Msaada wenu tunauthamini
Na Salma SaidMAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imevutiwa na azma ya
Jumuiya ya Ulaya (EU), kusaidia juhudi za kuimarisha sekta ya umeme nchini, kupitia vyanzo mbali mbali.
Alisema hatua hiyo italisaidia Taifa kwa kiasi kikubwa kuondokana na kadhia ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kupelekea kushuka kwa shughuli za uzalishaji.
Maalim Seif amesema hayo leo katika ukumbi wa hoteli ya kitalii ya Movenpick jijini Dar es Salaam, alipozungumza na ujumbe wa Jumuiya ya Ulaya (EU), ulioongozwa na Balozi wa jumuiya hiyo, Tim Clerk
Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo ulielezea azma ya EU ya kuisaidia Zanzibar katika uimarishaji wa nishati ya Umeme kupitia teknolojia ya kisasa, kutokana na vyanzo mbali mbali vya nishati hiyo, ikiwemo upepo, maji ya bahari pamoja na jua.
Alisema Zanzibar inahitaji kuwa na umeme wa uhakika ili kufikia lengo lake la kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kijamii nchini.Alisema kwa sasa Zanzibar inategemea zaidi umeme unaotokana na nguvu za maji kupitia waya wa chini ya bahari, ambapo kutokana na uchakavu uwezo wake wa kusambaza umeme ni megawati 40 tu ,sambamba na kuwa na Majenereta 32 yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 25, hali inayokwaza kwa kiasi kikubwa azma ya Serikali kufikia malengo ya kukuza uchumi wake.
Alianisha kuwa mahitaji halisi ya umeme ni megawati 50 lakini kutokana uzalishaji duni wa majenereta yaliopo, kiwango kinachozalishwa bado hakikidhi haja.
Aidha alisema mbali na mpango wa Shirika la Changamoto la Millenia (MCC) la awamu ya pili ya kusambaza umeme kupitia waya wa chini ya bahari unaotarajiwa kukamilika ifikapo Januari 2013, bado ipo haja ya kuwa vyanzo vyengine vya uzalishaji umeme ili kuwa na umeme wenye kutosheleza muda wote.
Maalim Seif alieleza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na EU na kuahidi kulichukulia suala hilo kwa uzito unaostahili na akisisitiza umuhimu katika uhifadhi wa mazingira wakati utekelezaji wa miradi yote inayowekezwa nchini.
Katika hatua nyingine Maalim Seif alimweleza Balozi huyo umuhimu uliopo kufuatia azma ya Serikali ya upanuzi wa Bandari ya Zanzibar kwa ajili ya mizigo eneo Mpigaduri.
Alisema hali hiyo inatokana na ufinyu wa eneo katika bandari ya Malindi, huku kukiwa na tatizo la kina cha maji kupungua kutokana na ongezeko la mchanga bandarini hapo.
Alimhakikishia Balozi huyo kuwa serikali inahamini mchango mkubwa na shughuli zote zinazoendeshwa na EU katika maendeleo ya nchi.Nae Balozi Clerk aliishauri Serikali kukaa pamoja na wadau wote wa sekta ya Umeme na kutaka utafiti wa kina ufanyike ili kuweza kufahamu uwezo, athari na gharama za uzalishaji wa umeme huo kupitia vyanzo hivyo.
Alisema Jumuiya ya Ulaya iko tayari kugharama uendeshaji wa miradi hiyo kupitia teknolojia ya kisasa ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Aidha alimhakikishia Makamu wa kwanza wa Rais kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kutoa misaada yake ya kifedha kwa ajili ya maendeleo na ukuzaji wa uchumi wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment