Sunday, 15 September 2013

Dk. Mwakyembe aicharukia TPA

na Shehe Semtawa
 
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametoa siku moja kwa uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuwataja watu wanaojihusisha na hujuma za wizi wa mafuta kwenye bomba kubwa la TPA.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wafanyakazi wa TPA kuhusu changamoto na mafanikio ya utendaji kazi wao.
Dk. Mwakyembe alisema anaamini kuwa watu hao wanafahamika kwa kuwa si rahisi hujuma kama hiyo kufanywa na mtu asiyekuwa mtaalamu wa sekta hiyo.
Dk. Mwakyembe alisema wezi hao bila hofu wamejaribu kulitoboa bomba hilo kubwa ambalo limeigharimu serikali mamilioni ya shilingi na kuunganisha mabomba yao chini kwa chini kisha kunyonya mafuta hayo hadi kwenye stesheni zao za kuhifadhia mafuta.
Alisema kuwa wezi hao wamekuwa wakiibia serikali lita 35,000 hadi 40,000 katika kipindi kisichojulikana kitendo ambacho ni sawa na uhujumu uchumi.
“Tiper ndio vinara wa wizi huo hivyo naagiza kuvunja mkataba, pia muwalete ili waje wawataje waliohusika na wizi huo, kwani umefanywa kitaalamu pia nasikia kuna Mzungu ambaye amezoea kutoa rushwa lakini kwa hili naamini watarudi kwao Ulaya,” alisema na kuongeza kuwa:
“Baada ya wizi kupungua kwenye Mamlaka hiyo Bandari nawapongeza sana lakini wapo watu ambao si waaminifu, wamebuni mbinu mpya za kuihujumu serikali kwa kutumia mbinu nyingine,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema kuwa alimfahamisha Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo juu ya hujuma hiyo inayofanywa na kampuni hiyo ya Tiper, kitendo ambacho kilimsononesha.
Alisema suala hilo linagusa masilahi ya nchi, hivyo wameamua kulifanyia kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini ili kuhakikisha kila aliyehusika anachukuliwa hatua zinazostahili, lengo likiwa ni kukomesha vitendo kama hivyo visiweze kujirudia tena.
Dk. Mwakyembe alisema serikali haitakaa kimya kwa kuwa kitendo kilichofanyika ni hujuma ambayo ingeweza kuangusha uchumi wa nchi na kuzorotesha huduma za jamii, hivyo ni lazima wahusika washughulikiwe.
Aidha, Dk. Mwakyembe ameutaka uongozi wa TPA kuacha mara moja mpango wake wa mara kwa mara wa kupeleka boti na mitambo mingine kwenye karakana zilizoko Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya matengenezo, mpango aliouita kuwa ni wa kujitengezea ulaji kwa watu wachache.
Aliiagiza TPA kuwa lazima ijipange kwa kuandaa bajeti ambayo itawasaidia kujenga karakana yake na si kujenga mazingira ya ulaji wa fedha za serikali kinyume cha utaratibu, kama ikitokea hivyo ni lazima wizara ipewe taarifa na si vinginevyo.
Akizungumzia Bodi ya TPA, alisema bodi hiyo ina ufa na yote hayo yanachangiwa na watu kugombea ulaji, kitendo ambacho kinawakatisha tamaa wafanyakazi ambao wanaonesha juhudi kubwa katika kuchapa kazi.
Kuhusu wafanyakazi
Dk. Mwakyembe aliutaka uongozi wa TPA kuhakikisha kuwa unasimamia haki za wafanyakazi wote bila kubagua na pindi ikitokea kiongozi kumuonea mfanyakazi wa chini atamshughulikia bila kujali cheo chake.
Kituko
Kwenye kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, alianguka chini wakati akielekea kukaa kwenye kiti, na kufanya aondolewe kwenye jukwaa kwa muda kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.
Aliporudi jukwaani alikuwa akichechemea, hali iliyomfanya aombewe na waziri kuwa asome taarifa huku akiwa amekaa, kutokana na maumivu aliyopata baada ya ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment