Sunday, 29 September 2013

Katiba ni Mwafaka wa Kitaifa, Viongozi zungumzeni


ZITTOKABWE
 
Na Mhe. Zitto Kabwe
Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya sheria ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011.
Mjadala na upitishaji wa sheria hii uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu kwa vitendo vya kihuni kutokea Bungeni ambavyo nisingependa kuvirejea kutokana na aibu kubwa ambayo Bunge liliingia.
Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya. Hii imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo.
Masuala ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa na kuzungumza.
Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa.
Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi.
Kuna kundi lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata Katiba bora.
Kuna kundi la Wabunge ambao kwa chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge. Naamini watu hawa wanaota ndoto za mchana kwani hakuna mahusiano yeyote kati ya uchaguzi mkuu na kuandika katiba mpya.
Kama Bunge hili la sasa na Serikali hii itashindwa kukamilisha zoezi hili, Bunge linalokuja na Serikali itakayoingia madarakani itaendelea nalo.
Hivyo sio lazima kupata Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. CHADEMA imependekeza kuwepo na marekebisho ya mpito kwenye Katiba ya sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea binafsi na kadhalika. Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.
Changamoto kubwa sana ya siasa za Tanzania ni kelele. Wanasiasa hatuzungumzi kwenye masuala yanayohusu uhai wa Taifa. Kila chama kinakuwa na misimamo yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya kuzungumza na kujadiliana kama Watanzania. Mwaka 2011 hali ilikuwa hivi hivi mpaka kundi la Wazee viongozi wastaafu walipoingilia kati na kupelekea wanasiasa kukaa na kuzungumza.
Bahati mbaya sana viongozi wale ndio sasa wamepewa usukani wa kuandika Katiba kwa kuwa kwenye Tume. Hawawezi tena kufanya kazi ile ya kutafuta suluhu iliyopelekea Rais kuzungumza na viongozi wa vyama vyote vya siasa ikulu jijini Dar es Salaam.
Vyama vya Upinzani nchini sasa vimeungana kupinga muswada wa marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na Uratibu, viongozi waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo.
Badala ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno ya kejeli na kadhalika. Taifa halijengwi namna hii. Taifa linajengwa kwa mwafaka na Katiba ni moja ya nyenzo wa Mwafaka wa Taifa. Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Katiba haiandikwi barabarani bali huandikwa mezani kwa watu kukaa na kukubaliana masuala ya Taifa dhidi ya maslahi ya kivyama ya wanasiasa.
Hakuna kilichoharibika. Bado tunayo nafasi kama Taifa kukaa na kukubaliana. Kwa hali ya sasa nafasi hii ipo mikononi mwa Mkuu wa Nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba ya nchi yetu. Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama kutoridhia sheria hiyo.
Si sawa kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi na pia kinatafsirika kama kumshurutisha (blackmail) Rais wake.
Kutosaini muswada huu kunaweza kuleta mgongano kati ya Wabunge wa CCM na Rais. Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama chake kwamba umoja wa kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya chama chao. Pia kikatiba Rais anasaini miswada kuwa sheria akiwa Mkuu wa Nchi na sio Mkuu wa Serikali ya Jamhuri. Akiwa Mkuu wa Nchi maslahi mapana ni kuweka mwafaka wa pamoja miongoni mwa wananchi. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutumia mamlaka yake kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni ili uweze kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge. Ibara ya 97 ya Katiba ya sasa imeweka masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais ataurudisha muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji wake utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote. Hii itakuwa hatua muhimu sana katika historia ya demokrasia yetu. Rais afuate ushauri huu kwani una manufaa makubwa.
Hata hivyo, ni lazima pawepo na mazungumzo miongoni mwa wanasiasa na makundi ya kijamii kuhusu Katiba. Katiba nzuri itapatikana pale tu ambapo mazingira ya kisiasa yanaonyesha nia njema kwa pande zote kisiasa. Kukwepa kuangaliana machoni na kuzungumza tofauti zetu za kimitazamo ni hatari zaidi. Juzi ngumi zimerushwa Bungeni. Kesho zitakua mitaani na vijijini kwetu. Tunataka kujenga Taifa la namna hiyo?

No comments:

Post a Comment