Lipumba: Rushwa itamalizwa nchini kwa kukamata mapapa, sio vidagaa
Na Joyce Mmasi RUSHWA ni adui wa haki.Hii ilikuwa ahadi ya kila mwanachama wa chama cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanzania na ambayo iligeuka kuwa sehemu ya maisha ya kila mwananchi.Kwa bahati mbaya, rushwa imeendelea kuwapo na kubadilika kuwa donda ndugu lisilopona, ni ugonjwa hatari kuliko hata Ukimwi. Jambo kubwa na ambalo ni la hatari katika rushwa ni kuwa imegeuka kuwa sehemu ya maisha ya kila Mtanzania. Mtoaji au mpokeaji rushwa hafanyi hivyo kwa hofu wala kificho, anafanya kila kitu hadharani kana kwamba ni jambo la kawaida na lisilo na hatari yoyote katika jamii. Vita dhidi ya rushwa imekuwapo tangu nchi ilipata uhuru miaka 50 iliyopita, lakini haijawahi kupata suluhu au kuwa na dalili ya kuishinda. Hii inatokana na kile kinachoelezwa kuwa vita hii inabagua kwa kuwalenga maskini au wanyonge, na kuwaacha matajiri na wenye uwezo. Vita hii imekuwa ya upande mmoja. Ni vita vya rushwa dhidi ya wanyonge na maskini. Haiwagusi matajiri na wenye mamlaka, hata kama watakamatwa au kuhusika moja kwa moja na rushwa watafumbiwa macho au itaelezwa kuwa hakuna ushahidi wa kuwakamata achilia mbali kuwafungulia mashtaka na kuwatia hatiani. Kwa kuwa ni vita dhidi ya wanyonge na maskini, endapo atahisiwa mnyonge au maskini wa kipato, atachukuliwa hatua haraka ikiwemo kufunguliwa mashtaka na wengi wao wapo jela wakitumikia vifungo.Lakini, wala rushwa na watoaji rushwa wakubwa, wanapotajwa au kuhusishwa moja kwa moja na matukio ya utoaji, ulaji na wizi wa mali ya umma hufumbiwa macho na kuwapa nguvu na haki ya kujiona kuwa wenye haki ya kuendelea na mchezo huo wa kula, kutoa au kuiba mali ya umma.Kwa mtazamo wake, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anaionaje rushwa katika Tanzania? Swali kwake lilikuwa, je? harakati za kupambana na rushwa nchini zinaridhisha? Naye anajibu, “Mapambano dhidi ya rushwa yatafanikiwa tu endapo wala rushwa wakubwa wanaotajwa watakamatwa, kufikishwa mahakamani, wapatwe na hatia na kisha wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria Vita dhidi ya rushwa itaonekana ya dhati endapo haitakuwa kwa baadhi ya watu huku wengine wakiachwa kana kwamba haiwahusu licha ya kuonekana, kutajwa na kuhusishwa na matukio ya rushwa.” Profesa Lipumba anaongeza kuwa vita dhidi ya rushwa haiwezi kufanikiwa kwa maneno pamoja na kuwakamata wala rushwa wadogo huku wale wakubwa na ambao wanajulikana wataendelea kufumbiwa macho na kutafuta ushahidi dhidi ya tuhuma za rushwa zinazowakabili. Anasema taasisi zinazohusika katika mapambano dhidi ya rushwa ikiwamo Takukuru zimekuwa kimya linapokuja suala la kuwashughulikia wala rushwa wakubwa huku ikielekeza nguvu zake kwa wale wadogo na ambao sio vigogo. Anasema hali hiyo ya kuwaacha bila maelezo wala rushwa wakubwa ni doa kubwa kwa taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa na kamwe mafanikio dhidi ya vita hiyo hayawezi kupatikana achilia mbali kumalizika kwa tatizo hilo nchini. “Ukitaka kufanikiwa katika vita hii hupaswi kubagua kwa kukamata baadhi ya watu, ni vyema kupambana na kila muhusika…..hakuna mwenye kinga hapa, hata kama ni kigogo, kama anatajwa akamatwe na achukuliwe hatua, lakini hii ni tofauti hapa kwetu kwani wale mapapa wa rushwa wanaachwa na kukamata vidagaa, hii ni hatari na tusitegemee mafanikio katika vita hiii, ”anasema Prof Lipumba. Anaongeza kuwa rushwa imekuwa sehemu ya maisha kwa Watanzania wengi na haionekani kuwatisha watu kama enzi za Mwalimu Julius Nyerere na akasema hii inatokana na udhaifu wa viongozi waliopo madarakani. Anasema mafanikio katika vita dhidi ya rushwa yanapaswa kwenda sambamba na uadilifu kwa viongozi wote ambao anasema ndicho kiini cha tatizo lenyewe. “Watu hawana woga wa kudai au kupokea rushwa, kila sekta, katika mahakama, polisi, kote kunanuka rushwa,…uadilifu hakuna tangu kwa kiongozi, mpaka kwa wafanyakazi wanaowaongoza, na hii inasababishwa na mazingira yaliyopo sasa ambapo hakuna mwenye hofu ya kukamatwa wala kushitakiwa,” anasema Prof Lipumba anasema kiini cha kuzidi kudorora kwa vita dhidi ya rushwa, kinachangiwa na ukimya wa makusudi unaofanywa na taasisi zinazohusika na mapambano hayo hasa katika kuzishughulikia rushwa kubwa zinazoelezwa kutikisa uchumu wa nchi. “Kampuni iliyoanzisha utaratibu wa kuchota fedha za EPA ni Kagoda Agricultural Ltd, lakini ni jambo la kushangaza sana ni kuona mpaka leo hii wahusika hawajakamatwa, achilia mbali kufikishwa mahakamani…..kesi nzito nzito zimefumbiwa macho, hazishughulikiwi tena….kwa utaratibu huu huwezi kupata mafanikio, Unapozungumzia rushwa unapaswa kuanza na watuhumiwa na tuhuma kubwa kubwa kama hizo, hii itaondoa maswali yaliyojaa kwa wananchi kuhusiana na umakini wa taasisi zinazohusika katika vita hii” anasema.Akizungumzia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Prof Lipumba anaibeza akieleza kuwa inaonekana inafanya kazi zake kisiasa na kupoteza uwezo na imani kwa wananchi. “Takukuru haiaminiki tena, imepoteza credibility (uaminifu), inaonekana kufanya kazi zake wakati wa kura za maoni za chama tawala, CCM, lakini wakati wa uchaguzi mkuu ambao matukio ya rushwa yalikuwa nje nje, hawakuonekana kabisa, hata pale wagombea wa nafasi mbalimbali katika vyama vya upinzani, walipopeleka taarifa za matukio au vitendo vya rushwa hawakusikilizwa, kujibiwa wala kufanyiwa kazi” anasema.Anasema kutokana na hali hiyo, imani ya Watanzania dhidi ya taasisi hiyo inaendelea kupotea, jambo analosema ni hatari na itachangia kudumaza vita hivyo vinavyolitikisa taifa. Je, ana maoni gani kwa serikali katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa, Profesa lipumba anajibu, “Ushauri wangu ni mmoja, umakini na nia ya dhati unahitajika katika kupambana na rushwa….hakuna haja ya kufumbia macho baadhi ya watu kwa sababu zozote, wote wanaohusika, na wanaotajwa wachukuliwe hatua sawasawa tena kwa uwazi Sidhani kama kusingekuwa na woga kwa vidagaa kujitanua endapo wale mapapa wanaotajwa waziwazi wangekamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.” |
No comments:
Post a Comment