Saturday, 1 January 2011

Chadema yatwaa umeya Kigoma Ujiji


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika


Hatimaye kitendawili cha meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma, kimeteguliwa jana, baada ya Diwani wa Kata ya Rusimbi Ujiji (Chadema), Beji Bakari, kuchaguliwa kuwa Meya mpya wa Manispaa hiyo.
Beji alichaguliwa kushika wadhifa huo baada ya kupata kura 15 dhidi ya kura 12 alizopata mpinzani wake, John Mutabiirwa (CCM) katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa manispaa hiyo jana. Kura moja iliharibika.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya Kibirizi (Chadema), Yunus Luhovya, alichaguliwa kuwa Naibu Meya wa manispaa hiyo baada ya kupata kura 15 dhidi ya kura 13 alizopata Salum Akilimali (CCM).
Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Desemba 17 mwaka jana, lakini ukaahirishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika baada ya CCM kukata rufaa kupinga mgawanyo wa madiwani kwa kutaka iongezewe diwani mmoja au Chadema ipunguziwe diwani mmoja, jambo ambalo halikufanyika.
Akiwashukuru madiwani kwa kumchagua, Beji aliwataka kuondoa tofauti zao za kiitikadi, badala yake waungane na kufanya kazi kama timu ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya Kigoma, Johh Mongela, aliwataka madiwani wote kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utendaji wa madiwani badala ya kuweka mbele maslahi ya vyama vyao.
CHANZO: NIPASHE    

No comments:

Post a Comment