Monday, 31 January 2011

Hali ya wasiwasi yatanda Misri




CAIRO,Misri

HALI ya wasiwasi imezidi kutanda nchini Misri baada ya jeshi la nchi hiyo kuamua kuingilia kati mgogoro wa kisiasa unaondelea nchini humo.Habari kutoka nchini humo zimeleeza kuwa wasiwasi huo umeongezeka zaidi baada ya ndege mbili za kivita na helikopta ya kijeshi kuranda katika anga ya  eneo wazi la Tahrir, mahala ambapo waandamanaji wengi wamekusanyika.

Mbali na ndege hizo imeelezwa kwamba  msururu wa vifaru uliwasili katika eneo hilo, lakini ukazuiwa na waandamanaji.

Mwandishi wa wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC Jeremy Bowen aliyepo kwenye eneo la Tahrir amesema  kwamba kuna hali ya kutojali baina ya waandamanaji, ambao wanalituhumu jeshi kwa kujaribu kuwatisha.

Kuwasili kwa msururu wa vifaru na milio ya ndege za kivita angani kunadaiwa kumezusha hali ya wasiwasi miongoni mwa maelfu ya waandamanaji.

Imeelezwa kuwa licha ya kuwepo kwa magari ya kijeshi, waandamanaji walionekana kama wakiwa na uhuru wakuranda katika eneo la katikati ya  jiji, huku askari wa kuzuia ghasia ambao wamekuwa wakipambana na waandamanaji wakiwa hawaonekani.


Mapigano kati ya waandamanaji na vyombo vya dola, hasa polisi wa kuzuia ghasia, yanadaiwa kusababisha vifo vya watu wasiopungua 100  tangu kuanza kwa harakati hizo Jumanne wiki iliyopita huku maelfu ya watu wakijeruhiwa baada ya ghasia kuzuka na kufika hadi katika miji ya Cairo, Suez na Alexandria.

Wakati huohuo, matangazo ya shirika la habari la al-Jazeera kupitia mitambo ya satelaiti ya Misri yamesitishwa.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mapema jana kuamrisha shirika hilo la Kiarabu ambalo limekuwa likitangaza maandamano hayo, kufunga shughuli zake nchini humo.

Katika hatua nyingine,Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton ametoa wito wa kuwepo na "mabadiliko ya utawala yenye utaratibu" nchini Misri.

Mama Clinton ameliambia shirika la habari la ABC kuwa Marekani inataka kuona mabadiliko ambayo yataleta serikali ya kidemokrasia.

"Tunataka kuona uhuru, hatutaki kuona ghasia zinazofanywa na vyombo vya usalama," amesema Clinton.

No comments:

Post a Comment