Wednesday, 9 March 2011

Vita dhidi ya waasi vya chacha Libya

Ras Lanuf
Jumuiya ya kimataifa inataka marufuku ya ndege kupaa Libya iwekwe
Wanajeshi wanaomtii kwa kiongozi wa Libya Kanali Muamar Gaddafi, wameshambulia mji wa Zawiya ulioko magharibi mwa nchi hiyo kwa makombora.
Mmoja wa wakaazi wa mji huo aliyefanikiwa kutoroka amesema ameona vifaru hamsini pamoja na magari ya kijeshi yakiwa yamewabeba wanajeshi wanaomuunga mkono kanali Gaddafi.
Hospitali kuu imeripotiwa kuzidiwa na idadi kubwa ya majeruhi.
Mashariki mwa Libya, waasi walioko katika mji wenye utajiri wa mafuta wa Ras Lanuf , wameshambuliwa kutoka angani na makombora.Watu wasiopungua thelathini wamejeruhiwa.
Wakati huo huo waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani Hillary Clinton amesema kuwa uamuzi wowote wa kupiga marufuku ndege kupaa katika anga ya Libya unastahili kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa na wala sio Marekani.
Amesema ni muhimu hatua hiyo ionekane kuwa imetoka kwa raia wa Libya na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na wala sio chagizo la Marekani.
Bi. Clinton kadhalika amekariri wito wa serikali ya Marekani kumtaka Kanali Gaddafi ajiuzulu kwa njia ya amani, lakini akaonya kuwa mzozo uliopo nchini Libya huenda ukadumu kwa kipindi kirefu.

No comments:

Post a Comment