Monday, 27 June 2011


Gaddafi sasa kukamatwa 
 
                                                          Kanali Muammar Gaddaf


 
Mwandishi wetu na Mashirika
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), imetoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, akituhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu dhidi ya raia wake.Hati hiyo imetolewa na majaji wa mahakama hiyo jana, wakati ambao oparesheni za Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (Nato) dhidi ya kiongozi huyo zikitimiza siku 100 bila kufanikiwa kumuondoa madarakani.

Pamoja naye, hati hiyo imemjumuisha pia washirika wake wakuu akiwamo mwanaye Saif al-Islam na Mkuu wa Ujasusi wa Libya, Abdullah al-Senussi wote wakituhumiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Hatua hiyo ya majaji hao wa ICC inatokana na ombi lililofikishwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Luis Moreno Ocampo ambaye alidai kwamba watatu hao wanahusika kuamuru na kusimamia mauaji ya waandamanaji walioibuka kutaka kuondoka madarakani kwa Kanali Gaddafi ambaye ameshaitawala Libya kwa miaka 41 sasa.
Hati hizo za kukamatwa kwa watatu hao ziliombwa na Ocampo mwezi Mei, akisema watu hao walihusika na "mashambulio yaliyopangwa na yaliyosambaa" kwa raia.Ocampo alisema mahakama hiyo ina ushahidi kuwa Kanali Gaddafi "aliamuru binafsi mashambulio kwa raia wa Libya wasio na silaha na alihusika kwa kukamatwa na kunyanyaswa kwa wapinzani wake wa kisiasa.

Gadaffi ni kiongozi wa pili wa nchi, barani Afrika ambaye bado yuko madarakani kutakiwa kujibu tuhuma katika ICC akimfuatia kiongozi wa Sudan, Omar Al Bashir ambaye hati yake ilitolewa Julai 14, 2008.

Hata hivyo, kiongozi huyo hajawahi kukamatwa hadi leo na viongozi wa nchi za Afrika wamegawanyika kimsimamo kuhusu kukmatwa kwa Al Bashir ambaye nchi yake imegawanywa kufuatia Sudan ya Kusini kuamua kujitenga rasmi ifikapo Julai 1, 2011 mpango ambao una baraka za jumuiya ya kimataifa.

Kama ilivyo kwa Al Bashir, suala la kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwa Gaddafi linaweza kuvigonga vichwa vya wakuu wa nchi na Serikali za Afrika, ambao tangu mwanzo kupitia Umoja wa Afrika (AU), walionyesha msimamo wa kumuunga kiongozi huyo, wakitoa mwito kwa Nchi za Magharibi kusitisha mashambulizi nchini Libya.

Maandamano nchini Libya dhidi ya Kanali Gaddafi yalianza Februari mwaka huu, baada ya maandamano ya aina hiyo kufanikisha kuwaondoa madarakani Rais aliyetawala kwa muda mrefu nchini Tunisia, Albedine Ben Ali na baadaye aliyekuwa Rais wa Misri, Hosni Mubarak.Akitoa uamuzi huo, Jaji Sanji Mmasenono Monageng aliyeongoza jopo la majaji walioidhinisha hati hiyo alisema Kanali Gaddafi anayo “mamlaka kamili isiyohojiwa” katika dola ya Libya na vikosi vyake vya usalama ambavyo amekuwa akivitumia atakavyo.
Jaji huyo aliongeza kuwa Kanali Gaddafi pamoja na mwanaye, Saif al-Islam “walipanga na kusimamia kwa nanma zote mikakati ya kuzuia maandamano ya raia” dhidi ya utawala wake na kwamba mkuu wa ujasusi, al-Senussi alitumia nafasi yake kuamuru mashambulizi dhidi ya raia waliokuwa wakiandamana.
Hata hivyo, Serikali ya Kanali Gaddafi imekuwa ikikanusha kuhusika na mauaji ya raia na kuzituhumu ndege za Nato ambazo zimekuwa zikiendesha mashambulizi yake nchini Libya kwa kile kinachotajwa kuwa ni kusimamia utekelezaji wa azimio la UN la kuwalinda raia kwa kuzuia ndege za kivita za majeshi ya Kanali Gaddafi kuruka katika anga ya Libya, akisema ndizo zinazotekeleza mauaji hayo ya raia.
Pia, hati hiyo imetolewa wakati Serikali ya Libya hivi karibuni ikiwa imeshaeleza kwamba haitambui mahakama hiyo ya ICC na suala la uamuzi wowote kuhusu kutolewa kwa hati hiyo haliwashughulishi.
Wakati majaji hao wakitoa uamuzi wa kutaka Kanali Gaddafi akamatwe na kufikishwa kwenye mkono wa sheria, Shirika la Habari la Serikali ya Tunisia, TAP lilieleza kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Abdelati Obeidi yupo katika visiwa vya Djerba Kusini mwa Tunisia akifanya majadiliano na washirika wao wa nje.

Uingereza wazungumza
Akizungumza muda mfupi baada ya kutolewa kwa hati hiyo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague alisema amefurahishwa na uamuzi huo wa majaji kwa kuwa watuhumiwa hao wanatakiwa kuwajibika kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu ambao wamekuwa wakiusimamia.“Uingereza itaendelea kuiunga mkono ICC kwa namna zote na inaitaka Serikali ya Libya kutoa ushirikiano wa kutosha katika uchunguzi wa ICC,” alisema Hague.

“Hati hiyo inaonyesha namna Gaddafi alivyopoteza uwezo wa kutawala na inaonyesha sababu za kumfanya aondoke haraka madarakani. Vikosi vyake vimeendelea kuwashambulia raia wa Libya bila huruma, vinatakiwa viache mara moja,” aliongeza.

Hague alisema pia kwamba wapo watu katika utawala wa Kanali Gaddafi ambao hawana budi kumtosa na kwamba wanawapongeza wale walioamua kujitoa katika Serikali yake tangu awali akiwaelezea kwamba wanatoa historia mpya ya mashujaa waliokataa kugeuka dhidi ya watu wao.



No comments:

Post a Comment