ALISIMAMA kutoa hoja, hakupewa fursa; akaambiwa akae chini. Hakukaa. Akaambiwa atoke nje; hakutoka. Wakaitwa askari kumtoa kwa nguvu, ukazuka mzozo uliozaa masumbwi bungeni.
Ni kauli gani ambayo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitaka kutoa?
Vyanzo vyetu vya habari vilivyo karibu na Mbowe vilimnukuu jana akisema alichotaka kusema, akazuiwa na Naibu Spika, Job Ndugai, ni hiki hapa:
“Kwanza, nilichotaka kusema ni kutoa hoja ya kuomba shughuli za Bunge zisitishwe kwa muda ili Kamati ya Uongozi ya Bunge ijadili makandokando yote ambayo yalikuwa yametokea juu ya muswada huo, ukiwamo uongo wa mwenyekiti wa kamati ya Bunge, uongo wa serikali bungeni na masuala mengine yote, ili sasa Bunge lipate mwelekeo chanya juu ya muswada huo na mchakato mzima wa Katiba Mpya kwa masilahi ya wananchi.
“Hivyo hoja yangu ilikuwa muhimu sana kusikilizwa, ili viongozi wakutane kuokoa jahazi na kuondoa sintofahamu ambayo hatimaye imesababisha mjadala mkubwa na muswada mbovu kupitishwa bungeni kwa masilahi ya upande mmoja wa CCM,” Mbowe alikaririwa akisema.
Vyanzo hivyo vilisema kuwa kama Ndugai angemsikiliza Mbowe, hakuna fujo ambazo zingeibuka bungeni. Badala yake, naibu spika huyo alitumia ubabe kumlazimisha Mbowe akae chini, na baadaye akamwitia askari wamtoe, jambo ambao wabunge wengine wa upinzani walilikataa, wakajitoa mhanga kumlinda Mbowe.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kama Ndugai angemsikiliza Mbowe, viongozi wa Bunge wangekutana na kuweka mazingira ya mjadala wenye hoja zenye afya kwa ajili ya masilahi ya Watanzania.
Vyanzo hivyo vinasema suala la Kiongozi wa Upinzani Bungeni kupewa nafasi kusema anaposimama hufanyika kwa mujibu wa kanuni ya 5(1) inayosema:
“Katika kutekeleza majukumu yake, yaliyotajwa katika ibara ya 84 ya Katiba, Spika ataongozwa na kanuni na pale ambapo kanuni hazikutoa muongozo, basi Spika atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi, kanuni zingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.”
Kwa kuzingatia kanuni hii, na kwa kuwa Bunge letu linafuata utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola (Westminster Model) ambao unatoa nafasi ya pekee kwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani anaposimama kutaka kusema jambo bungeni, makundi kadhaa ya wananchi yamekuwa yakimlaumu Ndugai kwamba alipaswa kumhukumu Mbowe baada ya kusikiliza hoja yake.
“Angempa nafasi ya kusema au kusikilizwa kwanza ili ajue kiongozi mwenzake alitaka kusema nini au alikuwa na jambo gani zito au la dharura ambalo lingeweza hata kusaidia Bunge zima, hivyo wananchi kunufaika,” kilisema chanzo kimoja cha karibu na Mbowe.
Mbowe alisema kuwa Ndugai anapaswa kuelewa kuwa bungeni ni mahali ambapo panapaswa kuheshimiwa kwa mijadala mikali, yenye hoja za afya kwa ajili ya masilahi ya wananchi, kwani moja ya kigezo muhimu katika uvumilivu wa kujadiliana ni kusikiliza, lakini hakutoa fursa hiyo kwa sababu anazozijua.
Duru za siasa zinaeleza kuwa Ndugai alilifanya kwa makusudi kumzuia Mbowe kwa sababu ya maelekezo yaliyotokana na vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vilivyoketi hivi karibuni jijini Dodoma.
Rais Kikwete njia panda
Wakati muswada huo uliopitishwa kwa maoni ya upande mmoja wa wabunge wa CCM ukisubiri kusainiwa ili kuwa sheria, Rais Jakaya Kikwete amewekwa katika wakati mgumu kusaini muswaada huo.
Ugumu huo unatokana na malalamiko mengi kutoka nje na ndani ya nchi ambayo yameelekezwa kwa CCM, kwamba imekusudia kuhakikisha inatengeneza Katiba itakayolinda masilahi yao badala ya kujali masilahi ya taifa.
Wakati wabunge wa kambi ya upinzani wakisusia mjadala na kutoka nje, wabunge wa CCM walipitisha muswada huo bila kuujadili, na bila kuzingatia hoja ya ushirikishwaji wa Wazanzibari.
Hatima ya muswada huo iko mikononi mwa Kikwete ambaye anakabiliwa na wakati mgumu kama ataamua kuusaini au kulitaka Bunge litimize kwanza hitaji hilo lililoleta sokomoko inayoweza kudhuru mchakato mzima huko mbeleni.
Kama Rais Kikwete atatumia busara kama za awali, upo uwezekano mkubwa muswada huo ukarejeshwa bungeni ili ujadiliwe baada ya kutimiza vigezo.
Ugumu huo unatokana na dhamira yake ya wazi kwamba anataka kuweka historia ya kuandika Katiba upya wakati CCM inamzunguka kwa kufanya njama za kisirisiri, kuhujumu mchakato wa Katiba Mpya kama njia ya kumkomoa Mwenyekiti wao, Rais Kikwete.
Chanzo Tanzania daima
No comments:
Post a Comment