SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema imekuwa makini katika kuhakikiisha rasimu mpya ya mswaada inatoa fursa kwa wananchi kuzungumza mambo yote muhimu yanayohusu Muungano bila ya vikwazo vyovyote.Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari alipokuwa akijibu maswali ya wajumbe wa baraza la wawakilishi waliotaka kujua suala zima la Muungano ambao ni kero kubwa kwa wazanzibari.
Aidha Waziri huyo alisema masuala yote ya Muungano yatajadiliwa katika kipindi cha majadiliano ya rasimu mpya ya katiba ya Tanzania na kuwataka wananchi kujipanga katika kutoa maoni yao kwani maoni yao yatarahisishia serikali katika utendaji wake wa kazi.
Akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliyetaka kujua iwapo wananchi watakapotoa maoni yao nja wakasema Muungano kwao wao ni kero serikali itaheshimu maoni hayo, Waziri huyo alijibu kwamba maoni ya wananchi yataheshimiwa lakini na serikali itapima maoni hayo kwani nayo ina upande wake wa kutafakari.
“Maoni ya wananchi yataheshimiwa lakini pia wananchi nao wanatakiwa wajue kama serikali yao ina wajibu wake, na serikali inayo haki ya kuwafahamisha wananchi wake kwambamaoni haya ni sawa na maoni haya yatahatarisha hili na hili hivi ni vitu vya kuzingatiwa pia” alisema Waziri huyo ambaye ni bingwa wa fani ya sheria.
Naye katika swali lake la msingi Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani (CUF) Hijja Hassan Hijja alitaka kujuwa mambo gani ya msingi yamekubaliwa wakati utakapofika muda wa kujadili rasimu ya katiba kwa wananchi ikiwemo suala la Muungano.
Waziri Abubakar alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejifunza kwamba ni lazima mambo ya muungano ya serikali zote mbili yajadiliwe kwa uwazi katika rasimu ya katiba itakayowasilishwa kwa wananchi.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejifunza kwamba ni lazima kwa mambo ya Muungano, serikali zote mbili zishirikiane tokea mwanzo wa maandalizi wa jambo hilo vyenginevyo inaweza kusababisha kutofahamiana baina ya serikali zetu mbili. Kitendo ambacho hatukipendi” alisema Waziri huyo.
Alisema kwa kuwa msingi wa katiba ya Jamhuri ya Muungano ni Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar haikuwa sahihi kukataza kuzungumza kuwepo kwa Muungano kama vile hilo ndio jambo la msingi linahitaji kupatiwa ufumbuzi.
“Kwa kuzingatia hilo rasimu mpya ya mswaada iliyotayarishwa na wanasheria wakuu wa serikali na Zanzibar na Tanzania pamoja na watendaji wao kwa pamoja walikubaliana kuondoa sharti la kutojadiliwa kwa baadhi ya maneno muhimu wakati wa mchakato wa tume ya katiba ya kukusanya maoni” alisema waziri huyo.
Abubakar aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba wananchi wengi hawaujuwi mkataba wa Muungano wa asili amabpo mwaka 1964 mkataba wa Muungano uliorodhesha mambo 11 ya awali ikiwemo katiba ya Jamhuri ya Muungano, mambo ya nje, ulinzi na usalama, polisi na mamlaka juu ya mambo yanayohusu hali ya hatari.
Mambo mengine ni uhamiaji, mikopo na biashara za nchi za nje, utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato na ushuru wa forodha na bandari, usalama wa anga, posta na simu.
“Mheshimiwa Spika ni kweli kwamba wananchi wetu wengi hawajuwi mkataba wa Muungano wa asili ingawa nakala zake zipo nyingi. Kwa mujibu wa sheria Nam. 7 ya mwaka 1984 sheria yeyote au hati yeyote inakuwa halali kwa ajili ya matumizi ama baada ya kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali au hati hiyo au sheria hiyo kuainisha tarehe ya kuanza kwake” alisema Abubakar.
Alisema au kuanzia kwa hati hiyo imetiwa saini. Kuwepo kwa hati au sheria za asili ni suala la uwekaji wa hati au sheria husika. Hata hivyo wizara yake imeanza kuchukuwa hatua za kuhakikisha kwamba hati hiyo ya asili inapatikana.
Abubakar alisema wanasheria wa pande zote mbili wametakiwa kukutana na kuandaa rasimu ya mswaada wa sheria “Serikali ya Zanzibar kupitia mwanasheria mkuu, katibu mkuu wizara ya katiba na sheria na watendaji wengine wa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali, wamefanya vikao vinne na mwanasheria mkuu wa SMT na watendaji wake ambapo kati ya vikao hivyo vinne, vitatu vilifanyika Zanzibar na kimoja kilifanyika Dar es salaam”.
Waziri huyo alitaja baadhi ya maeneo muhimu ambayo wamekubaliana pande mbili hizo ni rais wa Muungano kuunda tume ya katiba kwa kushirikiana na kukubaliana na rais wa Zanzibar, ushauri wa kisheria katika kuunda tume uzingatie pia ushauri wa mwanasheria mkuu wa Zanzibar, na tume kuwa na idadi sawa ya wajumbe kutoka pande mbili za serikali.
Mengine ni kuondoa sharti la wajumbe kuthibitishwa na bunge, mawaziri wa katiba wa SMZ na SMT pamoja na wanasheria wakuu wa SMZ na SMT kuwa wajumbe wa bunge la katiba.
“Mheshimiwa Spika maelezo haya yataletwa kwa waheshimiwa wawaqkilishi hivi karibuni baada ya kumaliza hatua ndogo ndogo za rasimu hiyo na baada ya kupeleka taarifa hii kwa baraza la mapinduzi. Vile vile utakuwepo utaratibu wa kuwaelezea wazanziabri hatua zote za mswaada huu ulipofikia” alisema Abubakar.
No comments:
Post a Comment