Vifo vya wasanii Five Star: Watano wazikwa giza totoro |
*Vilio vya tawala Temeke Na Victor Mkumbo, Mtoni MIILI ya wasanii 13 wa bendi ya muziki wa taarab nchini ya Five Stars waliopata ajali ya gari mkoani Morogoro usiku wa kuamkia jana iliwasili jana usiku na baadhi yao kuzikwa usiku huo huo kutokana na kuharibika vibaya.Miili hiyo iliwasili jana saa 2 usiku ikiwa katika malori matatu ikitokea mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi ambayo yalifanyika jana na wengine kuzikwa leo katika maeneo mbalimbali. Miili hiyo ilipowasili katika Ukumbi wa Equator Grill, ilishuhudiwa na umati wa mashabiki wa muziki huo, wadau na baadhi ya ndugu wa marehemu hao. Miili hiyo ilipakiwa katika malori hayo kwa msaada wa usafiri kutoka Morogoro pamoja na kuhifadhi maiti hao ambao ulitolewa na Mbunge wa Morogoro, Abdulaziz Mohamed Abood. Hata hivyo, ulizuka utata kwa baadhi ya ndugu wa marehemu kulalamikia kuchukulia miili hiyo katika eneo la Equator kutokana na kuwa eneo hilo kuwa sehemu ya kuuzia pombe wakidai kuwa kutokana na imani yao ya Kiislamu, siyo vizuri kuchukulia maiti katika eneo kama hilo. Akizungumza na Dar Leo jana usiku, mratibu wa mazishi, Hamisi Kajumulo, amesema wanashukuru kumaliza salama kutokana na utulivu uliokuwapo wakati wa kuchukukua miili ya marehemu. Amesema kutokana na baadhi ya miili kuharibika, maiti watano walilazimika kuzikwa na wengine mazishi yao yatafanyika leo katika maeneo mbalimbali. Amezitaja maiti zilizozikwa jana usiku kuwa ni pamoja na Husna Mapande, Tizo Mgunda, Issa Kijoti, Hamisa Mipango na mhasibu wa bendi, Nassor Madenge. Alisema maiti watakaozikwa leo ni pamoja na Sheba Juma, Omary Hashim, Ramadhan Kinyoya, Omary Tall, Haji Babu, Tamir Maulid, Hassan Ngeleja na Mimuna Makuka ambaye alikuwa mnenguaji katika kikundi cha Kitu Tigo. “Tunashukuru kwa kumaliza kupokea maiti zote bila kikwazo ambapo pia ndugu wa marehemu wameweza kuzichukua kwa utulivu mkubwa bila kipingamizi chochote kwa ajili ya mazishi … Lakini pia tunawashukuru ndugu wa marehemu kwa kuwa waelewa kutokana na kutaka kugomea kuchukua miili kwani ilifikia katika eneo ambalo imani yao haikuliani nalo,” alisema Kajumulo. Aliongeza kusema: “Tulijaribu kuwaelewesha wale walioanza kuleta utata kwa kutaka kugomea kuchukua miili ya marehemu katika eneo hili kutokana na imani za kidini ila ilibidi tuchukue muda kuwaelimisha na baadaye walikubaliana na sisi kuwa hili ni tukio la kushtukiza, hivyo hatukuweza kuandaa eneo jingine zaidi ya hapa ambapo ilikuwa kambi yao kubwa,” alisema Kajumulo. Naye Mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi nchini ya The African Stars Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema katika tasnia ya muziki wa taarab wamepata pengo kubwa ambapo kuliziba itachukua muda mrefu. Amesema wamepoteza watu maarufu katika muziki huo hivyo ni vigumu kupata watu wanaofanana na wale waliopata ajali kwa ajili ya kuziba nafasi zao. Amesema kupeteza maisha kwa wasanii hao kutafanya muziki huo kutokuwa na ladha kutokana na ushindani uliokuwepo kati ya Five Stars na Jahazi. “Tumepoteza watu muhimu katika muziki wa taarab na pengo lao halitazibika mapema na ushindani katika muziki huo utakuwa mdogo sana kutokana na kupeteza wasanii wengi kwa wakati mmoja, tunaomba tutoe ushirikiano wa kutosha kwa ajili ya kuwapa moyo na kuwafariji ndugu wa marehemu,” alisema Asha. Amesema wasanii ifike muda wawe na ushirikiano wa kutoleana michango katika majanga makubwa hasa ya misiba ili kuweza kurahisisha mambo mbalimbali yanayoweza kujitokeza na kuyatatua mara moja. Wasanii hao walikufa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia jana baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali eneo la Doma mkoani Morogoro na kuua wanamuziki 13 papo hapo. Ajali hiyo ilitokea baada ya gari walimokuwa wakisafiria kuligonga kwa nyuma lori lenye shehena ya mbao lililokuwa limesimama maeneo ya kijiji cha Doma, mpakani mwa mbuga ya wanyama ya Mikumi, Kilosa mkoani Morogoro. |
No comments:
Post a Comment