Sunday, 13 October 2013

                 
Raza: Zanzibar bado inayo fursa kuwa huru kiuchumi



Mohamed Raza Mwakilishi wa Uzini,  akizungumza na Waandishi wa Habari, kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu Zanzibar katika ukumbi wa Grand Palace Hotel Malindi Mjini Zanzibar
Mohamed Raza Mwakilishi wa Uzini, akizungumza na Waandishi wa Habari, kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu Zanzibar katika ukumbi wa Grand Palace Hotel Malindi Mjini Zanzibar
 
 
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliofika kumsikiliza Mohamed Raza alipokuwa akizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu Zanzibar katika ukumbi wa Grand Palace Hotel Malindi Mjini Zanzibar
 
Wazanzibari wameombwa kuendelea kuungana katika kupigani maslahi ya Zanzibar katika Muungano, na kwamba Zanzibar bado inayo nafasi ya kuwa huru kiuchumi kupitia mchakato wa Katiba Mpya.
Wito huo umetolewa na Mwananchi mzalendo, Mohamedraza Hassan Dharamsi alipokuwa akizungumza na Wanahabari kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu Zanzibar katika mkutano alioufanya Hoteli ya Grand Palace Forodhani mjini Zanzibar.
Amesema yeye anaamini katika Muungano na sio Utengano na kudai kuwa kama Muundo wa Serikali mbili umeshindikana ni vyema ukawepo Mfumo mpya wa Muundo wa Serikali tatu.
Ameongeza kuwa kinachotakiwa na Wazanzibari walio wengi ni kuona nchi yao ya Zanzibar inakuwa huru kujiamulia mambo yake ya Kiuchumi bila kuitegemea Tanganyika. “Sisi tupo huru lakini hatupo huru kiuchumi tunataka Zanzibar ijiamulie mambo yake yote yanayohusu uchumi, kuwa na Bendera haitoshi kuwa huru Uchumi ndio uhuru” Aliongeza Raza.
Kuhusu Mchakato wa Katiba mpya unavyoendelea, Raza amemshauri Rais Shein kuwaita Wasaidizi wake Makamu wa Kwanza Maalim Seif na Makamu wa Pili Balozi Seif kushauriana na kuwa na Kauli moja juu ya hatma ya Zanzibar. “Mi namuomba Rais wangu Dkt. Shein akutane na Maalim Seif na Balozi Seif wajifungie Chumbani wajadiliane vyakutosha kisha tupate pakusimamia sio kila mtu kusema vyake kuhusu Katiba Mpya”
Akizungumzia kuhusu Kisiwa cha Fungu Mbaraka, amesema Kisiwa hicho ni mali ya Zanzibar kama maelezo yalivyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar  na kwamba asilani Tanganyika haina uwezo wa kukihodhi kisiwa hicho. “Ndugu zangu waandishi ushahidi upo wa kutosha kuwa Fungu Mbaraka ni Mali ya Zanzibar lakini kwa vile kisiwa hicho kipo kwenye kitalu namba nane cha Mafuta ndugu zetu Wabara wanadai ni Kisiwa chao, hii haikubaliki maisha” alisisitiza Raza.
Amesema inashnagaza kila Zanzibar inavyotaka kujikwamua kiuchumi baadhi ya viongozi wa Tanganyika wamekuwa wakiweka pingamizi jambo ambalo si jema kwa mustakabali wa Muungano na Taifa kiujula.
Ameongeza kuwa hivi karibuni kuna Kiongozi alidai Rais Shien kavunja Sheria kwa kusaini Mkataba wa Kuchimba Mafuta, na kuongeza kuwa kiongozi huyo alipaswa kumuomba Radhi Rais Shein. “Huyu alipaswa kumuomba Radhi Rais Shein,kwani wao wamevunja Sheria mara ngapi? Leo kusaini Mafuta jambo ambalo limekubaliwa ndio imekuwa tatizo” alihoji Raza ambaye pia ni Mwakilishi wa Uzini.
Raza ameongeza kuwa ataendelea kupigania Maslahi ya Zanzibar bila kuogopa Vitisho  vyovyote kwa kufuata misingi ya Katiba na Sheria za nchi.
Kuhusu tozo ya kodi ya simu, amesema kodi ni jambo la msingi kwa maendeleo ya nchi lakini kodi hiyo inapaswa iinufaishe Zanzibar na siyo Tanzania bara.
Mohammed Raza ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini aliweka wazi kuwa aliyoyasema ni maoni yake binafsi kama Mwananchi na siyo mawazo ya Mwakilishi wa Uzini.

No comments:

Post a Comment