Monday, 30 September 2013

JK arejea nyumbani kutoka Canada na Marekani




Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 30, 2013 wakitokea Marekani katika ziara ya kikazi.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Jordan Rugimbana na nyuma yao wa pili kushoto ni Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam Afande Suleiman Kova



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda huku Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilali akiangalia wakati alipowasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 30, 2013 akitokea Marekani na Canada katika ziara ya kikazi.



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Mbunge wa Rombo (CHADEMA) Mhe Joseph Selasini wakati alipowasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 30, 2013 akitokea Marekani katika ziara ya kikazi. Wanaofuatia ni Mbunge wa Nkenge (CCM) Mhe. Asumpta Mshama na Mbunge wa Wawi (CUF) Mhe Hamad Rashid Mohamed.



Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakilakiwa na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Septemba 30, 2013 wakitokea Marekani katika ziara ya kikazi. PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amerejea
nchini mchana wa leo, Jumatatu, Septemba , 2013, baada ya ziara ya kikazi yenye
mafanikio makubwa katika Marekani na Canada.

Miongoni mwa shughuli nyingine nyingi katika ziara hiyo, Rais Kikwete alihutubia Kikao
cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.

Rais Kikwete ambaye aliondoka nchini Jumapili ya Septemba 15 alianzia safari yake
mjini San Francisco, Marekani, ambako miongoni mwa mambo mengine alizindua
Ubalozi Mdogo wa Tanzania katika Jimbo la California.

Rais pia alikutana na kuzungumza na Jumuia ya Watanzania katika Jimbo hilo na
kukaribishwa katika Jiji la Vallejo katika sherehe za miaka 20 za uhusiano wa
kimji kati ya Jiji hilo na mji wa Bagamoyo.

Ziara ya Rais Kikwete San Francisco ilifuatiwa na ziara ya mjini Washington ambako shughuli
zake kubwa zilikuwa kukutana na viongozi wa Bunge la Marekani na pia kuhudhuria
Hafla ya Chakula cha Usiku cha Taasisi ya Kulinda Hifadhi na Mazingira ya Bunge
la Marekani (ICCF) ambako alitunukiwa
tuzo maalum za Mtunzaji Mazingira Bora wa Mwaka.

Aidha,Rais Kikwete alishuhudia utiaji wa saini mikataba ya kufungua Ofisi Ndogo za
Ubalozi wa Tanzania katika majimbo mbali mbali ya Marekani.

Baada ya hapo, Rais Kikwete alikwenda Canada ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya
Udaktari wa Sheria na Chuo maarufu na kikongwe cha Canada cha Guelph ambacho ni
maarufu duniani kwa shughuli na utafiti wa kilimo.

Kufuatia ziara hiyo ya Canada, Rais Kikwete alikwenda New York ambako alikuwa na shughuli
nyingi ikiwa ni pamoja na kuhutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la UN Ijumaa ya wiki iliyopita, akakutana na Katibu Mkuu wa UN Mheshimiwa Ban
Ki Moon, akashiriki kikao maalum cha wakuu wa nchi kujadili hali ya Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
kilichoitishwa na Mheshimiwa Ban Ki Moon.

Akiwa mjini New York, Rais Kikwete pia alikuwa kiongozi pekee wa Afrika aliyealikwa
kushiriki katika Mkutano wa Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama na taasisi
zisizokuwa za kiserikali duniani na pia alihudhuria Halfa Maalum iliyoandaliwa
na Rais Obama alipomaliza kuhutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la UN.

Aidha, Rais Kikwete alishiriki Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Clinton Global Initiative na pia akawa mzungumzaji rasmi katika
Mkutano wa Kupambana na Ujangili Duniani uliotishwa na Rais Ali Omar Bongo
Ondemba wa Gabon.

                                                          Imetolewa na:

                                              Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

                                                                    Ikulu,

                                                       DAR ES SALAAM.


                                                         30 Septemba, 2013

No comments:

Post a Comment