Thursday, 23 June 2011

Tanesco yatangaza mgawo wa saa 10 kwa siku nchi nzima

 


Fundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akiwa kwenye hatua za awali za kuweka transfoma eneo la Magomeni Usalama Dar es Salaam jana.Picha na Silvan Kiwale
Waandishi Wetu
SHIRIKA la Umeme (Tanesco), limetangaza mgawo mkubwa wa umeme usio na kikomo, utakaokuwa kwa saa 10, siku saba kwa wiki nchi nzima.

Maafisa wa shirika hilo na Wizara ya Nishati na Madini wamesema mgawo huo umetokana na upungufu wa maji katika bwawa la Mtera na transfoma zake kuzalisha umeme mdogo kuliko mahitaji.Kwa mujibu wa tangazo la ratiba ya mgao huo lililotolewa na Tanesco jana, mgao huo utakuwa wa kati ya saa sita hadi 10 kwa siku ambapo maeneo yatabadilishana muda wa mgawo.

Hata hivyo, tangazo hilo la Tanesco limekuja wakati maeneo mengi nchini yakiwa na mgawo wa muda mrefu na ambao unachukua muda wa saa zaidi ya zilizotangazwa jana na shirika hilo hali iliyosababisha malalamiko kwa wananchi.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo mgawo huo utakuwa wa kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili ambapo baadhi ya maeneo yatakosa umeme mchana na mengine yatakosa usiku.Tanesco ilisema katika baadhi ya maeneo umeme utakatika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni, wakati maeneo mengine yatakosa umeme kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 5.00 usiku.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jana, Mhandisi Mkuu wa Tanesco, Juliana Pallangyo alisema mgawo huo unatokana na kupungua kwa kina cha maji katika bwawa la Mtera.

Alisema mahitaji ya umeme ni megawati 850 wakati uzalishaji ni megawati 600 hali inayochangia upungufu wa umeme.

“Mahitaji yaliyopo ni makubwa wakati umeme unaozalishwa ni mdogo, tunashindwa kumudu mahitaji ya watu wote kwa wakati mmoja na ndiyo maana tunakuwa na mgawo,” alisema Pallangyo.Aliongeza kuwa licha ya matatizo hayo shirika hilo lina malengo ya kusambaza umeme vijijini ambako bado hakujafikiwa na umeme.

Katibu adai mgawo utakuwa historia

Akizungumzia kuhusu mgawo huo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema mgawo huo unaweza kuwa historia katika miaka miwili ijayo na kwamba hali ya sasa inatokana na upungufu wa maji katika bwawa la Mtera ambalo linaweza kufungwa kwa sababu hiyo.

Katika hatua nyingine, Jairo alisema Serikali ya China itatoa mkopo wa dola za Marekani 778 milioni sawa na Sh1,167,000 bilioni, kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kufunga bomba kubwa la kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam, itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

Alisema hatua hiyo itafanyika endapo Serikali ya Tanzania itafikia makubaliano na Serikali ya China katika mazungumzo baina yao yanayotarajia kuyafanya wiki ijayo.Iwapo mpango huo utafanikiwa kampuni ya China Petrolium Company ndiyo itakayozalisha umeme.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Jairo alisema, kiasi hicho cha fedha ni kulingana na upembuzi yakinifu uliofanywa na kwamba gesi itakayozalishwa itasaidia kupunguza tatizo la umeme na uharibifu wa mazingira nchini.

Alisema bomba linalozalisha gesi kwa sasa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni dogo likiwa na ukubwa inchi 30 hivyo uzalishaji wake pia ni mdogo.“Sisi kama wizara tunajitahidi kuweka mipango ya muda mfupi ya kukabiliana na tatizo la umeme lililopo nchini kwa hiyo Serikali ya China itatupa fedha hizo kama mkopo kwa ajili ya kuzalisha gesi hiyo,”alisema Jairo.

Imeandaliwa na Raymond Kaminyoge, Timoth Marko na Elizabeth Ernest

No comments:

Post a Comment