Wednesday, 18 September 2013

TAMKO LA WIZARA YA MAMBO YANJE JUUYABALOZI WA CHINA KUSHIRIKI SHUGHULI ZA NDANI YA NCHI





                                               TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefuatilia taarifa kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini, kuhusu kushiriki kwa Mheshimiwa Lu Younqing Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika huko Shinyanga, mwishoni mwa juma lililopita.

Taarifa hizo zimeambatana na picha zinazomuonyesha Mheshimiwa Lu akiwa amevaa kofia yenye nembo ya CCM. Habari zinaeleza kuwa Balozi alikwenda Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vita kuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.

Wizara inatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vilevile inatambua kazi nzuri ambayo Balozi Lu Younqing amekuwa akifanya toka alipowasili nchini Tanzania. Kutokana na tukio hili, Wizara inapenda kuelekeza  kwamba kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa sio sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia.  Mkataba huo wa Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi. Aidha, Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986 ambayo ni zao la Mkataba wa Vienna pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi.

Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki.  Na kwa tukio hili pia Wizara  imechukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena.



                                                              IMETOLEWA NA:

                        WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

                                                        18 Septemba, 2013

                                                         Dar Es Salaam.
 
 Balozi wa China akisisitiza jambo huku Balozi Kairuki akimsikiliza kwa makini.
 
 
 Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mbelwa Kairuki (kulia) akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youqing kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na China.
 
 
 Katibu Mkuu wa CCM, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana (kushoto) akimtambulisha Balozi wa China nchini, Lu Younqing kwenye moja ya mikutano ya chama hicho mkoani Shinyanga wiki iliyopita. 

 
Balozi wa China nchini, Lu Younqing akihutubia kwenye moja ya mikutano ya ccm mkoani Shinyanga wiki iliyopita.  

No comments:

Post a Comment