengele vya mabadiliko ya katiba ya Zanzibar, ambayo kwa sasa ina Makamu wawili wa Rais kutokana na serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwepo huko.
“Sababu nyingine nayoweza kusema ni kwamba katiba mpya ni muhimu kuwepo ili iendane na wakati, Katiba tuliyonayo inaeleza Tanzania inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea wakati kipindi hiki kuna mfumo wa vyama vingi na kila chama kina sera yake,” alisema.
Katika hatua nyingine, Msekwa ambaye alikuwa na wakati mgumu kutokana na CCM kulaumiwa kwa matatizo mengi ya katiba ya sasa na washiriki wa mdahalo kiasi cha mwongozaji wa mdahalo huo, Rose Mwakitwange, kutuliza munkari wa washiriki, alitetea kuwa katiba ya sasa haikuwa na matatizo bali utekelezaji wake.
Alitolea mfano kuwa kuna Sekretarieti ya Maadili, ambayo imeanishwa kwenye katiba na ndio yenye dhamana ya kushughulikia viongozi waovu.
“Unajua tunapaswa kuacha kulaumu katiba tu…sio kila tatizo linasababishwa na katiba pia kuna udhaifu wa utekelezaji,” alisema Msekwa na kuungwa mkono na baadhi ya washiriki ambao walitaka taifa litengeneze mfumo wa kudhibiti maadili ya viongozi.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, (NCCR- Mageuzi), aliipinga kauli ya Msekwa kuwa katiba ya sasa haina matatizo na kueleza kuwa katiba ya sasa ni dhaifu na kwamba ipo haja ya kuundwa mpya itakayoweka bayana maovu ya sasa ya viongozi.
Msekwa, ambaye alitumia mdahalo huo kuelemisha wajumbe wa katiba yenyewe, hata hivyo, alitaka suala la katiba lishirikishe wananchi wote, ambao wanapaswa kuelimishwa kuhusu katiba yenyewe na sio kuachia wanasiasa peke yao.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alisema CCM kinapaswa kuelewa kuwa suala la Katiba halikwepeki wala kuzuilika na kwamba ni hitaji la wananchi kwa sasa.
Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, alisema Katiba mpya ni lazima kwa sababu wananchi wanadai Tanzania mpya.
Alipendekeza kwamba Tume iliyokusudiwa kutungwa na Rais Kikwete ipitishwe na Bunge ili mapendekezo yake yote yatekelezwe isijeikatokea kama tume zilizopita.
Akifunga mdahalo huo, Msekwa alisema “Niwaambie tu kwamba nilichokipata hapa inatakiwa Katiba mpya inayofanana na Tanzania ya leo na pia mchakato wake uwe wa uwazi usio na mashaka mashaka,” alisema
Aliwataka wananchi kuainisha mapungufu yote yaliyopo kwenye Katiba ya sasa. “Naomba nitoke hapa na yale yote tuliyoyatoa…nitayafikisha kwa wenzangu kwa sababu sina maamuzi”, alisisitiza.
No comments:
Post a Comment