Malecela apasuliwa moyo |
Habel Chidawali, Dodoma MWANASIASA mkongwe na kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Samwel Malecela ni mgonjwa na taarifa za uhakika zinaeleza kwamba amefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Uingereza. Habari za kuumwa kwa mwanasiasa huyo ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika chama tawala zilitangazwa jana na Spika wa Bunge, Anne Makinda wakati akiahirisha kikao cha bunge. “Naibu Spika (Job Ndugai) haonekani hapa kwa kuwa amesafiri, yuko Uingereza. Naye mheshimiwa Anne Kilango hayupo pia hapa kwa kuwa mzee Malecela (mume wake) anaumwa na amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kule Uingereza," alisema Spika Makinda bila ya kufafanua. Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye jana mchana mjini hapa zilieleza kuwa Malecelea alifanyiwa upasuaji huo nchini Uingereza na afya yake imeanza kuimarika. Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel aliieleza Mwananchi kuwa ofisi yake haikuwa na taarifa kuhusu kuumwa kwa Malecela kwa kuwa si mbunge tena. “Hata sisi tumesikia mle ndani (bungeni), lakini hatukuwa na habari hizo. Kwa hiyo, sina zaidi cha kueleza,’’ alisema Joel. Mmoja wa wabunge ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema jana kuwa Malecela yuko Uingereza na amefanyiwa upasuaji huo tangu Juni 14 na kwamba hali yake sasa imeanza kuimarika. “Kimsingi, mimi sijui amelazwa hospitali gani, lakini ukweli ni kwamba yuko Uingereza na alifanyiwa upasuaji Jumanne iliyopita na jana (juzi) nimezungumza na mtu wa karibu yake ambaye anasema kuwa hali yake ni nzuri. Tunamshukuru Mungu,’’ alisema mbunge huyo. Alisema kuwa Malecela alikwenda Uingereza kwa safari za kawaida ikiwa ni pamoja na kuangaliwa afya yake, lakini baada ya vipimo iligundulika kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na alitakiwa afanyiwe upasuaji mapema. Aliongeza kuwa baada ya majibu hayo, Malecela alitoa taarifa serikalini ambapo walimtumia fedha haraka na kumsafirisha mke wake (Anne Kilango) ili akamuuguze wakati amefanyiwa upasuaji. Nyumbani kwa mwanasiasa huyo, wasaidizi wake wa karibu walisema kuwa hali ya mzee huyo inaendelea vizuri. “Taarifa tulizoletewa kutoka kwa mmoja wa watu wanaomsaidia mzee, wanasema kuwa anaendelea vizuri na tuna imani kuwa Mungu atamsaidia, atapona na kurudi nyumbani haraka,’’ alisema mmoja wa watu wanaoishi nyumbani kwa Malecela,eneo la Kilimani mjini Dodoma. Malecela,77, ameshika nyadhifa kadhaa zikiwamo za uwaziri, uwaziri mkuu na mbunge kwa vipindi tofauti hadi alipostaafu siasa mwaka jana akiwa mbunge wa Mtera. Aliwahi pia kuwa makamu mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, ambako alishiriki katika kazi nyingi zikiwamo za kuwapigia kampeni wagombea wa wa chama hicho kila ulipojitokeza uchaguzi mdogo. |
No comments:
Post a Comment