MUSWADA WA KUPAMBANA NA MADAWA YA KULEVYA
Habari kwamba Serikali inaandaa Muswada
wa aina yake wa Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini hakika ni za kutia
moyo. Tunasema zinatia moyo kutokana na Muswada huo kupendekeza uundwaji wa
taasisi itakayopewa meno na madaraka kamili kupambana na biashara ya madawa
hayo. Kama sote tunavyofahamu, biashara hiyo ya dawa za kulevya imepanuka kwa
kasi ya kutisha na kuharibu maisha ya vijana wengi, mbali na kuchafua jina na
taswira nzuri ya taifa letu mbele ya jumuiya ya
kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania
imekuwa kichekesho cha dunia kutokana na Watanzania wengi kukamatwa kila kona ya
dunia wakisafirisha dawa hizo. Ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana
na Mihadarati na Uhalifu (UNODC), imesema Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa
za kulevya katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Takwimu zinaonyesha kwamba maelfu ya
Watanzania wanashikiliwa katika magereza katika nchi nyingi duniani na wengine
wengi wamenyongwa baada ya kutiwa hatiani na mahakama za nchi ambazo hazina
chembe ya uvumilivu wa biashara hiyo, ikiwamo China.
Ni vigumu kujua jinsi Tanzania
iliyokuwa ikiheshimika sana duniani imebadilika ghafla na kuwa kinara wa dawa za
kulevya. Haipiti siku bila kutangazwa habari za Watanzania kukamatwa wakiwa na
shehena kubwa za dawa hizo katika sehemu mbalimbali
duniani.
Jambo la kushangaza ni kwamba
wanaokamatwa ni vijana wanaopewa dawa hizo na wafanyabiashara wakubwa ili
kuzisafirisha, huku wafanyabiashara hao wakiendelea kutesa
mitaani.
Pamoja na kusema kwa muda mrefu kwamba
inayo majina ya ‘magwiji wa unga’, wakiwamo baadhi ya wafanyabiashara na
wabunge, Serikali bado imeshikwa na kigugumizi kuwataja hadharani au kuwafikisha
mbele ya sheria. Ndiyo maana tunasema hatua ya Serikali ya kuandaa Muswada huo
wa aina yake ili kuunda chombo chenye meno ya kupambana na biashara hiyo hakika
ni ya kupongeza.
Ni hatua ya kupongeza kwa sababu
Serikali sasa inaonyesha utashi na dhamira ya kupambana na biashara hiyo. Ni
kweli hatua hiyo imekuja ikiwa imechelewa sana kiasi cha tatizo hilo kuonekana
kuizidi kimo, lakini tunaamini muundo, madaraka na meno kitakachopewa chombo
hicho vitatosha kuiangamiza biashara hiyo haramu iwapo watateuliwa watendaji
wenye uadilifu kukiongoza.
Ni habari njema kwamba Muswada
unaotayarishwa unapendekeza chombo hicho kiwe huru, mbali na kuwa na vitengo
vyake vyenye madaraka ya kufanya uchunguzi, kukamata watuhumiwa na kuwafungulia
mashtaka bila kutegemea Jeshi la Polisi nchini. Chombo hicho kitakuwa na makazi
ya pamoja na Mahakama Maalumu itakayoundwa kuendesha kesi hizo ambazo zitachukua
muda mfupi kabla ya hukumu kutolewa. Hivi sasa kesi hizo zinachukua zaidi ya
miaka 10 kumalizika.
Muswada huo unataka watakaopatikana na
makosa wasiwe tena na uhuru wa kulipa faini. Mahakama nazo hazitaruhusiwa kutoa
dhamana kwa watuhumiwa na dawa zitakazopelekwa mahakamani kama ushahidi
zitaharibiwa mara moja, kinyume na sasa ambapo ushahidi huo unatunzwa kwa muda
mrefu. Uzoefu umeonyesha kwamba dawa hizo hupotea au huchakachuliwa katika
mazingira ya kutatanisha.
Tuna kila sababu ya kuwa na matumaini
kwamba sasa kiyama cha wauza ‘unga’ kimewadia. Tunaipongeza Serikali kwa kuweka
mbele masilahi ya taifa kwa kuandaa Muswada usio na simile katika kupambana
biashara hiyo haramu na hatari
No comments:
Post a Comment