Monday, 3 January 2011

Meya wa Chadema` Arusha ajiuzulu

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema


 Na Asraji Mvungi

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Sakata la uchaguzi wa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha linalodaiwa kuongozwa na Mameya wawili mmoja kutoka Chama Cha Mapinduzi CCM na mwingine kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limeingia katika sura mpya, baada ya aliyejitangazwa kuwa meya kupitia Chadema kutangaza kuachia ngazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Eestomih Mala, alisema baada ya kutafakari, wamegundua kuwa kitendo cha kuchagua Meya wao ni kuendelea kufanya makosa na kukiuka sheria.
Mala ambaye ni Diwani wa Kimandolu, alisema baada ya kukaa na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, wameona hakuna sababu ya kufanya hivyo kwani wanachojua wao ni kwamba nafasi ya Meya wa Jiji hilo bado iko wazi kwani kikao kilichomchagua Meya ni batili.
Alisema hawataenda mahakamani kwani wamebaini kuwa wakifanya hivyo watakuwa wamejimaliza.
“Uzoefu unaonyesha kuwa kukimbilia mahakamani sio tija kwani kesi inaweza kupigwa danadana hata zaidi ya miaka mitano. Sisi bado tuna hatua nyingi tunazoweza kuzichukua kudai haki yetu, hatuna wasiwasi kwani tunaamini kuwa tunatetea haki ya wananchi walio wengi,” alisema Mala.
Kuhusu msimamo wao wa kumtambua ama kutomtambua Meya aliyechaguliwa, alisema sio tu kuwa hawamtambu Meya huyo, Gaudence Lymo, bali hawautambui hata mkutano wa Baraza la Madiwani uliomchagua kwani ulikuwa wa upande wa chama kimoja cha CCM.
Aidha, Mala alikanusha vikali madai ya msimamizi wa uchaguzi wanaodai kuwa ni batili kuwa walishiriki katika uchaguzi huo na kutoa ufafanuzi kuwa walichoshiriki ni kula kiapo cha madiwani na sio vinginevo.
“Wanadai kuwa eti tulishiriki kumchagua huyo Meya, lakini tunapenda wananchi waelewe kuwa sisi hatutashiriki kwenye uchaguzi huo na tulichoshiriki sisi ni kikao cha kuapishwa kwa madiwani, huo uchaguzi wa Meya sisi hatukushiriki,”alisema Mala.
Alisisitiza kuwa pamoja na hujuma walizofanyiwa harakati zao za kutafuta haki zinaendelea ikiwemo ya kufanya maandamano yanayotarajiwa kufanyika keshokutwa yenye lengo la kuudhihirishia umma msimamo wao na jinsi wasivyoridhishwa na mambo mbalimbali wanayofanyiwa.
Aliwataka wananchi wa Jiji la Arusha kuwa watulivu na kutambua kuwa chama chao hakina mpango wa kuchagua Meya kama ilivyokuwa imeripotiwa awali na kwamba kinachofanyika sasa ni kuendelea kupigania haki kwa kutumia njia nyingine.
Tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa kisiasa katika jimbo la Arusha, kumekuwa na hekaheka za hapa na pale na hali ya kisiasa katika jiji hilo haijawa shwari hadi sasa.

No comments:

Post a Comment